Inawezekana kuwafanya vijana kuwa nguvukazi yenye ufanisi na inayotambua thamani na nafasi yao katika jamii na Taifa. Na kwa kutumia asasi za kiraia (AZAKI) inawezekana kabisa hili likafanyika kuanzia ngazi ya chini kabisa zilipo kaya zenye changamoto nyingi za kijamii. Mfano ni vikundi vya vijana wa Jijini Mbeya nchini Tanzania.
Boaz Mwasipu ni kijana mjasiriamali wa jijini Mbeya aliye tofuti sasa na alivyokua miaka miwili iliyopita. Ameshaendesha vizuri mradi wa kuzoa taka kwa malipo. Ameshajitolea kupitia Dawati la Jinsia katika masuala ya ulinzi kwa mtoto. Yeye pamoja na wenzake wanazalisha sabuni mbalimbali na kusindika viungo na mbogamboga. Pembeni pia ni mchuuzi wa bidhaa nyingi wanazotengeneza kwenye vikundi vyao, ambapo pia ni kiongozi – wa Kikundi cha Vijana cha Inuka Angaza Kata ya Ilomba na pia Mwenyekiti wa jukwaa la vikundi sita vya vijana toka katika Kata sita za Halmashauri ya Jiji Mbeya.
Miaka miwili iliyopita Boaz alikua kijiweni tu pamoja na wenzake wakizengewa na mambo hatarishi yote kwa vijana – mihadarati, ulevi, wizi na hata magonjwa ya zinaa. Yote hii ni kutokana na vijana kutojitambua. Wengi wao wameishia elimu ya msingi na sekondari na hawana stadi za ziada kuwapenyeza kwenye soko la ajira.
Swali hapa ni je, jamii yawezaje kubadili vijana kama Boaz wasiokua na tumaini la kesho wanaotoka kwenye kaya zenye changamoto nyingi kuwa vijana wakakamavu, wanaojitambua, wajasiriamali watengezaji na wachuuzi wa bidhaa za usafi na kilimo, wenye ndoto za kuwa na viwanda vya kati kupanua harakati zao za maisha? Jibu lake linagusa maeneo tatu: jamii, AZAKI na Serikali.
Utamaduni wa kujitolea na AZAKI
Mama Tusekile Aggrey, (54), ni Mwenyekiti wa SHOP, asasi iliyo nyuma ya mafanikio ya Boaz na wenzake. Hadithi yake na hii asasi inaanzia kwenye utamaduni wa kujitolea.
“Asasi yetu ilianza kama kikundi cha kusaidiana cha wanawake sita, tukianza kuweka akiba kutokana na mchango wa Sh 5,000 tu kila mwezi. Mwisho wa mwaka tulikua na utaratibu wa kugawana akiba ile. Siku moja tukapata wazo kuandaa tafrija tule na watoto yatima. Ilifanikiwa sana na kutufungulia maono mengi. Ndipo tukaamua sasa kuanzisha rasmi asasi ya kijamii ya SHOP” anaeleza Mama Tusekile.
Asasi ya SHOP inafata nadharia ya mabadiliko inayolenga kufikia vijana mitaani, kuwaweka katika sehemu salama wapatiwe uhamasishaji na mafunzo mbalimbali ili kusaidia kuinua kaya na kukwamua jamii kwenye umaskini.
Baada ya miaka kadhaa yakutekeleza miradi kadhaa ya kijamii, kwa miaka miwili sasa wamefanikiwa kupata ruzuku na uwezeshaji kiufundi kutoka taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS) ili kuwainua vijana katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Ushirikiano baina ya AZAKI na Serikali
Mradi huu uliunganisha mashirikiano kati ya AZAKI na juhudi za Serikali kupitia Idara za Maendeleo ya Jamii na ile ya Vijana jijini Mbeya. Kwa pamoja waliweza kuchanganua changamoto kuu za vijana kwenye jamii, kuweka mipango na bajeti kwa pamoja na kufanya mradi huu kuwa katika njia moja na juhudi za Serikali.
“Kwa kweli kabisa AZAKI wameongeza nguvukazi muhimu sana. Walivyopata tu rasilimali za mradi huu walifika kwetu tukachambua upya kwa pamoja changamoto za jamii na malengo yao. Tulipitia mpaka bajeti zao na kuwashauri katika maeneo kadhaa ili tuwe katika mstari mmoja” anaeleza Baraka Mronga, Afisa Vijana wa Jiji Mbeya.
Anasema mafanikio wanayopata Boaz na vijana wenzake yanatokana kwa kiasi kikubwa na masikilizano na ushirikiano wa karibu baina ya Idara husika Jijini Mbeya na AZAKI katika ngazi zote kuanzia jiji, Kata na mpaka mitaani.
Haya yanaungwa mkono na Maafisa wa asasi ya SHOP Amina Mwakalobo na Yusuph Simbaya. Wanasema wao wamekua wakiingia kwenye ofisi za Afisa Maendeleo za Kata na Jijini na kupokelewa kama watumishi wa Serikali, hivyo kurahisisha uratibu na msaada wa kiufundi katika kazi zao na vijana.
