Hapana kwa ukeketaji!

Kwa kupitia shughuli za utekelezaji wa mradi kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society shirika la Tusonge liliibua changamoto zinazosababishwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kufanikisha utatuzi wake. Matokeo yake yamewezesha watendaji wa vitendo hivi hasa mangariba kutoka jamii za wafugaji kutoka kata ya Arusha Chini wilayani Moshi kuacha vitendo hivi na kuwa mabalozi wa kupinga vitendo hivi vya ukatili katika jamii zao.

 

Naokoa maisha, kukeketa sasa basi!

Tusonge ilihamasisha na kufundisha jamii za wafugaji kuachana na vitendo vya ukeketaji wa wasichana kwenye jamii zao na wafaidika wakubwa wa uhamasishaji na mafunzo haya wamekuwa wakeketaji wa jadi wajulikanao kama mangaribia. Baada ya wengi wao kuelewa madhara ya vitendo hivi kwa watoto wa kike wameamua kuacha. Mfano mzuri ni Bibi Sara Koromo amabaye amekuwa mkeketaji wa watoto wa kike kwa miongo kadhaa na kuacha baada ya kuhamasishwa na sasa amewahamasisha wengine kuacha. Bi. Koromo anasema; “tunashukuru shirika la Tusonge kwa kutufundisha madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike na sasa nimeacha na siwezi kufanya au kushiriki tena hasa baada ya kufahamu madhara wanayoyapata wasichana hawa wakiwa wakubwa. Ndiyo nilikuwa nafanya kazi hii kwa kulipwa na kupata pesa lakini nikifananisha nilichokuwa napata na madhara yake havifanani nimeamua kuacha’’. Aliongeza; ‘’maisha ya hawa wasichana ni bora kuliko fedha’’.

 

Ni zaidi ya vitendo vya utamaduni!

Hosiana Samwel, mwanamke mwingine aliyeacha uketetaji baada ya uhamasishaji wa shirika la Tusonge. Hosiana anasema walivyokuwa wasichana wadogo walikuwa wakimuhofia sana Bibi Sara Koromo kwani alikuwa mkeketaji maarufu sana lakini cha kushangaza nae alivyokuwa mkubwa aliona Bibi Sara akipata pesa nyingi naye akaamua kuanza kukeketa.

‘‘Ni kumbukumbu za kutisha kwani mtoto anaekeketwa anatokwa na damu nyingi na anapata maumivu makali sana kwa sababu ukeketaji unafanyika bila ganzi. Tusonge wametusaidia sana kuacha vitendo hivi kwani ilikuwa kila mwezi wa kumi na mbili na wa sita shule zikifungwa ilikuwa nyakati za kufanya ukatili huu’’.

 

Vitendo vya ukeketeji havitekelezwi kama sehemu tu ya mila potofu lakini pia kama njia ya kujiongezea kipato kama Hosiana anavyoeleza; ‘‘nilikuwa napata shilingi elfu sitini (60,000/-) au beberu mmoja kwa kila msichana mdogo ninayemkeketa. Kwa watoto kumi kinakuwa kipato kizuri na kwa hiyo nilichukulia kama chanzo cha kipato changu.Tusonge walivyokuja kunishawishi niache nilidhani ni sababu ya wivu kwamba waliniona napata pesa lakini hatimaye nilielewa nia yao njema na nikaacha vitendo hivyo. Mpaka sasa kwenye kazi yetu ya kuzuia vitendo hivi tumeweza kuokoa watoto 20 wa kike waliokuwa wakeketwe wasikeketwe.Zamani kulikuwa na uadui kati yetu na hawa watoto lakini tangu tuache sasa kumekuwa na amani.’’

 

Nimabadilika baada ya Kuelewa                                      

Mwanamke mwingine mkeketaji wa zamani aitwaye Theresia Moreta alisema; ‘‘nilifuatwa na hawa wenzangu walioacha mwanzoni wakinishawishi niache pia nilikataa sababu nilikuwa napata pesa za kujikimu. Baadaye wakaja Tusonge wakanielimisha madhara ya vitendo hivyo hasa wakati wasichana hawa wakiwa wakubwa na kupata ujauzito wengi hupata madhara makubwa wakati wa uzazi na hupoteza hata maisha.Tunashukuru sana Tusonge kwani walikuwa wakitupitia majumbani kwetu na kutuelimisha kuhusu madhara ya ukeketaji kwa wasichana wadogo.’’

Mkurugenzi wa shirika la Tusonge  Aginatha Rutaza alisema kuhakikisha panakuwa na mbinu endelevu za kusaidia kuondoa ukeketaji wanawasaidia mangariba hawa kuwa na shughuli mbadala za kiuchumi ili wasirudie tena ukeketaji kama njia ya kupata kipato.