Wanakijiji waamua kusimamia maendeleo yao wilayani Kilolo

Kilimbwa ni kijiji cha ndanindani sana kwenye Kata ya Ibumu wilayani Kilolo mkoa wa Iringa. Ni kijiji kidogo na kipya cha umri wa miaka 10 hivi, lakini kinachokua kwa kasi sana. Wakazi wake wanaongezeka pia.

Wanakijiji wa Kilimbwa wameshaomba sana shule kwa ajili ya watoto wao. Watoto wao wanakwenda mwendo mrefu kuhudhuria shule katika vijiji vya jirani.

Siku moja, baada ya kuomba na kutoa taarifa sana waliamua kujenga wenyewe shule kwa ajili ya watoto wao; kwa mikono yao na rasilimali wanazoweza kupata hapo kijijini. Hii ni hadithi yao. Hadithi ya mabadiliko. Ushuhuda wa jinsi jamii moja ilivyoamua ni heri mara elfu kutatua changamoto zao wenyewe badala ya kukaa tu na kulalamika kwa serikali.

Hadithi hii inatokana na maamuzi ya wananchi kuamua kutenda; kuweka juhudi za kutatua matatizo yao wenyewe. Na chanzo cha maamuzi haya ya wanavijiji ni kampeni madhubuti za kuhamasiaha na kuwafunza wananchi umuhimu wa kujua na kushiriki kwenye michakato ya maendeleo yao. Na kwa sehemu kubwa mabadiliko haya yanatokana na jitihada za asasi za kiraia.

Jamii za vijijini ndio hujenga sehemu kubwa zaidi ya nchi ya Tanzania. Na kwa kuwa vijiji ndio moyo wa jamii za vijijini, basin ni sahihi kusema vijiji ndio vinashikilia jamii ya Tanzania. Na pia mabadiliko yeyote chanya kwenye vijiji yanatoa picha ya mwelekeo wa Taifa, au sehemu kubwa yake.

 

Jamii inayohangaika

Wanakijiji wa Kilimbwa hawakuwahi asilani kuona umuhimu wa uwajibikaji kwenye uongozi wa kijiji chao na wala jinsi wanavyofanya maamuzi kuhusu jamii nzima. Hawakujua haki zao wala umuhimu wa kushiriki, kuhoji na kuhusika na mipango na maamuzi ya maendeleo yao.

Viongozi wao wanatoa ushuhuda. “Tulikua na changamoto kubwa ya uwajibikaji hapa. Uongozi haukujali wananchi wake na wananchi nao hawakuona shida yeyote. Hakukua na uwazi kuhusu maamuzi na vipaumbele. Viongozi walijiona ndio kila kitu” anasema Bw Sethi Mnyamoga, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilimbwa.

Anasema hiki kilikua kipindi kibaya sana kwa jamii yao. Kulikua na maamuzi mabaya na matumizi mabaya ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi. “Hakuna kilichokua kinakwenda sawa sawa. Tulikua tumekwama sehemu mbaya sana.” Anaongeza Mtendaji Bw Majaliwa Nyalusi.

AZAKI zaingilia kusaidia

MMADEA ni moja ya asasi za kiraia (AZAKI) zinazofanya miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Iringa kwa sasa. Walifanya tathmini ya hali halisi katika jamii za Kilolo na kuamua kutafuta rasilimali fedha za kutafuta suluhisho kwa changamoto za jamii zilizopo.

Katika miaka miwili iliyopita walipata ruzuku na uwezeshaji kutoka taasisi ya Foundation for Civil Society ili kubadili ukosefu wa uelewa na ushiriki wa wananchi kwenye maamuzi, mipango na bajeti za harakati za maendeleo. Changamoto kubwa waliokua nayo ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wana uelewa wa msingi kuhusu masuala haya muhimu kwa ajili ya mchakato wa maendeleo ya kijiji. FCS ni moja ya wawezeshaji wakubwa sana wa AZAKI kupitia ruzuku na huduma za kujenga uwezo nchini Tanzania. Wameshafanya hivi kwa zaidi ya miaka 18 sasa wakifikia asasi zaidi ya 5,700 Bara na visiwani Zanzibar.

