Umiliki wa ardhi katika jamii za wawindaji, wakusanyaji na wafugaji

Kikundi cha Ujamaa Community Resource Team (UCRT), kilicho fadhiliwa na Foundation for Civil Society , kilianzisha mradi wa miaka miwili wa “Kuhamasisha Haki za kumiliki ardhi za wanawake katika jamii za wawindaji, wakusanyaji na wafugaji”. Katika vijiji vya Lerug, Partimbo, Orkitkit na Amei Wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara. Kwa kupitia Jukwaa la Haki na Uongozi la Wanawake, Mradi ulitarajia kuwawezesha wanawake mia mbili na arobaini (240) kutambua haki zao, na mia moja (100) kati yao wamiliki ardhi kupitia Hati Miliki za Kimila.

 

Hali ilivyokuwa na lengo la Mradi

Nia ya Mradi ilikua kushughulikia suala la haki za wanawake na usawa katika jamii ambazo kwa mila na desturi zao, wanawake hawana haki ya kurithi ardhi na mali, isipokua kwa kuwadhamini watoto wao. Watoto wakikua udhamini unakoma na wanakabidhiwa dhamana ya kumiliki mali za baba yao. Mfumo huu ulileta madhara mengi kwa wanawake; kwani waliwekwa pembezoni,walionewa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia, hawakushiriki katika masuala ya uchumi, na hivyo walidumaa kimaendeleo.

 

Kukubalika kwa Mradi 

UCRT ilitambulisha Mradi kwa viongozi wa vijiji vya Lerug, Partimbo, Orkitkit na Amei na kwa maafisa wa serikali za mitaa. Viongozi wa kimila kupitia uwezeshwaji katika vikundi vyao vya kijamii na kwa mafunzo. Kabla ya hapo ulifanyika uraghibishi, ushawishi na utetezi wa kuuza hoja kwa viongozi wa kimila kuwauzia wazo, walinunue na waweze kushiriki kikamilifu kwenye mradi. Wazo hili liiuzwa kwa viongozi wa kijamii kupitia mfumo  wa uongozi wa kimila katika vijiji; unaojumuisha Wenyekiti wa Vijiji, Wazee wa mila na mabaraza ya ardhi.

 

Majukwaa ya wanawake, haki na uongozi yaliundwa kwa lengo la kuwafikia wanawake wengi zaidi ili washiriki katika Mradi. Jumla ya majukwaa 10 yaliundwa katika vijijI hivyo vinne. Kila jukwaa lilijumuisha wanawake 24 ambao kwa ujumla liwawezesha wanawake 240. Vikundi vilipata mafunzo kuhusu ushiriki bila ubaguzi wa kitabaka, usawa wa kijinsia, thamani na umuhimu wa ardhi kama ulivyo ainishwa kwenye Sheria ya Ardhi Vijijini ya 1999. Usimamizi wa rasilimali za kijiji, uongozi, namna kufanya maamuzi na kutatua matatizo.

 

Mafanikio ya jumla ya mradi

Viwanja mia moja vinavyomilikiwa na wanawake vimeshapimwa Partimbo, Orkitikiti na Lerug na vinasubiri utolewaji wa Haki Miliki za Kimila. Baada ya mafunzo viongozi wa vijiji na wa kimila walielewa na kukubali wazo la kuwapatia wanawake ardhi kama sehemu ya maendeleo ya jamii. Wanawake walihamasishwa kutuma maombi ya kumiliki ardhi katika mkutano wa mwaka wa vijiji na maombi yao yalipitishwa na mabaraza ya vijiji.Kwenye vijiji ambavyo mipango ya matumizi ya ardhi ilishatayarishwa na waume zao hawakuwa na ardhi yakuwamilikisha, serikali za vijiji ziliwamilikisha ardhi ya wazi ya vijiji. Wanawake ambao waume zao  waliokua na ardhi walishawishiwa na viongozi wa vijiji kuwapa wake zao mashamba.

