Kwa ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society (FCS), shirika la Tanzania Initiative for Social and Economic Relief (TISER) lilitekeleza mradi wa kujenga amani na kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya ya Mvomero iliyopo takriban kilomita 132 kutoka mjini Morogoro. Wilaya hii hukumbwa na migogoro ya mara kwa mara inayohusiana na matumizi ya ardhi hasa baina ya jamii za wafugaji na wakulima.
Viongozi wajengewa uwezo wa kutatua migogoro
Ili kufanikisha mradi huu shirika la TISER liliwahusisha viongozi wa serikali za mtaa kwa kuwapa mafunzo ya jinsi ya kushughulikia migogoro ya kijamii. Hii ni kwa sababu mara nyingi migogoro midogo midogo isiposhughulikiwa kikamilifu na dalili zake kupuuzwa hugeuka kuwa migogoro mikubwa. Mmoja wa viongozi na wanufaika wa mafunzo yaliyotolewa na shirika la TISER alisema
‘‘Shirika la TISER lilifika hapa kwa mara ya kwanza mwaka 2016 na mafunzo yao yalitumia mbinu mbalimbali. Kwanza, walianza kutufunza sisi viongozi kuhusu mipango bora ya matumizi ya ardhi, sheria ya ardhi, masuala ya kutunza amani na utatuzi wa migogoro. Walifanya hivyo pia kwa viongozi wa wilaya na halmashauri. Pili, waliwajengea uwezo wanakijiji wa wilaya yetu kupitia mikutano ya kijamii, na kubandika picha zenye kuonyesha maeneo ya kilimo na ya ufuagaji ili kuimarisha mipango bora ya matumizi ya ardhi .Kama viongozi uelewa wetu kwenye utatuzi wa migogoro umeimarika. Mfano sasa nafahamu ya kuwa mtu akiharibu hekta moja ya mazao atalazimika kulipa fidia ya shilingi milioni 1,333,800 kwa mujibu wa sheria.’’ kaimu mtendaji wa kijiji cha Wami Luhindo Ndugu Jeremiah Kapera ambaye anasema.
Jinsi baraza la ardhi ilivyofaidika
Ili kutafuta suluhu la kudumu la migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima, TISER iliwajenga uwezo baraza la ardhi la kijiji juu ya namna za utatuzi wa migogoro ya ardhi kisheria. Hiki ni chombo muhimu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoletwa ikiwemo migogoro ya ardhi.
‘‘Mafunzo tuliyopata kutoka kwa TISER yametusaidia kutatua migogoro mingi ya ardhi inayoletwa kwetu na wananchi .Mara nyingi huziita pande zote zinazokinzana kuwasikiliza na kujaribu kutatua tofauti zao kwa amani. Jukumu letu lingine ni kusambaza elimu ya umuhimu wa amani na usalama kwenye maeneo yetu. Lengo ni kujenga utamaduni wa kujadiliana panapotokea changamoto hizi’’, alisema Mjumbe Baraza la Ardhi Mabrouk Masua.
Kwa kawaida kama kesi isipotatuliwa na baraza la kijiji inapelekwa kwa mtendaji wa kijiji na baraza la ardhi la kata kwa kusikilizwa zaidi.Mwana baraza mwingine bwana Haji Issa Kimaro anaongeza kusema
‘‘Shirika la TISER limekuwa ni msaada mkubwa katika kurudisha na kudumisha amani kwenye jamii zetu. zamani hatukujua njia bora ya kukaa pamoja kati ya wakulima na wafugaji. Kwa uhamasishaji wa TISER, sasa wakulima wanaheshimu mifugo ya wafugaji na wafugaji pia wanaheshimu mashamba na mazao ya wakulima’’.
Wafugaji wanasemaje?
Kati ya watu ambao wamefaidika sana kutokana na mradi huu uliotekelezwa na TISER ni bwana Philipo Kipuyo mkazi wa kata ya Dakawa ambaye ni mfugaji anaeleza hali ilivyokuwa kabla na jinsi gani shirika la TISER kupitia mradi huu lilivyofanikiwa kurudisha amani.
‘‘Hali ilikuwa mbaya kabla ya mradi wa TISER ,wafugaji walikuwa wanatunza mifugo mingi na maeneo ya malisho na ya kilimo yalikuwa haba na hili lilisababisha migogoro.Shirika la TISER walikuja kuhamasisha watu juu ya umuhimu wa amani katika kuleta maendeleo, mfano sio sawa kwa wafugaji kuachia mifugo ikala mazao ya wakulima na pia si vizuri kuuwa mifugo ya wafugaji. Uhamasishaji wa masuala ya usalama na amani ulifanyika kupitia mikutano mingi hapa mvomero kwangu mimi uwepo wa TISER hapa kwetu ni mkono wa Mungu. Tunawashukuru sana’’.
Kwenye mafunzo shirika la TISER liliwafunza wafugaji mbinu bora za ufugaji zinazozuia ufugaji wa holela unaoleta migogoro baina yao na wakulima. Kwa sasa wafugaji kama ndugu Kipuyo wamepunguza mifugo yao ili waweze kuitunza vizuri na sasa anachungia kwenye uzio jumla ya n’gombe wake 25, anakusanya majani na kulishia mifugo yake kwenye uzio. Pia amepunguza jumla ya mifugo yake kutoka n’gombe 70 mpaka 50 hii imemrahisishia namna ya kuitunza.
Shirika la FCS linasaidia miradi ya kulinda amani na utatuzi wa migogoro kwa kutafuta suluhu ya muda mrefu kupitia miradi kama huu.Hii ni kwa kuwa linaamini amani ni msingi wa maendeleo wa nchi yoyote ile.