Kwa ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society (FCS) shirika la Tanzania Initiative for Social and Economic Relief (TISER) lilitekeleza mradi wa amani na utatuzi wa migogoro katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Mafanikio ya mradi huu yametokana na shirika la TISER kufanya kazi pamoja na jeshi la Polisi wilayani Mvomero.Mradi ulitumia mbinu mbalimbali kufanikisha malengo yake ikiwemo mafunzo ya kujengea uwezo, uhamasishaji na uwezeshaji wa michezo kuhamasisha watu kwenye shughuli za kurudisha amani.
Jinsi Polisi walivyoshirikishwa
Ukweli ni kwamba jeshi la polisi lina dhima ya kuhakikisha amani inakuwepo. Katika utekelezaji wa mradi huu, shirika la TISER lilifanya kazi na jeshi hili kwa kiwango kikubwa kama wadau wa amani na usalama wa raia na mali zao. Hii ni kwa sababu Polisi ni alama ya usalama wa raia na wanafanya kazi kwa karibu na raia kwa kuhakikisha usalama wao na wa mali zao. Shirika la TISER liliwahusisha kikamilifu kwa kujenga uwezo wao kwenye njia za kudumusha amani kama mijadala ya kijamii ili kurudisha na kudumisha amani.
Akizungumza jinsi shirika la TISER lilivyosaidia jamii, Inspekta Emmanuel Mfuru wa polisi wa kituo cha wilaya ya Mvomero anasema ‘‘Hali ilikuwa tete kabla ya mradi huu kwani uadui kati ya wakulima na wafugaji ulikuwa mkubwa kwani walikuwa wakipigana, mifugo iliuliwa, hujuma ilikuwa kubwa na mashamba yalikuwa yakichomwa moto. Shirika la TISER limesaidia sana kutatua changamoto zilikuwepo kwa kuyaleta haya makundi mawili yaliyokuwa hasimu kukaa chini na kuacha vurugu na kutatua tofauti zao kwa amani’’.
Kufuatia amani iliyorudi kutokana na mradi huu Inspekta Emmanuel anaongeza ‘‘Ilikuwa kama miujiza kuona utulivu umerudi na ilitupa nguvu ya sisi kuendelea na mikakati ya kurudisha usalama’’.
Aliongeza kusema kwamba kabla ya mradi huo kituo cha Polisi cha Wami Dakawa kilikuwa na askari wengi waliokuwa tayari kushugulikia matukio ya uvunjifu wa amani baina ya wafugaji na wakulima kwani ilikuwa ni kawaida .Sasa hali hiyo imebadilika na mashauri na kesi kati ya makundi hayo yaliyokuwa hasimu yamepungua. Zamani walikuwa wakipokea kesi kwa siku kati ya 15 mpaka 20 lakini kwa sasa kwa siku wakipata kesi nyingi hufika 5 tu na pia migogoro imekua michache na mashauri yanayoripotiwa yamekuwa machache.
Sasa ni Wamoja!
Katika mradi huu shirika la TISER liliwezesha uanzishwaji wa kamati za utatuzi wa migogoro na kuendesha semina kwa ajili ya amani. Wadau katika semina hizi walikua wajumbe kutoka pande zote yani wakulima na wafugaji ili kuwaletea pamoja kujadiliana changamoto zilizokuwepo na jinsi ya kuzitatua.
Mmoja ya washiriki wa kamati hizi ni mchungaji Daniel Mgusa wa kanisa la Assemblies of God anasema ‘‘
“Kabla ya mradi huu uadui ulikuwa mkubwa kati ya makundi haya kiasi kwamba wafugaji walikuwa hawaendi nyumba za ibada wanazoenda wakulima na wakulima wakifanya hivyo hivyo’’
Michezo kama nyenzo ya amani
Shirika la TISER limetumia michezo kama nyenzo ya kuwaleta pamoja wakulima na wafugaji ilikusaidia kurejesha amani katika wilaya ya Mvomero. Waliamua hivyo kwa sababu michezo inasisitiza usawa, kufanya kazi pamoja na nidhamu ya kufikia lengo moja.Matokeo yake mbinu hii ilisaidia sana upatikanaji wa amani kwa kupunguza migogoro na kuleta umoja. Akilizungumizia kuhusu michezo hii mkurugenzi wa TISER bwana Otanamusu Masaoe anasema ‘‘Tulitengeneza timu zilizowahusisha wakulima na wafugaji hii ilisaidia kuwafanya wawe wa moja kwani unakuta mkulima anacheza timu moja na mfugaji hii ilisaidia sana kuondoa hisia kali’’.
Shirika la TISER liliandaa michezo hii katika eneo la Wami Sokoine ambapo watu wengi kutoka maeneo ya karibu walihudhuria. Mbali na mpira wa miguu pia kulikuwa na michezo mingine kama kuvuta kamba, kufukuza kuku na netiboli na watu wa jinsia, umri, kazi na dini tofauti walihudhuria.
Mradi huu umeonyesha kuwa na umuhimu katika kupunguza migogoro na kuimarisha umoja baina ya makundi tofauti. FCS imekuwa ikifanya kazi na mashirika mengine pia mbali na TISER kujenga uwezo wa majadiliano ya amani kwenye mikoa mbalimbali hapa Tanzania zenye changamoto za migogoro.