Uwezeshaji Vijana Jijini Mbeya
Hatua ya msingi kabisa kwa SHOP ilikua kuwezesha uundwaji wa Majukwaa sita ya Vijana ya Kata na pia vikundi vyao 11 vya ujasiriamali. Hivi ndio vyombo vikuu vya kuwafikia vijana na kuweza kuwapatia elimu ya kujitambua na uelewa wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2017. Majukwaa haya yalifikia mitaa 42 ya Jiji la Mbeya.
Vijana pia walipatiwa mafunzo mbalimbali yakiwemo masuala yaliyoainishwa kwenye Sera ya vijana, ujasiriamali na stadi za maisha kwa lengo la kuhamasisha kiu ya kukwamua kaya na jamii zao kiuchumi.
Kampeni za mafunzo zilieneza uelewa wa vijana kuhusu fursa zao kisheria kama zilivyowekwa bayana kwenye Sera . Hizi ni pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa vijana kutokana na fungu la 4% kutoka kwenye mapato ya kila Halmashauri. Vijana walieleweshwa hatua za kupitia na mambo ya kufanya ili kuweza kufaidika na uwezeshaji huu kitaifa.
“AZAKI zimesaidia sana kuongeza kujitambua na uelewa wa vijana. Kati yao wameweza kutambuana – wa kujitolea, wajasiriamali, viongozi na wabunifu mbalimbali wa kutatua changamoto za kijamii” anasema Bw Ona Geofrey, Afisa Maendeleo wa Jiji la Mbeya. Anaongeza “Uelewa na ushiriki wa vijana kwenye masuala ya sera na mchakato wa maendeleo ni hatua muhimu sana. Pia mafunzo kuhusu stadi za maisha na masuala ya msingi kama uwekaji akiba, utunzaji mazingira kupitia kuongeza thamani kwenye taka mbalimbali na masuala ya afya ya vijana iliwafanya vijana kujielewa zaidi katika mazingira yao. Pia iliwapa ufunguo wa wapi waanzie katika kujikwamua kimaisha”
Mafanikio ya utatu wa jamii, AZAKI na Serikali
“SHOP wamefanikiwa sana kuamsha hamasa ya vijana kwenye mafunzo na kampeni zao za kijamii kwa sababu ya kutumia nadharia na vitendo. Wengi wamevutika na stadi mbali mbali kama vile utengenezaji sabuni na bidhaa za usafi, usindikaji wa matunda, mboga na viungo na kubuni bidhaa mpya kutokana na taka za karatasi na plastiki” anasema Elly Mwakaswage, Afisa Maendeleo ya Kata wa Isyesye, Mbeya.
Anaongeza “Hakuna kitu kinachangamsha ubongo wa vijana kama baada ya mafunzo kuona umezungukwa na fursa kadhaa katika changamoto kwenye jamii. Hii imeamsha hamasa ya vijana kutaka kutatua matatizo yao wenyewe” Anaamini kuwa vijana wanaojitambua na wenye stadi mbalimbali za maisha wana nafasi zaidi ya kujikwamua kimaisha na kujikinga na makundi na mambo mabaya kwenye jamii kama mihadarati na ulevi.
Anaishauri SHOP kubuni mashirikiano na taasisi za kifedha kuwezesha uundwaji wa bidhaa mahsusi za kifedha na mikopo kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali vya vijana ambavyo vinafanikiwa na kuhitaji mikopo kutanua shughuli zao za uzalishaji na masoko. “Tunahitaji mkopo mahsusi kwa vijana na shughuli zao. Serikali inaweza kuwezesha hili kwa kuangalia mafanikio ya hawa vijana wa Mbeya” anasema Bw Mwakaswage.
Boaz na wenzake wa Kikundi cha Inuka Angaza (wanachama 20) wanaendelea juhudi za ujasiriamali. Kufikia Agosti 2019 walikua wanazalisha miche 400 ya sabuni kutokana na mafuta ya mawese. Wanatengeneza pia sabuni za maji kwa ajili ya kufanyia usafi majumbani na mahotelini. Kwenye uzalishaji wa sabuni wapo Kikundi cha Jitambue pia chenye wanachama 9. Kwa upande mwingine, Kikundi cha Usindikaji (wanachama 30) wanaongeza jitihada kusindika pilipili, mbilimbi, viungo na kutengeneza mvinyo mara tatu kwa mwezi.
Changamoto na mambo ya kujifunza
Juhudi za AZAKI kwa vijana zimekubalika kwa kiasi kikubwa sana jijini Mbeya. Hili limepata msukumo kutokana na mashirikiano mashinani na kupitia kwenye serikali za mitaa. “Bado kunahitajika ubia zaidi kwenye jitihada hizi. Tutathmini pamoja, tuweke mipango na bajeti za vipaumbele vya pamoja. Hii itapunguza kwenda kusiko na kupoteza fedha kwenye marudio baina ya watekelezaji mradi” anashauri Bw Ona.
Pia inashauriwa kuwepo na muendelezo baada ya muda wa mradi kukoma kwani hiyo huweza kuua jitihada na hatua iliyofikiwa kwani kunakosekana msimamizi kwenye jamii. “Tunatakiwa kuwashirikisha wazazi pia katika uwezeshaji wa vijana kwani kaya hunufaika na hivyo mradi waweza kushika mizizi vizuri kwenye jamii” anasema Bw Mwakaswage.