Utangulizi
Tanzania League of the Blind (TLB) ambao ni Chama cha watu wenye ulemavu wa macho kiliendesha mradi wa utetezi kwa watu wenye ulemavu. Mradi ulifadhiliwa na shirika la Foundation for Civil Society (FCS) na kutekelezwa wilayani Kwimba kilometa 85 kutoka jijini Mwanza. Pamoja na malengo mengine mradi ulijikita kuwasaidia watu wenye ulemavu kujikwamua na kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo.
Ushirika kwenye uwezeshaji
Umakini na mafinikio ya mradi huu umetokana na ushirishwaji wa wadau muhimu katika utekelezaji kwa mfano, Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) na Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi (TAS) wilayani Kwimba. Mdau mwingine muhimu ni serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Kwimba hasa Idara ya Maendeleo ya Jamii. Akizungumza kuhusu ushirikiano huu Ndugu Isaac Malumbu ambaye ni katibu wa TLB Kwimba alisema; ‘‘Mbinu zetu zote kwenye mradi zimekuwa shirikishi kwenye utetezi, mafunzo na uhamasishaji’’.
Jinsi vikundi vilivyowakwamua walemavu
Kwa kushirikina na idara ya maendeleo ya wilaya ya Kwimba TLB ilihamasisha walemavu kujiunga kwenye vikundi ili vipate mikopo ya kufanyia biashara katika halmashauri. Jumla ya vikundi 14 vilianzishwa kutoka katika kata 10 za wilaya ya Kwimba.Wanachama wa vikundi hivi walielimishwa jinsi ya kuanzisha biashara , jinsi ya kutunza fedha na kusajiliwa rasmi.
Mpaka sasa vikundi vyote 14 vimepatiwa mikopo kutoka mfuko maalumu ulioanzishwa kupitia sheria ya fedha serikali za mitaa inayotaka asilimia 2 ya mapato ya halmashauri kutengwa kwa ajili ya mikopo ya watu wenye walemavu.
Kikundi cha Kazi na Maendeleo kilichopo kijiji cha Malemve wilayani Kwimba ni moja ya vikundi vilivyofaidika na mikopo hiyo. Kikundi kina jumla ya wanachama watano kati yao wawili ni walemavu wa macho na watatu ni walemavu wa viungo. Kikundi hiki kimepata mkopo mara mbili. Kikundi hiki kimerejesha malipo ya mkopo wa kwanza wa shilingi milioni moja na sasa wamekopeshwa tena shilingi milioni moja . Ndugu Cosmas Stanley Katibu wa kikundi alikuwa na haya ya kusema;
‘‘Tunashukuru kwa kupata mikopo hii miwili ambayo imetuwezesha kuanzisha na kupanua biashara yetu na kuwa kubwa zaidi. Kabla ya biashara hii, maisha yetu yalikuwa magumu na tulipata changamoto kubwa mbili; Moja , tulikuwa hatuna uwezo wa kiuchumi na tulitegemea kufanya kazi ngumu zisizoendana na hali zetu (ulemavu). Pili, tulionekana wategemezi kwenye jamii yetu na tusioweza kujipatia mahitaji muhimu’’. Aliongeza kwa hisia; ‘‘Hali ni ilikua ngumu sana kwetu.’’
Kabla ya mradi, wanakikundi walikuwa wanapata pesa kiduchu zisizomudu kuwawezesha kupata mahitaji muhimu ya kwao binafsi na familia zao. Shughuli zao za biashara kwa sasa zinaunafuuu mkubwa katika kuzifanya kuliko kazi za mwanzo ambayo walilazimika kufanya ikiwemo kazi ya kuponda kokoto za ujenzi ambayo ni ngumu sana. Sasa wananunua mazao kama dengu, mtama, mahindi, mchele, choroko, maharage mabichi na viazi vikavu kutoka kwa wakulima wadogo na kuuza kwa wafanyabiashara wakubwa. Na mara nyingi mazao haya huletwa na wakulima wenyewe kwenye jengo la ghala lao hivyo kurahisisha ukusanyaji na gharama.
Nje ya jela na Kuondokana na umaskini
Mradi huu umesaidia na kuwapa nafasi watu wenye ulemavu kuepukana na majanga mengine mfano bwana Kahindi Masingija mmoja ya wanakikundi anasema; ‘‘Nina watoto sita na mwanzoni ilikuwa ngumu kuwapatia chakula na kuwapeleka shule. Ugumu wa maisha ulinilazimisha pamoja na kuwa mlemavu wa macho kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya aina ya bangi ili kusaidia familia yangu. Matokeo ya kazi hiyo yalinisababisha mimi kukamatwa na polisi, kushitakiwa na kufungwa jela kwa miezi saba. Nilijisikia vibaya na matokeo haya.’’
Aliongeza; ‘‘Nashukuru tangu nijiunge na kikundi hiki sifanyi biashara hizo haramu kwani sasa napata kipato halali kwa sababu niliweka pesa tunazogawana kwenye biashara ya kikundi na kufungua duka langu dogo lililoniongezea kipato.’’
Kipato kimeongezeka.
Pia kwenye mikopo hii kuna watu wenye ulemavu waliopata mkopo binafsi mathalani bwana Laurent Semando wa Ngudu, Kwimba Alisema; ‘‘Nilikuwa nahitaji pesa za kupaongeza biashara yangu ili nikidhi mahitaji ya bidhaa za ngozi hapa Ngudu na maeneo ya karibu kwa bidhaa kama viatu vya shule, mikanda, na viatu vya wazi.Nilisikia kuhusu mikopo hii niliwashawishi wenzangu tuunde kikundi tupate mikopo hii lakini wengi waliogopa na kukataa .Nikaamua kwenda mwenyewe. Kwa msaada wa shirika la TLB na afisa maendeleo Bi. Rosalia Magotti nilifanikiwa kupata mkopo.
Bwana Laurent alipewa mkopo wa shilingi Millioni 1 na laki 8 ( uliomsaidia kuongeza mtaji wa biashara yake. Aliweza kununua ngozi, vigongo, gundi, na uzi na kusaidia kulipia gharama za kupangisha. Kipato chake kimeongezeka zaidi kwani sasa anaweza kutengeneza jozi sabini za viatu kutoka jozi 30 za mwanzo. Na kila jozi huuzwa kwa shilingi elfu thelathini ambapo anapata faida ya shilingi elfu kumi na tatu na sasa anapata shilingi laki tano kwa mwezi.
Watu wenye ulemavu waneemeka na milioni 18
Jumla ya shilingi milioni 18 zimetolewa na kukopeshwa kwa watu wenye ulemavu wilayani Kwimba akizungumzia hilo Bi Rosalia Magotti alisema; ‘‘Tumeshirikiana na TLB kuwahamasisha watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hii na vikundi 14 vimeanzishwa katika kata 10. Na jumla vikundi hivi vimepata mikopo ya kiasi cha shilingi 18,151,112/-.Aliongeza;‘‘Vikundi vilivyonufaika ni vile vilivyo sajiliwa ambapo wana katiba, akaunti ya benki na wameweka pesa kidogo za kianzio.
Mafinikio yameanza kuonekana kwani vikundi zilivyokopa zimemeshaanza kurejesha mikopo yao. Inaonesha ya kuwa watu wenye ulemavu si wategemezi na wanaweza kujitegemea kama mradi huu ulivyoonyesha.