Klabu za kujifunza zasaidia wanafunzi kujikinga na ukatili mkoani Arusha

Kituo cha Centre for Women and Children Development(CWCD) kinatekeleza mradi wa miaka miwili wa‘’Kuzuia na kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia ‘’unaofadhiliwa shirika la Foundation for Civil Society chini ya eneo la  mila potofu katika kata kumi  za Wilaya ya Arusha Kaskazini mwa Tanzania.

Lengo la mradi ni kujenga ufahamu na kushughulikia ongezeko la aina za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika jamii ya kimasai zikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji, kuto kutambua haki ya wanawake na watoto kumiliki ardhi na kutambua haki za wanawake na watoto.

 

Mkabala wa Mradi

Ili kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia katika jamii mradi ulilenga kushughulikia maeneo matatu katika mifumo ya kijamii; ikiwemo uwezeshwaji wa wanawake, watoto, viongozi wa kimila na viongozi wa serikali.

Vilabu vya kupambana na ukatili viliundwa katika shule 37 za Msingi na Sekondari ili kuongeza ufahamu na kushughulikia  tatizo la ukatili wa kijinsia katika mfumo wa shule. Wanafunzi walifundishwa namna ya kutambua aina zote za ukatili wa kijinsia, jinsi ya kutoa taarifa, stadi za msingi za maisha, kujiwekea malengo binafsi na masuala ya afya na usafi. Haya yote yalilenga kumwezesha mtoto wa kike aweze kujiamini, kuelewa haki zake, kujithamini, kujitambua na kuweka malengo ya kumsaidia atimize ndoto zake.Mafunzo hayo yalikusudia kuweka mazingira rafiki ya kuwalinda wasichana na watoto kwa ujumla dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

 

Majukwaa kumi (10) ya wanawake yaliundwa, mmoja kutoka kila Kata yenye malengo kama ya vilabu vya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijnsiamashuleni. Majukwaa yalijumuisha uwezeshwaji wa ujasiriamali kuwawezesha wanawake  wajitegemee na kuboresha maisha yao. Walipata mafunzo kuhusu ujasiriamali, miradi ya jamii ya kuongeza kipato na ubora wa maisha. Katika kueneza ujumbe ndani na nje ya jamii wanawake wachache walitambuliwa na kuteuliwa kuwa mabalozi wa kufundisha na kuhamasisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika jamii zao.

 

Mabadiliko katika Jamii

Serikali kwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Jinsia imetoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa aina zote kwa wanawake na watoto. Maafisa wote wa Wizara kuanzia Waziri, Naibu Waziri, watumishi wa ngazi zote wamekuwa wakihamasisha ujumbe huu; katika ngazi zote za maendeleo kwa wadau wa asasi za kiraia na wadau wa maendeleo. Hii imechangia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya jamii mpaka taifa.

“Ujumbe uko wazi kabisa na tunaupeleka katika kila jamii tunako fanya kazi. Hata watoto walipinga ukeketaji na madhara yake siku ya Mtoto wa Afrika mbele ya Naibu Waziri. Tunaishukuru Wizara kwa kutoa tamko kali kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia na mapendekezo muhimu ya utekelezaji.” Haya yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji  wa Kituo cha CWCD, Bi Hindu Mbwedu.

 

Aliongeza kwamba hata maafisa wa afya wanajali hali za watoto na wanachukua hatua dhidi ya wazazi au ye yote ambae amehusika kwenye ukeketaji wa watoto wao. “mafunzo tuliyoendesha katika Kata 10 za Arusha ni kama msingi kwa Mikoa mingine kupambana na ukeketaji. Tuna amini tukijipanga vizuri na kufanya juhudi  ya kuongeza ufahamu na kutoa mafunzo kitaifa, siku moja tutakomesha ukeketaji na aina zote za ukatili  wa kijinsia.”

Wakati wa sherehe ya siku ya Mtoto wa Afrika serikali ilitoa ahadi ya kushughulikia ucheleweshaji wa haki katika kesi za ukatili wa kijinsia. Hii ni kutokana na kilio cha watoto kupitia nyimbo na mashairi yao wakidia haki.

 

Serikali pia iliahidi kuwa na midahalo ya kitaifa mara kwa mara ili kujadili aina zote za mila na desturi potofu zikiwemo; ndoa za utotoni,ukeketaji na ukatili wa aina zote wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kama taifa na kujenga mpango mkakati wa kitaifa kupambana na changamoto hizi.

Maafisa wa Wilaya ya Arusha walitoa wito na msisitizo kwa Mkoa kuwawezesha CWCD kupeleka mradi huu katika Kata zingine ambazo hazijafikiwa; na kuhamasisha halmashauri zitenge bajeti katika maeneo yao kulinda mikakati ya  haki za watoto.

 

Mabalozi wa Mapambano Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia

Kufuatia mafunzo ya uelewa wa  ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuchukua hatua za kujilinda na ukatili kupitia mifumo ya kijamii; mabalozi waliweza kuokoa wanafunzi 40 waliocha shule za msingi  kutoka Kata ya Musa na kuwarudisha shuleni kwa ushirikiano na klabu za jinsia na kamati za uongozi wa shule katika maeneo yao.

 

Katika Kata ya Kisongo Balozi wa jamii alibaini tishio la ukatili wa kijinsia na kuokoa watoto 6 dhidi ya ndoa za lazima kwa ushirikiano wa wazazi, walezi na viongozi wa kimila na serikali. Watoto wengine 10 wa Kata ya  Makebes waliokolewa kutoka kulazimishwa kuchunga ng’ombe na kuuza mifuko ya plastiki na kurudishwa shuleni.

