Tuna furaha tena!

Utangulizi

Kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society, taasisi ya Caritas ilitekeleza mradi wa kuhamasisha haki za watu wenye ulemavu wa ngozi. Mradi ulikuwa na mbinu za kusaidia kupunguza changamoto za watu wenye ualbino  katika manispaa ya Tabora. Mradi huu hasa ulijikita katika kutafuta majawabu ya kuduma na sio tu ya muda mfupi kwenye changamoto nyingi wenye ulemavu ngozi na kwa hivyo ulitumia mbinu mbalimbali kama mafunzo, warsha, kampeni na mikutano kuhamasisha haki za watu wenye ualbino.

Wanufaika ni watu wenye ualbino na viongozi wao, wanafunzi, walimu, waganga wa jadi, viongozi wa serikali za mtaa na viongozi wa kisiasa.

 

Changamoto za watu wenye ualbino na ubaguzi

Moja ya changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ualbino na hali yao ya vinasaba inayowasabibishwa washindwe kufanya kazi kama za kilimo vizuri kwenye mazingira magumu kama ya jua kali. Baya zaidi ni hali mbaya ya usalama mdogo waliyokuwa nayo sababu ya uwepo wa vitendo viovu vinavyofanywa dhidi yao mkoani Tabora na mikoa mingine ya jirani.

Katika hali ya kustusha vitendo hivi vilitokana na imani za kishirikina kuwa mtu akipata kiungo/viungo vya mtu mwenye ualbino anaweza kuwa tajiri kwa kusaidiwa na waganga wa kienyeji. Kote nchini ilienea ya kuwa waganga wa kienyeji ndo walichochea imani hizi ovu za kishirikina zilizopelekea watu wenye ualbino kutekwa, kunyofolewa viungo vyao na kuuwawa si Tabora tu bali hata mikoa mingine kama Mwanza na Shinyanga.

 

Sasa ahueni

Changamoto hiyo kubwa na ya kutisha ya usalama iliwafanya watu wengi wenye ualbino wakiwemo wanawake na watoto kushindwa kutoka majumbani mwao. Hii ilichangia hali ya kutengwa na kuwafanya wengi wasiwe na matumaini katika maisha. Akizungumza kuhusu changamoto hizi na akikumbuka jinsi hali ilivyokuwa mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye ualbino (TAS) mkoani Tabora Bi Blandina Joseph alisema;

 ‘‘Kwa sasa matukio hayo ya kusikitisha dhidi yetu watu wenye ualbino yamepungua sana na hali ya usalama imerudi kuwa kawaida. Sasa tunafanya kazi zetu kwa uhuru bila hofu tuliyokuwa nayo mwanzoni ya usalama wetu au ya kuitwa majina mabaya mitaani mfano zamani watu walikuwa wakituita sisi ni ‘dili’[1].Changamoto hizi zilikuwa kubwa sana kiasi  kwamba tulishindwa kutoka nje ya nyumba zetu kwa kuhofia usalama wetu. Tunashukuru sasa kwa juhudi za serikali na wadau kama Caritas matatizo haya yamekoma’’

Picha 1 Bw. Ramadhani Mramba na Bi. Blandina Joseph wakati wa mahojiano walipotembelewa

Sasa hali mjini Tabora na maeneo yake imekuwa bora zaidi kwa sababu ya juhudi za wadau na serikali kukabiliana na changamoto zilizokuwepo. Ushiriki na ushirikishwaji imefanikisha matokeo haya kwenye mradi sasa walemavu wa ngozi wanaishi vyema na wanajamii kama watu wengine,

Nasi tunaishi kama watu wengine sasa

Bwana Ramadhani Mrama naye alisema; ‘’kwa ujumla vitendo vya ubaguzi na kutengwa na jamii vimepungua sana Tabora na akatolea mfano zamani ilikuwa haiwezekani kwa mtu mwenye ualbino kuolewa au kuoa mtu asiye albino. Ila sasa hali hiyo imebadilika kwani mimi mwenyewe nimeoa mtu asiyekuwa na ualbino. Na kuna mifano mingi tu hapa Tabora. Pia sasa tuko huru kutekeleza haki zetu za kisiasa  kama kugombea nafasi za uongozi na tunaishi kama watu wengine sasa.

