Moyo wa kujitolea wasaidia AZAKI za Tanzania

Asasi za kiraia (AZAKI) nchini Tanzania zinatumia mikakati mingi sana kufikia jamii nyingi kwa miradi na jitihada zao. Moja ya njia inayofanikiwa zaidi kufikia watu wengi ni kutumia wahamasishaji jamii wa kujitolea. Hawa wamekua kiungo muhimu cha kampeni za jamii katika maeneo mengi nchini. Pamoja na AZAKI nyingi kutofautiana kiutendaji na kwa ajenda, matumizi ya watu wa kujitolea ni utambulisho wa karibu AZAKI zote.

Haijalishi jamii ni za mbali kiasi gani au kazi ya AZAKI ni ngumu kiasi gani, watu wa kujitolea hufikia popote pale AZAKI inapoenda. Wengi wao ni vijana wasiokua na ajira, waliotoka mashuleni na vyuoni. Wanazijua jamii zao vizuri sana kwa sababu walizaliwa na kukulia humu. Wao ni sehemu ya jamii hizi.

Wahamasishaji wa kujitolea ni nguvu kazi muhimu sana katika jitihada za AZAKI kupambana na mila potofu. Wanajituma sana katika kampeni za kijamii za kuhamasisha na kuelimisha kuhusiana na masuala ya haki ya wanawake kumiliki ardhi na uwezeshaji wao. Wanaunganisha jamii zao kupitia viongozi wa jamii, wananchi na AZAKI katika masuala ya haki za raia na binadamu, uwezeshaji wa vijana, ulinzi kwa watoto na uboreshaji maisha ya jamii.

Kila jamii wapo. Wanachohitaji sana ni mafunzo ya kazi wanayotakiwa kufanya na kisha kuwezeshwa kufikia vijiji, vitongoji na mitaa ya jamii zao.

Mara nyingi watu wa kujitolea huhitaji mafunzo ya  kitaalamu katika maeneo wanayotakiwa kuhudumu. AZAKI huwa na jukumu la kutoa mafunzo haya kabla ya kazi kuanza. Mafunzo yanahusu ngazi zote za kazi zao ikiwemo jinsi ya kufikia jamii na kushirikiana na viongozi wa kimila na jamii husika.

Kujitolea ili kuinua wanawake

Faustina Dunda anaishi Kijiji cha Wangama, wilayani Iringa. Faustina mmoja kati ya wanachama 14 wa Kikundi cha Jiongeze katika kijiji hicho kilichopo kilomita kadhaa toka Manispaa ya Iringa. Wengi wa wanachama wa kikundi hicho  ni wanawake. Faustina amekua akihudumu kwa kujitolea kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Anafanya kazi na asasi ya Tanzania Rural Women & Children Development Foundation (TARWORC)iliyopo Iringa katika masuala ya haki ya wanawake kumiliki ardhi na mapambano dhidi ya mila potofu.  Asasi hii inafadhiliwa na Foundation for Civil Society (FCS)

Jamii ndio ilipendekeza na kuniteua kufanya kazi hii. Naona ni heshima kubwa sana kuwa na jukumu hili. Pia nilibahatika kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya sheria za Ardhi na Ndoa pamoja na mila potofu na haki za binadamu” anasema Faustina.

Ameshafanya mengi kufikia jamii yake kupitia uhamasishaji, uelimishaji kupitia mikutano ya kijiji, kupita nyumba hadi nyumba, kampeni za jamii na kuhamasisha vijana wenzake.

Najiona mwenye bahati kupata nafasi ya kujitolea kwenye jamii yangu. Nimejifunza mengi. Nimekutana na watu wengi. Naipenda kazi hii pamoja na changamoto zake” anasema na kutaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi na ugumu wa jamii kubadilika kuhusu mila potofu. Pia ni changamoto kufikia jamii nyingi kwa kuwa hana usafiri wala mawasiliano kwenye kazi yake.

