Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) lilifadhili shirika la Kijogoo Group for Community Development kutekeleza mradi wa kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika kijiji cha Chikuti kilichopo kwenye kata ya Msogezi wilaya ya Ulanga ambayo ipo kilometa takriban 230 kutoka Mji wa Morogoro. Lengo la mradi lilikuwa ni kuhamasisha, kuongeza uwajibikaji na uwazi kwenye matumizi ya mali za umma ikiwemo fedha. Pia mradi ulilenga kujenga uwezo wa wananchi na viongozi wa serikali ya kijiji kwenye matumizi bora ya mikutano ya kijiji kufuatilia jinsi rasilimali za umma zinavyotumika.
Viongozi wajengewa uwezo kwenye uwajibikaji
Wafaidika wa mradi huu ni pamoja na viongozi wa kijiji na wananchi wa Chikuti waliojengewa uwezo kwenye masuala ya uwazi na uwajibikaji, ambazo ni nyenzo muhimu za utawala bora kwa umma. Baadhi ya viongozi waliofaidika ni pamoja na bwana Yusuph Mazengo ambaye ni Mtendaji wa kijiji na bwana Gibson Usolo Mwenyekiti wa kijiji hicho akizungumzia mabadiliko yaliyotokea tangu mradi uanze, alisema;
‘‘Kwenye mradi huu Kijogoo walituelimisha umuhimu wa uwazi kwenye mapato na matumizi ya kijiji na kwamba taarifa inabidi zisomwe kwenye mikutano yetu ya kijiji. Changamoto tuliyokuwa nayo ni mahudhurio ya wananchi kwenye mikutano hii yalikuwa hafifu na Kijogoo walitufundisha jinsi ya kuhamasisha ushiriki zaidi. Tulihamasisha na idadi ya watu imeongezeka kutoka wastani wa wananchi 70 mpaka 100 na sasa wananchi kati ya 200 mpaka 300 huhudhuria. Sasa uwazi umeongezeka kwani mapato na matumizi husomwa kwa wananchi na ni wao wanaopitisha matumizi kwa ajili ya utekelezaji. Pia mapato haya na matumizi hubandikwa kijijini hapo kwa wananchi kuyasoma na kuyapitia au kuuliza maswali kijijini hapo.
Jinsi mradi ulivyorudisha umuhimu wa mikutano ya kijiji
Bwana Yusuph Mazengo aliongezea na kukubaliana na bwana Gibson kwamba mradi ulikuja muda muafaka na umesaidia kuongeza sauti za wananchi kwenye usimamizi wa rasilimali za umma. Alisema; ‘‘Mkutano wa kijiji ni mahali ambapo maamuzi muhimu kuhusu kijiji hupangwa na ili kuongeza ushiriki wa watu uongozi wa kijiji tumeweka faini ya sh 2000/- kwa anayekosa kuhudhuria bila sababu maalumu, hii ni kusaidia kuongeza mahudhurio, wananchi wengi sasa wanahudhuria na kutoa maoni yao kwenye kuazimia mambo ya maendeleo ya kijiji chetu’’
Mradi umesaidia kuhusisha mikutano ya kijiji kama jukwaa la kutoa nafasi ya ushiriki wa watu na kuongeza uwazi kwenye uendeshaji wa shughuli za maendeleo ya kijiji. Sasa inawezekana kuchukua hatua madhubuti kivitendo na maamuzi kwenye mambo yanayohusu maendeleo ya kijiji kwa haraka zaidi. Kutokana na mradi huu mahudhurio yameongezeka, mfano, mkutano uliofanyika tarehe 12 Desemba 2018 watu 235 walihudhuria na wa tarehe 29 Desemba 2018 watu 246 walihudhuria. Huu ni ushahidi wa kuongezeka ushiriki wa wananchi kwenye mikutano ya kijiji kwani ni watu 97 tu walihudhuria mkutano wa tarehe 17 Agosti 2018.