Nawashukuru sana Caritas wakifadhiliwa na FCS katika kampeni hii ya kupinga vitendo vya ukatili na kuwanyima haki watu wenye ualbino.

 

Waganga wa jadi wanasemaje?

Vitendo vya utekwaji, kunyofolewa viungo na mauaji ya watu wenye ualbino vimekuwa na watuhumiwa wakubwa ambao ni waganga wa kienyeji. Caritas kwenye utekelezaji wa mradi huu iliwahusisha waganga wote wa kienyeji mkoani Tabora  na kuwafundisha juu ya haki za watu wenye ulemavu wa ngozi. Mmoja ya waganga walihudhurisha warsha hizi zilizoandaliwa na Caritas ni Ndugu Habibu Shabani Ndutu (63) alisema haya;

 ‘‘Nawashukuru sana Caritas kwa msaada huu wa mafunzo na uelimishaji kwangu na kwa jamii yangu ninayoiongoza kwa sababu ukiacha uganga wa kienyeji mimi pia ni kiongozi wa kimila wa kabila la Wayege. Kabla ya mradi kulikuwa na uadui mkubwa kati yetu na jamii kwa sababu ya mauji ya watu wenye ualbino kwa sababu waganga wote tulichukuliwa kwamba tunafanya vitendo hivi. Na hii ni sababu ya waganga wachache waliokuwa wakidanganya watu juu ya kuwafanya watu matajiri kutokana na viungo vya watu wenye ualbino kitu ambacho si kweli kabisa. Kwenye mradi huu pia nilishiriki kuwahamisisha waganga wengi wa kienyeji kushiriki na kuacha vitendo dhidi ya unyanyasaji wa albino.Nimeshiriki jumla ya warsha nane na nimejifunza kwa albino ni watu kama sisi na sio mizimu’’.

Mradi huu pia ulitumia mbinu mbalimbali kwenye uhamasishaji kama mashindano ya ngoma kwa washiriki wenye ujumbe wa kupinga vitendo vya unyanyasaji wa maalbino. Na kikundi kilichoongozwa na Mzee Habibu kilipata ushindi na kupewa zawadi pamoja na fulana zenye ujumbe wa kupinga vitendo viovu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Picha 2

Uboreshaji wa hali za watu wenye ualbino mkoani Tabora

Ndugu Baraka Makona ambaye ni afisa ustawi wa mkoa wa Tabora alisema wanafanya kazi na wadau mbalimbali kuandaa kliniki kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi katika hospitali ya rufaa ya Tabora wakiwemo Caritas. Pia kwenye kliniki hizo hutoa misaada mbalimbali kama vile mafuta maalum ya ngozi kwa ajili ya maalbino ambayo huwapunguzia madhara ya mionzo ya jua kwenye ngozi zao. Misaada mingine ni kofia, na miamvuli.Kliniki hiyo hufanyika kila baada ya miezi hutoa huduma ya kuangalia afya za watu wenye ualbino wale wenye matatizo ya kiafya hupewa huduma hospitalini au hushauriwa kwenda hospitali nyingine kubwa kwa rufaa.

Mkurugenzi wa Caritas Tabora Ndugu Timoth Chombo alisema; ‘‘kwenye mradi huu tulihusisha wadau wote ili kukabili changamoto zote za watu wenye ualbino. Nafurahi kwa sasa kumekuwa hamna vitendo vya mwanzo dhidi ya walemavu wa ngozi na afya zao sasa zinaangaliwa kwa ukaribu’’

[1]Moja ya majina ya kuudhi na kunyanyasa watu wenye ualbino wakimaanisha kuwa viungo vya mtu mwenye ualbino vinaweza kumfanya mtu kuwa tajiri kwa Imani za kishirikina.