MMADEA na wataalam wao waliweka kambi katika jamii za Kilolo na kuendesha kampeni za kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya msingi ya mipango, maamuzi na bajeti za maendeleo. Walilenga viongozi wa jamii, wananchi na pia kuwaunganisha na wataalam wa serikali toka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo. Kampeni hizi zilifanyika katika vitongoji, vijiji na Kata mpaka Halmashauri ya Wilaya.

Kipaumbele ni elimu

Baada ya kampeni zenye mafanikio sana, iliwachukua wanakijiji wa Kilimbwa miezi kadhaa tu kutoa maamuzi kwa sauti moja kuwa kipaumbele chao kilikua ni elimu kwa watoto wao. Katika masuala mengi waliyojadili waliona hakuna lililo muhimu zaidi ya kuwapatia watoto wao shule kijijini kwao badala ya kuwaona wanahangaika kwenda vijiji jirani kuhudhuria shule.

Walipanga kwa pamoja na kutekeleza kwa umoja ujenzi wa shule yao ya msingi pale Kilimbwa. Kila mwanakijiji alishiriki kupitia michango na nguvukazi. Katika kipindi kifupi walijenga matanuru mawili ya kufyatulia matofali ya kuchoma kwa ajili ya ujenzi wa darasa na ofisi ya walimu. Hawakuishia hapo.

Walijenga pia madarasa manne na choo cha walimu. Walifyatua jumla ya matofali 102,500 zenye thamani ya Shilingi milioni 20 kwa kutumia matanuri yao ya umoja. Matofali haya yalitumika kwenye miradi ya ujenzi mpaka kwenye lanta. Hapa walikwama na kwa sasa wanahangaika kutafuta fedha za kupaua madarasa haya mapya. Pia walichangia matofali 20,000 zenye thamani ya Shilingi milioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata ya Ibomu.

“Baada ya kufanikiwa kujenga darasa moja, sasa hivi tuna hamu ya kufanya mengi kwa ajili ya kijiji chetu. Na ndio kwanza tumegundua uwezo wetu kama wananchi. Tumeachana kabisa na tabia ya unyonge wa kulialia na kusubiri kila kitu toka serikalini. Kwa sasa tukihitaji kitu tunajadili, tunapanga na tunaanza kuchangia kwa nguvu zetu mpaka pale tutakapokwama. Ndio tunaomba msaada wa serikali” anasema Bw Nyalusi.

Safari bado ndefu

Wananchi wa Kilimbwa bado wana safari ndefu kujikwamua kimaendeleo. Wana mipango mingi baada ya kugundua uwezo wao kama wananchi. Lakini kama jamii yeyote, wanatingwa na vikwazo vingi. Viongozi wa kijiji wanakiri kuwa bado kuna baadhi ya wananchi wanaohitaji kusukumwa muda wote ili kushiriki kwenye michakato ya maendeleo ya kijiji. Na pia wengine wanahitaji mafunzo na kuhamasishwa mara kwa mara ili washiriki. Lakini changamoto kubwa zaidi hutoka kwa wanasiasa nje ya kijiji.

“Kuna kipindi tulikua tunajenga nyumba ya walimu. Tukachanga na kuweka juhudi zetu. Tulipofika kwenya lenta kuna mwanasiasa mmoja wilayani kwetu akatuahidi kuchangia kupaua. Tukafurahi na wananchi wakaacha kuchangia. Huyo mwanasiasa mpaka leo hii hajatimiza ahadi yake na tumebaki na jengo halijamaliziwa” anasema kwa huzuni Bw Sethi.

Hata hivyo, kwa jamii ambayo imeshapata ufunguo wa hamu na uwezo wao kushiriki kuchangia maendeleo yao hiki kikwazo kinaonekana kidogo sana ukilinganisha na uboreshaji maisha yao.