Ubalozi wa Ufaransa wawezesha asasi za kiraia katika mikoa 3

Taasisi ya FCS iliingia makubaliano na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania Januari 29 mwaka huu kwa ajili ya kuwezesha shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na asasi za kiraia katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mara.

 

Msaada huo wa ruzuku ndogo ndogo umelenga miradi ya ubunifu ya asasi za kiraia na mitandao yao, kupitia Programu ya PISCCA katika Ubalozi huo. Uwezeshaji huo unaunga mkono juhudi za asasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye lengo la kuinua uwezo wa wananchi kijamii, kiuchumi na kiutamaduni pamoja na kukuza asasi zenyewe. Lengo jingine la ruzuku hizo ni kuimarisha jumuia na ushirikiano baina ya asasi na wadau wao katika kuendeleza hali na uwezo wa wanufaika wa miradi hiyo.

 

Tayari asasi nne zinatekeleza miradi mbalimbali kupitia ruzuku iliyotolewa na PISCCA kupitia FCS. Asasi hizo ni NGONEDO, IWAPOA, Asylum Access na ATFGM ambazo zinatekeleza miradi kwa miezi 9.

Katika makubaliano hayo, FCS itatoa mafunzo maalum ya kujenga uwezo na pia kusimamia miradi ya asasi hizo wakati ambapo Wizara ya Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa ya Ufaransa (MFA) kupitia Ubalozi wao uliopo Dar es Salaam watatoa ruzuku za kuendeshea miradi hiyo.

 

Miradi hiyo pamoja na mafunzo kwa asasi husika yalianza kutolewa Januari mwaka huu kufuatia kuzinduliwa kwake na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Mheshimiwa Frederic Clavier na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga.

“Tunaukaribisha kwa mikono miwili ushirikiano huu na Ubalozi wa Ufaransa na wizara husika kama rasilimali muhimu katika kuinua hali ya maisha ya jamii ya watanzania katika maeneo ya miradi. Msaada huu utawasaidia wanawake kupitia mafunzo mbalimbali na uwajibikaji wa wananchi na pia kupambana dhidi ya mila na desturi potofu kama ya ndoa za utotoni na ukeketaji, na pia kuimarisha maisha jamii inayoishi katika mazingira magumu sehemu za mijini”