Utangulizi
Kutokana na ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society shirika la Kijogoo Community Development liliwezesha uanzishwaji wa kamati za ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma yaani PETs. Wajumbe wa kamati hiyo walichaguliwa na mkutano wa kijiji na baadae walipewa mafunzo ya mbinu za ufuatiliaji wa rasilimali za umma na jinsi ya kukusanya taarifa za matumizi kwenye miradi ya shule mjini Mahenge. Lengo lilikuwa kuhakikisha wananchi wa Mahenge wanapata uelewa na wanafuatilia na kukagua matumizi ya shule kuhakikisha miradi inakuwa kwenye viwango vinavyohitajika kwa thamani ya fedha iliyotumiwa.
Akizungumza jinsi alivyochaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya PETs Bi Joyce Shikanga mmoja wa wajumbe wa PETs alisema ‘‘uliitishwa mkutano wa kijiji na tulipendekezwa na kuchaguliwa na wananchi’’.
Ufuatiliaji ulivyosaidia upatikanaji wa chakula shuleni
Wajumbe waliopatikana na kupatiwa mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasimali za umma walianza kufuatilia shule ya Mahenge mjini na waligundua kuwa licha ya shule kuwa na majengo waliyoyapangisha kwa wafanyabiashara kulikuwa hamna uwazi kwenye mapato na matumizi ya pesa na rasilimali za shule. Katika hili Bi Joyce anaongeza ‘‘tulienda kuwaambia viongozi wa shule waweke mapato na matumizi wazi mwanzoni walikataa lakini kwa ufuatiliaji wetu wa mara kwa mara wakakubali baada ya madai yetu kuungwa mkono na kamati ya shule pia. Kuanzia hapo kukawa na uwazi wa mapato na fedha zikaongezeka. Aliongeza ‘‘sasa wazazi wanachangia shilingi 6,300/= badala ya shilingi 9,600/= walizopaswa kuchangia kwa kuwa hiyo tofauti inachangiwa na mapato yanayotokana na upangishaji wa majengo hayo ya shule kwa wafanyabiashara.
Picha 2 Bi Joyce Shikana akiwa na wajumbe wengine wa PETs kutoka kushoto ni ndugu Hansgary Kwanja na ndugu Wahabi Dongwala
Uwajibikaji umesaidia mapato kuongezeka na kupunguza kiwango cha pesa ambacho wazazi wangechangia mradi wa chakula shuleni.
Kamati ilivyofuatilia matumizi ya milioni 20
Mradi huu pia kupitia kamati ya ufuatiliaji yaani PETs ulifuatilia ujenzi wa darasa la kisasa katika shule ya Mahenge B baada ya serikali kutoa shilingi milioni 20. kwa awamu kwa ajili ya ujenzi huo. Mara ya kwanza zilitolewa kiasi cha shilingi milioni 8 na mara ya pili zilitolewa shilingi milioni 12. Kamati ilihakikisha matumizi na mapato hayo yanabandikwa kwenye mbao za shule ili kila mzazi na mwananchi ajue pesa iliyotengwa na matumizi yalivyofanyika kwenye ujenzi wa darasa hilo. Kamati ilikuwa ikifuatilia pia ununuzi wa vifaa vya ujenzi na jinsi ujenzi ulivyokuwa ukifanyika.
Mjumbe mwingine wa kamati ya ufuatiliaji ndugu Wahabi Dongwala anasema ‘‘kulikuwa na kusuasua kwenye ujenzi wa darasa hilo na hata kwenye ujenzi wa vyoo katika shule ya Mahenge B. Kijogoo walikuja na kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu zao ili miradi ifanyike na wananchi wengi walihamasika na kuja na hasa baada ya mkuu wa shule kubadilishwa kufuatia shinikizo letu na wananchi kwanini alishindwa kusimamia vizuri miradi hii’’.
Kwenye ujenzi wa vyoo vya shule wananchi walijitolea kufyatua tofali na nguvu zao katika ujenzi wake, hela za ujenzi zilitokana na mfuko wa jimbo. Vyoo vipya vina matundu kumi kutoka vyoo vya awali vilivyokuwa na matundu 4 tu kwa zaidi ya wanafunzi 500.
Akizungumza kuhusu mafanikio haya mwalimu Bi Happy Julia Ngulungu aliyekuwa mwalimu mkuu kabla ya kuondolewa kusimamia mradi huo anasema,
‘‘Kamati ya ufuatiliaji imekuwa makini kwenye kazi hii ya ufuatiliaji na kutupa changamoto kufanya vizuri, pia kamati imekuwa ikifuatilia maendeleo ya wanafunzi shuleni kwetu na matokeo yake mahudhurio ya wanafunzi yameongezeka sana. Pia wanajamii wamekuwa wakijitolea sana kwenye ujenzi wa miradi ya shule sababu ya kazi ya kamati kupitia Kijogoo na sasa mazingira ya shule yameboreka sana’’.
Akizungumza jinsi anavyojisikia mwanafunzi wa darasa la saba Abdul Said anasema ‘‘Mazingira mazuri ya darasa hili yananichochea kusoma kwa bidii na nina matumaini ya kufaulu vizuri kwenye mtihani wa taifa unaokuja. Tulianza kulitumia darasa hili mwezi wa saba wakati shule zilipofunguliwa na najisikia vizuri sana’’.
Ushirikiano unavyoboresha elimu Mahenge
Kwenye utekelezaji wa mradi huu shirika la Kijogoo limekuwa likifanya kazi na idara ya elimu ya wilaya ya Ulanga. Akizungumza kuhusu ushirikiano huo afisa taaluma msaidizi wa idara ya elimu wilaya ndugu Discipulus Domino Gabriel anasema wamekuwa wakifanya kazi na wadau wa elimu ikiwemo shirika la Kijogoo kuborsha elimu katika wilaya ya Ulanga. “Wazazi wamehamasishwa kuchangia miradi ya chakula shuleni na ununuzi wa vifaa vya shule mfano hivi karibuni kuna mdau amechangiamashine ya kupiga chapa na wazazi wamekubali kuchangia gharama za karatasi ili kuchapa mitihani’.