Utangulizi
Mradi huu umefadhiliwa na Foundation for Civil Society (FCS) na kutekelezwa na shirika la Tusonge. Mradi uliandaliwa kutumia mbinu mbalimbali ili kupata matokeo tarajiwa. Mbinu zilizotumika ni kama uwezeshaji, mafunzo, mikutano ya kijamii, kampeni za uhamasishaji dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na changamoto wanazokutana nazo makundi maalumu kama wanawake na watoto.
Ukatili wa kijinsia hauna mipaka
Vitendo vya ukatili wa kijinsia haufahamu kuhusu mipaka yoyote huathiri makundi maalumu kama wanawake na watoto kwenye tamaduni nyingi, kwa watu wenye rangi moja, makundi ya kijamii kwenye mataifa tofauti duniani. Inahusisha vitendo vya ukatili ambavyo vinawaweka wanawake na watoto wa kike kwenye hali ya hatari. Vitendo hivi vinahusisha ndoa za utotoni, ukeketaji wa watoto wa kike, ubakaji na unyanyasaji wa watoto kijinsia ambavyo mara nyingi huwaachia waathirika madhara ya muda mrefu ya kimwili na kiakili (kisaikolojia).
Jinsi mradi ulivyosaidia kamati ya MTAKUWWA
Mradi huu umesaidia kuifanya kamati ya kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto iweze kufanya kazi zake vizuri. Kamati hizi ziliundwa kutekeleza mpango wa taifa wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto (NPA-VAWC) kwa mwaka 2017/2018 – 2021/22 utekelezwe kwenye ngazi ya kata nchini.
Kabla ya mradi huu, uongozi wa serikali za mitaa uliweza kuanzisha kamati ya MTAKUWWA ya kata ya Arusha Chini lakini haikuwa na uwezo wa kutekeleza kikamilifu ili kupata matokeo tarajiwa. Mradi huu wa Tusonge ulisaidia kuipa uwezo kamati hii kwa wanakamati kujengewa uwezo wa kukabiliana na vitendo vya ukatili kwenye kata ya Arusha Chini, Moshi. Bibi Evarist Komba, MTAKUWWA ambaye ni mmoja wa wana kamati alikuwa na haya ya kusema juu ya kazi zao na jinsi walivyotumia walichofunzwa na shirika la Tusonge alikuwa na haya ya kusema; ‘‘Tulivyoelimishwa na Tusonge tulitoa mrejesho kwa jamii kwenye masula ya ukatili wa kinjinsia.Tulianza na kufuatuilia matukio ya ukatili kama mimba za utotoni na mengine dhidi ya watoto wadogo pia huwa tunaweka kumbukumbu ya matukio yanayotokea yale mabaya zaidi yanaripotiwa kwa mwenyekiti wa kijiji na baadaye polisi kwa hatua zaidi za kisheria.’’
Mjumbe mwingine Bi. Mwanahamis Katala; alisema; ‘‘Kamati yetu pia hushughulikia changamoto za wazazi ambao hushindwa kulea na kutunza vizuri familia ikiwemo watoto.Kuna wazazi walevi ambao kwao bora kulewa pombe za kienyeji kuliko kumnunulia mtoto vifaa vya shule kama madaftari na sare za shule. Tumekuwa tukiwaita wazazi wa aina hii na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kutunza familia kwa sababu mazingira magumu kwenye familia huwafanya wengine wakimbie na kwenda kuwa wafanya kazi wa nyumbani ambapo pesa huchukuliwa na wazazi hao hao mara nyingine.Tumejipanga kuangalia na kufuatilia vitendo vya ukatili wa kijinsia’’. Pia, Tusonge kupitia mradi huu walianzisha kikundi cha vijana kinachofahamika kama Wote Sawaili kuweza kufanya kazi na vijana kama wale wanaofanya biashara za bodaboda.
Samsoni Joshua, mwenyekiti wa kikundi hicho cha Wote Sawa alisema; ‘‘tulihudhuria warsha kadhaa zilizoandaliwa na Tusonge ambako tulijifunza aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia nimeshiriki kwenye kuzuia watoto wasipate changamoto kama kuwazuia wasiingiea kwenye mabanda ya video ambapo mara nyingi video zinazoonyeshwa huwa na madhara kwao. Pia tunawazuia watoto kutembea usiku ili wasidhurike na kutatua migogoro ya kifamilia. Mfano mzuri kuna mama alimfukuza mtoto wake usiku na kisu tulimpeleka kwa mwenyekiti wa kijiji na ugomvi ukaamuliwa bila kuleta madhara makubwa’’.
Tunatumia klabu yetu kupambana na ukatili wa kijinsia Tusonge kwa kupitia mradi huu waliona ya kuwa ukatili wa kijinsia unapaswa kuondolewa kwa kila hali ikiwemo kujenga uwezo wa wanafunzi kwenye kufahamu juu ya ukatili na kushiriki kuuondoa.Walisaidia kuanzishwa kwa klabu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na uongozi wa shule na walimu katika shule ya sekondari Langasani inayoitwa; ‘Vunja ukimya’.
David Ezekiel mwanafunzi wa kidato cha nne na kiongozi wa klabu hii alikuwa na haya ya kusema;
‘‘Tunazungumza kuhusu ukatili wa kijinsia kwenye jamii yetu na kukumbushana umuhimu na wapi pa kuripoti matukio haya. Klabu yetu hukutana mara moja kwa wiki kila siku ya jumanne.’’
Holiness Allen ambaye pia ni mmoja wa walio kwenye klabu alisema; ‘‘nimejifunza kuhusu ukatili wa kijinsia na kufahamu nini hasa maana ya ukatili wa kijinsia ni vitendo vya kikatili anavyofanyiwa kutokana na jinsi yake kama ubakaji na ulawiti.’’
Katika klabu hii wanafunzi hufanya shughuli nyingi za kielimu kama michezo ya kuigiza, na nyimbo zenye ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia. Wanatumia mbinu hizo kwenye kuhamasisha kwenye mikutano ya wazazi na ya jamii Kwa kile wanachojifunza wana malengo ya kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Mradi huu umesaidia kuweka mfumo wa kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia kwenye maeneo mbali mbali kwenye sehemu za ibada shuleni na kwenye jamii. Pia Tusonge wameteuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia ambao ni wana jamii wenye ushawishi kwenye jamii zao.