Ndoa ya Mitala na Haki ya Wanawake Kumiliki Ardhi

Mara ngapi umeshasikia ndoa ya mitala kama hadithi nzuri kuhusiana na masuala ya haki za wanawake katika jamii? Inawezekana hakuna. Tunaelekea kijiji cha Igula, eneo la Isimani mkoani Iringa kutafiti juu ya familia moja ya kipekee ya mitala. Tumeambatana na  Fatma Tweve na Diana Ndanzi, Mratibu na Afisa Ugani kutoka  Asasi ya kiraia ya TARWOK inayotekeleza mradi wa masuala ya umiliki wa ardhi na mali kwa mwanamke.

 

Hali halisi: changamoto za umiliki wa ardhi na wanawake

Hali halisi ya Igula na Isimani ni ya kutia wasiwasi. Ukitoka katika barabara kuu ya lami ya Iringa – Dodoma kupitia katika Bwawa la Umeme la Mtera, unachepuka katika barabara ya vumbi inayokupeleka kwenye eneo kavu sana la udongo mwekundu. Vumbi na ukavu wa eneo hili unaashiria wasiwasi wa upungufu wa chakula mwaka huu (2019) kwani mazao mengi yamekauka shambani kabla ya mavuno mazuri.

Hii inathibitishwa na viongozi wa kijiji cha Igula – Mwenyekiti Linus Kinyamagoha na Mtendaji Romanus Kapanga. Ni rasmi Kutakua na upungufu mkubwa wa chakula katika jamii hii inayotegemea sana kilimo cha kujikimu, ambacho kinasimamiwa zaidi na mwanamke katika kila kaya ya kijiji. Maana yake ni kwamba wanawake watakua na changamoto zaidi ya usalama wa chakula kwa familia zao.

 

Lakini pamoja na jukumu na nafasi hii ya mwanamke, katika uzalishaji kilimo na kulisha kaya, bado wanakinzana na mila potofu sana zinazokandamiza umiliki na matumizi yao ya ardhi, hata kama ni kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla. Wakiwemo wanaume. Hii ni jamii ya Wahehe ya Iringa.

“Wanawake kumiliki ardhi ilikua ni vigumu sana kwenye jamii yetu kutokana na mila za hapa. Thamani ya mwanamke ilikua chini mno, hata kupelekwa shule kipaumbele kilikua kwa wavulana tu” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Igula, Mzee Linus Kinyamagoha.

 

“Pamoja na juhudi za serikali kuhusu hili, bado jamii ilikua inatumia ujanja ujanja kumkandamiza msichana mpaka mwenyewe anaacha shule – atanyimwa mahitaji shuleni, atanyimwa ruhusa na kufanyiwa visa kwenye kaya mpaka kwenda shule inakua tabu, kwa hivyo suluhisho anaona aache tu shule. Tulikua nyuma sana” anaongeza.

Hali hii ukilinganisha na ongezeko la watu na kukua kwa kijiji kulimaanisha janga kwa jamii hii. Wanawake ndio wasimamizi wa uzalishaji kilimo katika kila kaya na wasipopata nafasi na sauti katika matumizi na umiliki wa ardhi kwenye uzalishaji maana yake usalama wa chakula unapungua. Na hakuna njia nyingine za uzalishaji. Mitaji hakuna ya shughuli za kiuchumi kama ufugaji, biashara na kilimo cha umwagiliaji. Maji hakuna hata ya visima, ingawa yapo karibu sana ardhini kwenye ukanda huu.

 

Maajabu ya mitala

Safari hii inawahusu Mama Mazena Mwenda (54) na Yosefina Mtomkali (60), wakewenza wawili kati ya watatu wa Mzee Yusuph Kasuke wa kijijini Igula. Wake hawa pamoja na mwenzao ni wamiliki halali wa jumla ya eka 40 walizopewa na mume wao na kuzifanyia taratibu rasmi za kupimwa na kupewa hati za umiliki. Hadithi yao ni ya kustaajabisha na kufungua macho.

“Kulima pamoja mashamba ya familia ilikua changamoto kwenye kugawa stahiki ya mavuno. Hii ilikua inaleta misuguano na uvunjifu wa amani kwenye kaya” anaeleza Mazena, mama wa watoto watano na mke wa Pili wa Mzee Yusuph. “Hivyo nikaongea na wenzangu halafu nikaondoka na kwenda kuanzisha kaya yangu. Wenzangu wakakubali. Sote tukaanza kulima na kusimamia mashamba yetu tofauti”

 

Wakina mama hawa wanaeleza utaratibu wa kugawa mashamba baina yao na kulima na kusimamia mavuno tofauti ulileta ufanisi wa hali ya juu msimu wa kwanza tu. Hii iliongeza sana usalama wa chakula na baki kwa ajili ya kuuza. Na hiki kilikua chanzo kwa mume wao kuona umuhimu wa kila mkewe kuwa na mashamba yake mwenyewe anayomiliki na kutumia. Na hii ndio hadithi kaya nyingi za mitala za Igula, huko Isimani zinajifunza na kuchukua kitu.

“Kwa kweli sasahivi tuna uhuru na amani katika kaya zetu. Kila mmoja anasimamia mipango na kilimo chake, mavuno na mauzo yake. Pia tunakodisha ardhi ambayo haitumiki na kupata kipato kinachosaidia kupeleka watoto shule” anaongeza Yosefina, mama wa watoto wanne na mke wa Kwanza wa Mzee Yusuph.