Mabalozi wa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ndani ya Jamii waliwezeshwa kufanya kazi na serikali za mitaa, shule na vijiji kwenye kampeni iliyohusisha kuweka mabango yenye ujumbe wa kuhamasisha dhidi ya ukatili wa kijinsia yenye  ujumbe “Niaache nisome sitaki ndoa za utotoni’” kampeni hii iliamsha hamasa ya kutandaa na kumfikia kila mwanajamii na kuendeleza kampeni.

 

Mabalozi hao wanaendelea na juhudi zao za uraghabishi kila sehemu. Kuhamasisha na kufuatilia masuala ya kuwalinda watoto na wanawake. Pia wanafuatilia Vilabu vyakupinga ukatili na unyanyasaji wa kijnsiashuleni. Kuelimisha na kuhamasisha  wanafunzi kuhusu aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia pamoja na adhabu kali wanazopata shuleni na nyumbani. Juhudi hizi zimefanikisha  azma ya mradi kukubalika na kumilikiwa na jamii pamoja na kuendeleza mradi.

 

Vilabu vya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijnsia mashuleni

Uanzishaji wa vilabu vya kupinga ukatili wa jinsia mashuleni ndio mafanikio makubwa ya Mradi. Vilabu hivi  vimebadilisha maisha ya wanafunzi wa kike, kutoka hali ya woga, unyoge, kutojiamini na chambo cha ukatili kwa kuwa sauti za ushindi katika jamii. Wale wasichana wa Kimasai, waliokua na soni, waoga wahanga wa ndoa za utotoni, wakilazimishwa kufanya kazi na kukeketwa, wamekuwa manusura shujaa! Wazazi na walezi wameanza kuwaogopa na kuwaacha wasikeketwe na kuozwa ndoa za utotoni. Kwa kuondoa woga na kupaaza sauti zao, wazazi na walezi wanaogopa serikali isije ikapata taarifa ya mila zao potofu na kuchukua hatua kali dhidi yao.

 

Vilabu hivi ni moja ya hadithi za mafanikio makubwa katika mradi huu. Wamezaliwa upya na kuhitimu kuwa mabalozi wanawake na wasichana mahiri. Wanakutana, wanajadili na kubadilishana sauti za ushindi ili kutokomeza aina zote za ukatili na mila na desturi potofu.

Shule ya msingi Enjoro, Kata ya Oljoro, juhudi za pamoja kati ya jamii na serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa, Idara za Elimu na Ustawi wa Jamii na Polisi zimewezesha kuokolewa kwa wasichana kumi na sita (16) kutoka kwenye makucha ya ndoa za lazima. Watu kumi na moja (11) wamekamatwa kwa kuendeleza mila na desturi potofu akiwemo Mwenyekiti wa kijiji ambae binti yake alikua kati ya wahanga.Ili kuonesha azma ya serikali kukomesha vitendo hivi vya ukatili, serikali ilimpandisha cheo Mlezi wa Kilabu alietoa ripoti ya matukio ya ukatili kuwa Mwalimu Mkuu wa Enjoro na kumshusha cheo aliyekuwa Mwalimu Mkuu aliefumbia macho kesi za ukatili  na kumfanya Mwalimu wa kawaida.

 

Baada ya kushuhudia mafanikio ya Vilabu vya shule, Afisa Elimu wa Wilaya alichukua uamuzi wa kuwatia moyo wadau katika Kata ishirini na saba (27) za Halmashauri za Arusha kuanzaisha Vilabu vya Haki za watoto kwenye shule zao.

Uamuzi kama huo ulitekelezwa katika shule ya msingi ya Engalaoni Kata ya Mwandet. Matokeo ya ukatili yaliripotiwa, wasichana waliokolewa na wahalifu kupelekwa mahakamani.

Vilabu vya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijnsiamashuleni pia vilianzisha ufundishaji wa kilimo cha kisasa cha mbogamboga kwa ajili ya kujiongezea kipato na stadi zingine za maisha ambazo watazitumia majumbani mwao.

 

Kupungua kwa Kesi

Takwimu za Ufuatiliaji na Tathmini kutoka CWCD, zinaonesha matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia umepungua kutokana na kuwepo kwa  mradi katika jamii. Mafanikio hayo yameleta mabadiliko chanya ya kuunganisha nguvu na ushirikiano kati ya serikali za mitaa, halmashauri, vilabu mashuleni na mabalozi wa mapambano dhidi Ukatili na Unyanyasaji.

 

Idadi ya ndoa za utotoni na za walio hatarini

Matokeo  2017 2018
Mahari zilizolipwa na kusubiri  ndoa 183 10
Mahari zilizolipwa na ndoa kufungwa 15 6
JUMLA 198 16

 

Kufuatia mafunzo na uelewa wa jamii, kuna ushirikiano zaidi kati ya Idara za serikali zinazo husika na watoto katika ngazi ya Wilaya hizi, pamoja na kamati za Mifugo na Elimu. Ambazo zilitoa ilani kupiga marufuku mtoto wa umri wa kwenda shuleni kubaki porini kufuga ng’ombe badala ya kuhudhuria masomo.

Kuogezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na jinsi ya kutoa taarifa ya kesi kumeiwezesha jamii kushughulikia kesi zake; na nimatarajio kwamba ushirikiano na mapambano yataendelea vizuri hadi ushindi kamili.