Kuwezesha jamii kuhusu uwajibikaji

Tunduru Paralegal Centre (TUPACE) ni asasi iliyopo mjini Tunduru katika mkoa wa Kusini wa Ruvuma. Wanatekeleza mradi wa uwajibikaji kwa jamii (SAM) na ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma (PETS) wilayani Tunduru. Pia wanafanya kazi na wasaidizi wa kisheria.  Asasi hii inapata ruzuku kutoka FCS.

Wafanyakazi hao wa kujitolea wa PETS walitokana na jamii husika kuwateua, kila kijiji kilitoa wawakilishi wao wenye elimu ya sekondari. Hawa walipatiwa mafunzo maalum mjini Tunduru kutoka kwa asasi ya TUPACE.

“Nimejifunza mengi na kukutana na watu wengi sana. Uelewa wangu na kujiamini kumeongezeka kwa kiwango kikubwa na sina hofu tena kuongea kwenye kadamnasi”Hassan Njongonda, Kamati ya PETS ya Kijiji cha Makoteni, Kata ya Ligoma.

Kwa sasa ninaelewa mengi kuhusu bajeti, ripoti za jamii na jinsi ya kuzisoma na kutafsiri. Ninaelewa jukumu na nafasi yangu kwa jamii yangu. Kazi ya kujitolea imeniwezesha kukutana na watu wengi na kuniongezea kujiamini”Subira Njaidi, Kamati ya PETS, Kijiji cha Ligoma, Kata ya Ligoma.

Sikufahamu kabisa masuala ya uwajibikaji na PETS. Ila kwa sasa nina ufahamu kiasi cha kutosha mpaka najiamini kushiriki na kujitolea kijijini kwangu, hususni kwenye kilimo” Raika Hassan, mkulima, pia ni mjumbe wa Kamati ya PETS, Kijiji cha Ligoma, Kata ya Ligoma.

Baada ya kumaliza Kidato cha Nne, sikupata nafasi ya kuendelea na masomo. Mafunzo ya PETS kwangu yaliongeza kiwango changu cha elimu na uelewa. Nimejifunza mengi na kukutana na wanataaluma wengi wakiwemo wanasheria na maafisa wa serikali. Kiwango change cha kujiamini kimepanda sana. Kwa sasa nina ufahamu mkubwa wa mipango na bajeti za jamii yangu” Said Achireka, mkulima na mjumbe wa Kamati ya PETS, Kata ya Nakapanya.

Kufanya kazi za kujitolea za PETS kijijini kwangu kumenifanya nijulikane kila sehemu. Ninajivunia sana kuwakilisha vijana kwenye kazi hii. Mafunzo mengi yakiwemo ya PETS yamenipa uelewa na elimu kuhusu taaluma mpya kabisa. Kwa sasa ninajiamini kuongea kwenye mkutano wowote kwani hofu yote imeondoka. Muhimu zaidi, kujitolea kumenifungulia fursa nyingi zaidi kwani nakaribishwa kushiriki kwenye kazi nyingi zaidi hapa kijijini” Habiba Said kutoka Kamati ya PETS, Kata ya Nakapanya.

Kujitolea na changamoto zake

Watu wengi wa kujitolea wanaofanya kazi na AZAKI za Tanzania hawalipwi mshahara ama kupewa posho ya utumishi kwa sababu nyingi muhimu. Lakini kubwa na ya kimkakati zaidi ni imani kuwa kufanya kazi na watu wakujitolea ni njia bora ya kufikia jamii kwasababu wao ni sehemu ya jamii na jamii inawapokea kwa urahisi Zaidi. Imani ya pili ni kwamba kutoa malipo kwa kazi za kujitolea huondoa kabisa ile mbegu ya utamaduni wa kujitolea kwenye jamii, ambayo ni msingi wa jamii kushiriki kutatua changamoto zao na kujiiunua.

AZAKI nyingi za kitaifa na zile ndogondogo zinaamini katika nadharia hii. Kwa hivyo, zaidi ya malipo muhimu ya kutekeleza kazi za mradi, wafanyafanya kazi wa kujitolea hawalipwi posho yeyote kama wafanyakazi wa AZAKI. Baadhi ya AZAKI hutoa posho kidogo kuwezesha wafanyakazi hawa kusafiri na kufikia jamii na kuwasiliana na walengwa wa mradi .