 

“Kila mtu ana mpango wa kuchukua mkopo kwa kutumia sehemu ya ardhi yake ili kuendeleza kaya yake. Kwa kweli uamuzi huu umeleta utulivu sana kwenye familia yetu. Na umetufanya tumempenda zaidi Mzee kwa kutusikiliza na kutuunga mkono” anasema Mama Mazena, huku akitabasamu.

 

Juhudi za kubadili mila potofu kwenye jamii

Iringa ni moja ya Mikoa iliyo nyuma sana kwenye masuala ya haki na nafasi za wanawake katika jamii. Pamoja na juhudi za serikali kupitia vyombo vyake, bado mzigo wa kubadili na kupambana na mila potofu umekua ni mkubwa mno. Na hapa ndio asasi za kiraia (AZAKI) ziliona fursa ya kuweka usaidizi na kuunga mkono Serikali kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii za Iringa.

“Baada ya kitambo cha tathmini tuliona haya masuala ya mila onevu na kandamizi kwa wanawake na mtoto wa kike yanakosa kipaumbele Mkoani kwetu na Serikali inawiwa vigumu kushughulikia kwa wakati mmoja. Na wanawake na watoto ndio walikua waathirika wa kwanza” anaeleza Silvanus Juma, Afisa wa Asasi ya TARWOK inayofanya kazi za kijamii mkoani Iringa.

 

Anaendelea kuhadithia “Jamii ilimkandamiza mwanamke kwenye umiliki wa ardhi kwa imani potofu kuwa ‘anatakiwa kurithi kule atakapoolewa’. Hii ilimkata kabisa nafasi yake kwenye familia yake ya uzao. Na kule anapoolewa, kama akibahatika, hakuwa na nafasi ya kurithi pia”

Juhudi za kupambana na mila potofu na kandamizi kwa wanawake, hususan katika masuala ya umiliki wa ardhi na mali zinahusisha wadau mbali mbali. Asasi ya TARWOK ilipata ruzuku na kujengewa uwezo na Taasisi ya Foundation for Civil Society ili kutekeleza mradi katika Kata 12 zenye vijiji 45 mkoani Iringa. Shughuli mama katika mradi huu ni pamoja na kampeni za kuhamasisha, kuelimisha jamii na kufanya utetezi kupitia mabaraza na mikutano ya vijiji, matamasha na shughuli za kijamii pamoja na vyombo vya habari, hususan kituo cha redio kilichopo mkoani Iringa.

 

Nyingine ni kampeni za utoaji elimu kuhusu masuala ya Sheria za Ardhi na Ndoa na nafasi ya mwanamke kwenye jamii. Pia kuwezesha upatikanaji wa wahamasishaji jamii wa kujitolea wa masuala ya ardhi katika vijiji 60 (mmoja kila kijiji). Hawa walipatiwa mafunzo na sasa wanahudumu kwenye vijiji vyao.

Mradi pia ulijengea uwezo Mabaraza ya Usuluhishi ya Ardhi ya Kata 12 wilayani Iringa. Hii ilihusisha mafunzo ya masuala ya sheria zote muhimu, hususani Sheria  za a Ardhi  Na. 4 na Na. 5 na ya Ndoa na kusisitizia  nafasi ya mwanamke katika jamii. Zilifanyika pia juhudi za utetezi na uchechemuzi kwa viongozi wa serikali za mitaa kwa kila Kata. Hii ni pamoja na Madiwani, viongozi wa vijiji, vongozi wa kijamii na wa dini.

 

Jamii yafaidika

Mpaka kufikia sasa, wanawake 232 wamefanikiwa kupata hati za kimila za umiliki wa ardhi katika vijiji vya Magubike (48), Wangama (88) na Igula (63). Na kizuri zaidi ni kwamba 32 kati yao wamelipa kwa pesa zao kupata huduma hii. Pia vimeanzishwa vikundi vya kina mama 9 kupitia mradi huu na kupatiwa mafunzo kwa jumla ya vikundi 41 kuhusu masuala ya ujasiriamali pamoja na masuala ya haki za ardhi kwa mwanamke.

 

Masijala za Ardhi zimeanzishwa katika vijiji vya Ikuvilo, Lumuli, Kipera and Holo. Pia kumekua na ongezeko la wanawake wanaopigania haki zao za umiliki wa ardhi katika mabaraza ya ardhi – kukiwa na kesi 15 za wanawake tu wakati wa kuandika ripoti hii. Hii inaonesha mwamko na uelewa wa wakina mama kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi na jinsi ya kuyashughulikia.

Huu mradi umefikia vijiji 60 kwa ujumla. Umewezesha vijiji nane kupata masijala za ardhi (Igula, Magozi, Ndiwili, Isaka, Nyang’oro, Ilolo Mpya, Mkulula na Mawindi). Vijiji vingine vitatu (Mikong’wi, Uhoming’yi na Isupilo) tayari wameanza jitihada zao kuanzishiwa masijala za ardhi. Wameulizia utaratibu na wameleta maombi ya usaidizi kwa asasi ya TARWOK.

 

Changamoto bado nyingi

Bado kuna changamoto nyingi kwenye mradi huu. TARWOK wanataja mojawapo ni ahadi ya huduma za bure kutoka kwa Asasi nyingine za kiraia ambayo inaua juhudi na kazi yao ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutaka kuchangia upimaji, urasimishaji na umilikishwaji ardhi.

Pia wameona muda na rasilimali za utekelezaji wa mradi kuwa finyu mno kuweza kufikia jamii kubwa. Hii ina maana juhudi kubwa inafanyika katika sehemu ndogo, hivyo haileti thamani ya fedha za uwekezaji. Na ufinyu huu wa rasilimali unapunguza ufanisi kwenye usimamizi na ufuatiliaji wa mradi na jamii zilizofikiwa.