PROGRAMU YA UTAWALA BORA
Program hii ina matokeo makuu mawili
Matokeo I: Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) zinatoa huduma bora na zenye usawa.
Lengo kuu la eneo hili la matokeo ni kuhakikisha huduma bora zinatolewa na kupatikana katika ngazi ya serikali za mitaa. Tunaamini kuwa kama Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakuwa na uwazi zaidi na kuwajibika kwenye michakato yao ya kufanya maamuzi na matumizi ya rasilimali basi utoaji huduma bora za kijamii kwa umma utafikiwa. Kwenye sehemu hii ya matokeo FCS inatoa ruzuku kwa asasi zinazotekeleza miradi ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji jamii (Social Accountability monitoring(SAM)) na Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma (Public Expenditure tracking Surveys(PETs)) katika sekta nne za; Elimu, Maji, Kilimo na Afya.
Matokeo II: Kuwepo kwa Michakato bora ya kidemokrasia inayozingatia haki za wananchi, hasa haki za makundi ya pembezoni (Mfano, watu wenye ulemavu,Vijana, na wanawake).
Serikali imefanya juhudi kadhaa kushughulikia changamoto zinazohusiana na masuala ya jinsia, unyanyapaa, ukatili na ubaguzi unaoathiri wanawake, watu wenye ulemavu na makundi ya pembezoni. Licha ya juhudi hizo, Ukeketaji na aina nyingine za ukatili dhidi ya watoto na ukatili wa Kijinsia kwa ujumla bado vinaendelea katika sura tofauti tofauti kama ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili, ukatili wa kijinsia, ukatili wa kisaikolojia na ukatili wa kiuchumi kama vile wanawake kukosa umiliki wa ardhi na umiliki mwingine wa mali. Haya yote kwa sehemu kubwa yanafanywa na wanaume. Kuhusu haki za watu wenye ulemavu, licha ya juhudi kadhaa zilizofanywa na Serikali kama vile kutoa maagizo ya kisera na sheria, ubaguzi katika jamii na unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu bado unaendelea. Kutengwa huku kijamii kunakwamisha ushiriki wao kikamilifu katika masuala ya kijamii na kiuchumi na kupunguza upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwa watu wenye ulemavu. Kwenye eneo hili la matokeo FCS inafadhili miradi inayohusu: –
- Utetezi na uchechemuzi dhidi ya mila potofu kama vile Ukeketaji, Ukatili dhidi ya Watoto (VAC) kama vile Ndoa za utotoni, Mimba za Utotoni,) na Ukatii wa kijinsia kama vile Ubakaji na aina nyingine za ukatili dhidi ya wanawake).
- Utetezi na uchechemuzi wa haki za watu wenye Ulemavu ili kuongeza ushiriki wao kwenye uwajibikaji wa umma na michakato ya utawala wa serikali za mitaa, huduma bora ikiwemo elimu na afya, hasa kwa Mashirika na Mitandao ya Watu Wenye Ulemavu kutoka mikoa yote ya Tanzania
- Kukuza upatikanaji wa ardhi na hakimiliki na umiliki wa mali nyingine kwa wanawake
PROGRAMU YA UWEZESHAJI KIUCHUMI
Chini ya program ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, FCS inafadhili AZAKi kutekeleza miradi ambayo italeta matokeo yafuatayo:
Matokeo I: Kuhakikisha kuwa vijana wajasiriamali wamepata masoko kiurahisi, rasilimali na mali za kujiingizia kipato.
Jitihada kubwa zinazopewa ufadhili ni pamoja na:
Jitihada kubwa zinazopewa ufadhili ni pamoja na:
- Kufanya kazi na serikali za mitaa kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa vijana kuanza, kupanua na kukuza biashara zao, na kutumia fursa nyingine za kiuchumi zinazopatikana kwenye maeneo yao.
- Kuwawezesha vijana aidha mtu mmoja mmoja au kikundi kuanzisha miradi ya kujiingizia kipato ili kuboresha maisha yao na kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na kupata 4% ya fedha zilizotengwa kwa vijana katika ngazi za wilaya, manispaa na Halmashauri za Miji.
- Miradi ambayo itaendelea kuongeza ujumuishaji wa vijana kwenye mifumo ya serikali na michakato ya kufanya maamuzi.
PROGRAM YA KULETA AMANI NA UTATUZI WA MIGOGORO
Lengo la Programu: Kuchangia wanajamii kuishi kwa amani na mshikamano miongoni mwao, kati ya jamii na jamii na vikundi vya watu mbalimbali ndani ya jamii
Miradi inayopewa ufadhili ni pamoja na:
- Miradi inayohimiza Umoja wa Kitaifa na mshikamano kati ya makundi ya watu
- Jitihada za mazungumzo ya kuleta amani kwa kuziba tofauti za kisiasa na kuhimiza mazungumzo ya kisiasa kati ya vyama mbalimbali vya siasa
- Miradi ambayo inahimiza jitihada za utatuzi wa migogoro inayohusu maliasili ikiwemo migogoro ya ardhi.
- Miradi na jitihada zinazokuza mazungumzo ya amani kati ya dini mbalimbali