 

Kijiji cha Partimbo, Kata ya  Partimbo, Laalarkir

Mifano halisi ya mafanikio ya mradi huu inaonekana dhahiri katika kijiji cha Partimbo ambapo  mpango wa uwezeshaji  umefanikisha wanawake mia moja na hamsini na mbili (152) kuomba umilikishwaji wa mashamba. Mpaka  sasa mashamba 20 yameshapimwa na yanasubiri kutolewa kwa hatimiliki za kimilakwa mujibu wa Mwanaidi Massawe, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Partimbo.

 

“Kwa sasa sio rahisi kwa wanaume kuuza ardhi ya familia kwani wanawake wanatambua haki zao, na hii imepunguza migogoro ya ardhi ndani ya familia” alisema Mwanaidi. Aliongeza kwamba mikakati ya uwezeshaji bado inahitajika ili kuongeza uwezo wa wanawake kujiamini katika umiliki wa ardhi; akitoa mfano wa wapimaji wa ardhi walioshindwa kuwapimia wanawake ardhi yao waliopewa na mume wao kwa kutokuwepo kwa mume wao siku ya upimaji’’.

 

James Mshana, Katibu wa Partimbo anasema mradi umeweka rekodi katika kijiji chao; kwani wanawake wengi wamewezeshwa na ubaguzi wa kijinsia umepungua na wanawake wanaheshimika sana kuliko zamani. Kumilikishwa ardhi kumekua kitendo cha kihistoria katika kijiji chao kwa mwanamke kumiliki ardhi.

 

Pamoja na mafanikio hayo, Mshana anatoa angalizo la kuwajumuisha viongozi wa kimila kwenye ushiriki  wa Jukwaa la Wanawake na uwezeshwaji kama wanawake badala ya kuwatenga na kuwategemea watoe maamuzi yanayopitishwa na mabaraza na mikutano ya kijiji.

Catherine Losurutya, Afisa Jinsia na Wanawake UCRT, anakiri wanaume wamehamasika kupima ardhi zao na kupata hakimiliki za Kimila kwa ajili ya ardhi ya familia, wake na watoto. Mabadiliko haya yamechangia  mahudhurio na ushiriki wa wanawake kuongezeka katika mikutano ya kijiji na maslahi pamoja na sauti zao kusikilizwa na kuzingatiwa. Wanawake wamewezeshwa kiuchumi, wameunda vikundi vya kuweka akiba katika kijiji cha Lesuit, wametengeneza katiba na wako katika mchakato wakusajili kikundi chao. Wameanza kulima mazao ya msimu kwenye mashamba yao ili kupata fedha za kujenga nyumba zao za kuishi.

 

Changamoto za Mafunzo

Mipango ya vijiji, matumizi ya ardhi na mipaka bado haijaeleweka vizuri kwa wanavijiji  jambo ambalo limesababisha wavamie sehemu zilizotengewa hifadhi na matumizi maalum; ambayo imechangia baadhi ya wanakijiji kupunguziwa ardhi yao wakati wa upimwaji kwa kukosa kujua mipaka.Wasichana bado hawajatuma maombi ya kumilikishwa ardhi japo wamepata mafunzo  na uwezeshaji kutokana na mila kuwazuia wanawake kurithi ardhi ya familia.Hata hivyo wavulana wameomba kumilikishwa ardhi.

 

Mila na desturi nyingi zimewanyanyasa sana wanawake ambao wamezidi kuonyesha uwezo mkubwa na utashi wa maendeleo lakini wanakosa uwezeshaji. Ili kuzuia mila na desturi zisizo kuwa na maslahi kwa wanawake wala jamii na kuwabagua; kuna haja ya kuwekeza kwa vijana kuwawezesha washiriki na kuzielewa haki za wanawake na madhila wanayoyapata mama zao, ili wasaidie kupinga ubaguzi wa kijinsia.