Wasaidizi wa kisheria wanavyopunguza migogoro ya ardhi Morogoro

Ingawaje watu wengi wanamiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, lakini sio wengi wanaozifahamu sharia zinazofungamana na umuliki huo wa ardhi. Hali hii imesababisha migogoro mingi ambayo ambayo ina changamoto zake katika kuitatua. Mkoani Morogoro, asasi isiyo ya kiserikali ya Kituo cha Wasaidizi wa Sheria kwa kufadhiliwa na Taasisi ya FCS inatekeleza mradi unaojishughulisha na utatuzi wa changamoto hiyo.

Katika kijiji cha Mngazi, matukio yanayotokana na migogoro kuhusu umiliki wa ardhi yalikuwa matukio ya kawaida kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa Ndugu Octavian Kobelo ambaye ni Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, kabla ya kuanza kuutekeleza mradi huo ofisi yake ilikuwa ikishughulikia kesi sita hadi saba kwa siku licha ya zile alizozipeleka kwenye baraza la kata. Migogoro hii ilisababisha muda mwingi kupotea vadala ya kushughulikia masuala ya maendeleo. Lakini changamoto hizi zilikuzwa kutokana na ukweli kuwa idadi kubwa ya wananchi hawakuwa na hakimiliki za kimila kwa ardhi waliyokuwa wakiimiliki.

Ili kutatua changamoto za ardhi, asasi ya Wasaidizi wa kisheria iliingilia kati kwa kufanya shughuli mbalimbali. Kwanza walitoa mafunzo kwa wahamasishaji na kutoa elimu kwa wananchi 15 na viongozi wa serikali ya kijiji kuhusu umuhimu na mchakato wa kupata haki miliki ya kueasimishwa ardhi.

Wahamasishaji waliopata mafunzo walitembea nyumba kwa nyumba kutoa elimu kwa wanakijiji wenzao kuhusu umiliki wa ardhi na hasa changamoto wanazokabiliana nazo wanawake katika mchakato mzima wa kumiliki ardhi.

Kama wasemavyo wahenga, mwanzo ni mgumu na ndivyo ilivyokuwa kwa wakazi wa kijiji cha Mngazi. Baadhi ya wananchi walipinga suala hilo lakini baada ya muda, walianza kukubali wazo hilo lililotokana na elimu kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi kisheria.

Hadi mwezi Machi 2018 asasi hiyo ilikuwa imeshawapa hati za kumiliki ardhi wanakijiji 100. Ndugu Shaaban Kimwaga, mwenyekiti wa kijiji hicho alisema elimu waliyoipata na uhamasishaji uliofanyw aumewasaidia sana kubadili msimamo wa wananchi wake. Siku hizi, idaid ya mashauri au kesi zinazofikishwa kwenye ofisi ya kijiji ni kati ya moja na mbili tu.

Msimamo kuhusu umiliki ardhi miongoni mwa wanawake sasa umebadilika. Awali, wanaume walishindwa kabisa kuwaamini na kuwaruhusu wanawake kuandikisha majina yao kwa ajili ya kupata haki miliki, jambo ambalo lilisababisha wanaume wengi kuwafukuza wake zao pasipo kuwapa haki ya kuwa na kipande cha ardhi. Mwanadada Sinahamu Swala, mmoja wa wahamasishaji waliopagtiwa mafunzo na asasi ya Wasaidizi wa sheria alizimulia hivi: “Sababu iliyonifanya nijihusishe na mradi huu ni kutokana na kuona jinsi wanawake walivyokuwa wakinyimwa haki ya ardhi na ukatili waliofanyiwa katika harakati za kudai haki hiyo ya kumiliki ardhi”.

Mwenyekiti wa kijiji, Mzee Shaaban anathibitisha kuwepo kwa mabadiliko hayo. “Siku hizi mwanaume na mwanamke wanakuja ofisini kwangu kuanza mchakato wa kupata hati ya kumiliki ardhi. Pale mwanaume alipokuja peke yake kutaka apewe hati, sisi tulimshauri aje na mkewe”.

Wimbi hili la mabadiliko ya wanawake kuanza kumiliki ardhi lilipigiwa upatu sana na shauri la Binti Asha Ali Kitogo, mama wa watoto wawili ambaye alilazimika kuachana na mumewe na kupeleka shauri lake Mahakama ya Mwanzo . Baada ya kushinda shauri lake kwenye mahakama hiyo, mumewe waliyeachana nae aliamua kumshitaki kwenye Mahakama ya Wilaya. Ndipo Asha alipoomba msaada wa kishera kutoka kwa asasi ya Wasaidizi wa kisheria, wamakijiji cha Mngazi waliopatiwa mafunzo na viongozi wa seirkli ya kijiji. Katika mahakama hii ya wilaya, mama huyo alishinda pia na mumewe kuamriwa apewe ekari tatu, shilingi milioni moja, baiskeli mbili na nyumba.

Elimu na uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi kulikofanywa na wafanyakazi wa kujitolea akiwemo Sinahamu, umetoa hamasa kubwa kwa wanakijiji kuamua kuchanga fedha ili kujenga Ofisi ya Baraza la Ardhi itakuwa inakutana.

Kisa hiki ni uthibitisho wa matokeo ya utoaji elimu katika kusaidia kutatua changamoto za umiliki ardhi. Mradi huu uliofanywa na asasi ya Wanasheria Wasaidizi wa Morogoro sio tu kwamba umepunguza migogoro ya ardhi lakini pia imesaidia sana maendeleo ya wanawake katika kumiliki ardhi na ushirikishwaji wajamii katika maendelo.