Wakurugenzi wa AZAKi: AZAKi ziko imara na zina umuhimu kwenye

AZAKi zinatoa Wito wa Ushirikishwaji wa Makundi yaliyopo  Pembezoni kwenye Uchaguzi ujao

Asasi za Kiraia (AZAKi) zinakuza ushiriki wa wananchi na uwajibikaji kwenye michakato ya uchaguzi kwa kufanyakazi na mamlaka za uchaguzi na wadau wake ili kuimarisha demokrasia.

Haya yalisemwa wakati wa majadiliano kwenye Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKi waliokuwa wakijadili  mada inayohusu  Jukumu la Asasi za Kiraia kwenye Uchaguzi wa Kidemokrasia. Hafla iliyoandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) iliyowaleta pamoja wakurugenzi wa AZAKi zaidi ya 80 kutoka Dar es salaam na mikoa mingine ya Jirani kwa ajili ya majadiliano na kuimarisha uwezo wa AZAKi juu ya uchaguzi wa kidemokrasia.

‘’Ulinzi wa haki za raia ni jambo la muhimu sana katika kuboresha michakato ya kidemokrasia kwenye jamii jumuishi. Mkutano wa leo unatoa nafasi kwa wadau wa uchaguzi kujadili jukumu la AZAKi kwenye chaguzi za kidemokrasia huku tujikielekeza kwenye Uchaguzi Mkuu ujao 2020. AZAKi zinasaidia kuhimiza  uchaguzi wa kidemokrasia kwa kuongeza ujumuishi, uwazi, uwajibikaji na kujenga imani ya watu kwenye michakato ya uchaguzi ”alisema Francis Kiwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS.

Kwa mujibu wa Ndugu Kiwanga FCS ni mfadhili wa muda mrefu wa ushiriki wa Asasi za Kiraia kwenye michakato ya demokrasia hapa nchini. Aliongeza kusema “ FCS imesaidia AZAKi nyingi kutoa elimu ya uraia kwa kushirikiana na  mamlaka za uchaguzi, kusimamia mchakato wa uchaguzi na kuongeza ushirikishwaji wa jamii zilizo pembezoni kwenye michakato ya uchaguzi. Mwaka uliomalizika 2019, tulitoa wito wa maombi ya ruzuku mahususi kwa Asasi za Watu wenye Ulemavu kutekeleza miradi ya kuimarisha ushiriki wa Watu wenye Ulemavu kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020. Katika eneo hili FCS  tumetoa uzoefu wa kipekee na utaalam’’

Wanajopo wa jukwaa hilo walikuwa ni pamoja na maafisa kutoka Tume ya Uchaguzi (NEC) Emmanuel Kawishe, Mratibu Maternus Mallya kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani. Inspekta Bwana Issa Asali, Anna Henga kutoka Muungano wa AZAKI Waangalizi wa Uchaguzi Tanzania. (TACCEO) Mwenyekiti kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWYA) Ummy Nderiananga na Shalika Mayunama kutoka TGNP Mtandao.

Bwana Kawishe alitoa muhtasari wa mipango ya Tume ya Uchaguzi kwa uchaguzi mkuu ujao, maadili ya wadau wa Uchaguzi, jukumu la AZAKi kwenye michakato ya uchaguzi katika nyanja za kutoa elimu ya Upigaji kura na Uraia, uangalizi wa uchaguzi na vigezo vya kuteuliwa kufanya kazi hizo.

Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi alijadili juu ya majukumu yake katika kusimamia amani na ushiriki wa wananchi wakati wa uchaguzi. TACCEO kwa upande mwingine ilijadili kuhusu Ufuatiliaji na uangalizi wa michakato ya uchaguzi kwa kuangalia majukumu ya AZAKi kwenye uchaguzi na fursa za ufuatiliaji wa uchaguzi ngazi za wananchi. Mwishoni, SHIVYAWATA, UNA na TGNP walitoa maoni yao juu ya ushiriki na ujumuishaji wa Watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake kwenye michakato ya uchaguzi.