Ushirikiano na umoja unaibadilisha jamii

FCS kwa kushirikiana na taasisi ya Huduma za Kisheria ya Legal Services Facility (LSF) zilifanya mafunzo jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2018 ikiwa ni muendelezo wa mkutano wa kwanza uliofana mwaka 2017. Mkutano wa mwaka huu uliolenga katika kubadilishana uzoefu, uliwaleta pamoja wataalam kutoka taasisi za FCS na LSF.

 

Mambo waliyojifunza wataalam hao yalikuwa na shabaha ya kuziunganisha taasisi hizo mbili kupitia uzoefu na utalaam wao ili kubaini mbinu mkakati za ushirikiano baina ya taasisi hizi.

Wakati FCS ni mdau mkubwa katika utoaji ruzuku hapa nchini, LSF ni taasisi ya kushughulikia masuala ya uwezeshaji wananchi hasa wanawake kupata haki kwa njia ya kuwajengea uwezo katika masuala ya sheria. LSF hutoa ruzuku bila upendeleo ili kujenga taasisi za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria ili kuwajengea uwezo wananchi kwenye masuala ya haki kisheria.

 

Wakifungua mafunzo hayo, wakurugenzi wa taasisi hizi walitoa rai ya kuimarisha ushirikiano kama njia ya kuwafikia wananchi wengi, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali na kubadilishana njia za uwezeshaji.

Katika nasaha zake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bwana Francis Kiwanga alisema taasisi hizo mbili ni washirika wenye ajenda za kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto zinazofanana katika maisha yao ya kila siku. Kiwanga alisema pia “FCS kama taasisi ya kimaendeleo, tunapitia katika mchakato ule ule na kupata uzoefu na changamoto zinazofanana katika utendaji wa kazi zetu. Mwendelezo huu wa mikutano ya mafunzo baina yetu ulioanza mwaka jana ni muhimu sana na unahitaji ushiriki wa wadau zaidi wakiwemo kutoka tasnia ya haki na sheria, vyombo vya habari nk”.

 

 

Mojawapo ya mada zilizojadiliwa wakati wa mkutano huo wa mafunzo ilihusu jinsi ya kuondoa muingiliano wa kazi baina ya taasisi hasa katika utoaji wa ruzuku baina ya FCS na LSF. Katika mkutano huo, wataalam wa taasisi hizo walijadili njia za kupunguza marudio ya kazi zinazofanywa na taasisi nyingine katika sekta mbalimbali ili kuepuka upotevu wa rasilimali na mashindano yasiyo kuwa na tija kwa jamii. “Tunalenga kujenga taasisi imara na madhubuti ili kutoa huduma bora kwa wananchi”, alisema Kiwanga.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa LSF, Kees Groenendijk aliafiki yaliyosemwa na mwenzake wa FCS kuwa tangu mkutano wao wa kwanza kumekuwepo na ushirikiano na mawasiliano ya kiutendaji baina ya taasisi hizo na hivyo kuzinufaisha. Bwana Groenendijk alizitaka taasisi hizo kuimarisha mshikamano na kupanua wigo wa ushirikiano kwa wadau wengine pia.

 

“Kiutendaji, tunakabiliana na changamoto zinazofanana. Kuna baadhi ya vitu vinashabihiana katika kazi zetu, hivyo basi hatuna budi kujifunza na kubadilishana taarifa zaidi. Tuna ajenda inayofanana na tunajivunia kazi hii na njia tunazotumia kufanya kazi zetu. Kwa pamoja, tunahitaji kuangalia njia za ushirikiano zaidi na miundo ya taasisi zetu kwa manufaa ya taasisi zetu”, alisema Bwana Groenendijk.

 

Mkutano huo wa mafunzo wa siku moja ulijikita katika kuangalia mifumo wa kiutendaji ya FCS na LSF, yakiwemo masuala ya:-

  • Usimamizi wa rasilimali na uendelevu wa taasisi
  • Usambazaji wa taarifa na mawasiliano
  • Mahusiano na wadau wa maendeleo
  • Uendeshaji na usimamizi wa ruzuku
  • Kujenga uwezo
  • Hali ya sekta ya asasi za kiraia nchini