Hali za wenye ulemavu zaboreshwa

Kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society, shirika la walemavu wasioona, Tanzania League for the Blind (TLB)  lilitekeleza mradi wa kutetea haki za watu wenye ulemavu wilayani Kwimba, katika mkoa wa Mwanza. Moja ya malengo ilikuwa kuhakikisha walemavu wanapata huduma muhimu kwa kuwa wao wanamahitaji muhimu kuwawezesha kuishi maisha yao ya kawaida. Mradi umesaidia watu wenye ulemavu kuishi maisha bora zaidi na kuishi kama sehemu ya jamii nzima. Kabla ya mradi watu wenye ulemavu walichukuliwa kuwa wasio na tija na walibaguliwa kwenye huduma nyingi za kijamii.

 

Mradi wawapunguzia gharama za kuishi watu wenye ulemavu

Changamoto moja kubwa waliyokuwa nayo watu wenye ulemavu wilayani Kwimba ni kuwa kutokana na hali zao za ulemavu wanalipia zaidi kwa mahitaji yao maalumu kuwafanya waishi maisha ya kawaida kama wengine. Kwa mfano bidhaa kama mafuta ya kupaka ili kuzuia athari za miale ya jua kwa walemavu wa ngozi huuzwa kati ya shilingi elfu hamsini mpaka elfu tisini, hii ni gharama kubwa kwani wengi wana kipato cha dola mbili za kimarekani (shilingi elfu nne mia sita hivi za kitanzania) au chini ya hapo kwa siku.

 

Juma Mageshi, mlemavu wa ngozi na kiongozi wa chama cha maalbino Tanzania (TAS) anasema; ‘‘ni muhimu kwa serikali na wadau kusaidia kwani bidhaa hizi ni gharama kubwa mfano mlemavu wa ngozi anahitaji angalau chupa tatu kwa miezi sita’’.

 

Isaac Malumbu wa TLB, mlemavu wa macho anasema pia hata kwao fimbo nyeupe ni gharama; ‘‘ukihitaji fimbo nyeupe kwa mtu mwenye ulemavu wa macho ni shilingi elfu hamsini na wengi hawamudu sababu ya vipato vidogo’’.

 

Isaac Malumbu pia alisema ili kupunguza tatizo la gharama za baiskeli za magurudumu matatu, sasa zinatengenezwa Mwanza ili zigawiwe kwa wahitaji.

 

TLB imekuwa ikishirikiana na serikali ya wilaya kupunguza changamoto hizi za gharama kwa watu wenye ulemavu. Mfano kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 na ya 2018/2019 shilingi milioni saba zilitengwa. Afisa ustawi wa jamii wa hospitali ya wilaya ya Kwimba, Bibi Lightnessalisema; ‘‘katika mwaka 2017/2018 bajeti kwa mahitaji ya watu wenye ulemavu ilikuwa shilingi milioni nne na kwa mwaka 2018/2019 ilikuwa milioni 3 (TZS 3,000,000/-). Kiasi cha shilingi milioni mbili (TZS 2,000,000/-) kilitumika kununua mafuta maalumu kwa walemavu wa ngozi pamoja na kofia, miwani na miamvuli ya kuzuia jua na milioni mbili (TZS 2,000,000/-) zilitumika kwa huduma za watoto 118 wenye ulemavu.

 

‘‘Kwa msaada huu na juhudi tumeweza kuwa na mafuta maalumu kwa ajili ya walemavu wa ngozi kwenye akiba yetu na pia jumla ya fimbo nyeupe 15 zitagawiwa kwa walemavu wa macho” alisema bwana Juma Magesha.

 

Bwana Kahindi Masingija ni mmoja wa waliopatiwa fimbo nyeupe zilizotolewa na idara ya ustawi wa jamii Kwimba alisema sasa ataacha kutumia fimbo ya mti na atatumia fimbo nyeupe kwa ajili ya kutembelea. ‘‘nina furaha kupata fimbo hii maalumu kwani itakuwa msaada mkubwa kwenye kutembea kwa urahisi nawashukuru TLB na wadau wote na nitaacha fimbo hii ya kawaida’’

 

 

Mwana Olimpiki Maalumu!

Mradi huu pia umefanikiwa kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye sekta na fani mbalimbali ikiwemo michezo. Mwezi Novemba mwaka wa 2017 Christina Lazaro (11) mlemavu wa akili alishiriki kwenye michezo ya olimpiki maalumu Zanzibar baada ya kuwa mshindi wa kwanza kwa mkoa wa Mwanza. Serikali ya wilaya ya Kwimba kupitia idara ya ustawi wa jamii ilisaidia gharama za yeye na mwalimu wake kwenda Zanzibar na kushiriki.

 

Mwalimu wake Maria Maguli alikuwa na haya ya kusema;‘‘Christina anapenda mchezo wa kukimbia na kufanya mazoezi. Kwenye mashindano ya Zanzibar alishiriki mbio za mita 100 na alipata nafasi ya saba na akapewa beji. Tunashukuru serikali ya wilaya kwa kutupatia nauli na kulipia gharama za malazi na kula. Natumaini tutapata tena msaada huo mwakani.’’.

 

Christina nae alipata fursa ya kusema kwa kifupi; ‘‘nilifurahi kushiriki mashindano na naendelea kufanya mazoezi ili mwakani nishiriki na kushika nafasi ya kwanza.

 

Picha 2 Christina akiwa ameshika beji yake aliyozawadiwa kwenye mashindano yam bio Zanzibar.Kulia ni Mwalimu wake  Bi Maria Maguli

 

Kujumuishwa kufanya maamuzi

Watu wenye ulemavu wamekuwa wakishirikishwa kwenye kamati mbalimbali kufuatia mradi huu. Mathalani wameteuliwa kwenye kamati ya kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambapo huchangia mawazo jinsi ya kuondoa vitendo vya ukatili wilayani Kwimba. Kwenye kamati hiyo yupo bwana Juma Magashi wa TAS Kwimba, bwana John Kabelo wa CHAVITA Kwimba, bwana Isaac Manumbu wa TLB Kwimba na bwana. Nyerere Mussa wa CHAWATA Kwimba.

 

Akizungumza kuhusu ushirikishwaji Bwana. Nyerere Julius Musa alisema; ‘‘Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye hizi kamati umeongeza sauti yetu kwenye maamuzi. Pia watu wenye ulemavu wameshirikishwa kwenye kamati nyingine kama kamati ya ukimwi ya wilaya.

 

 

Mradi umesaidia miundombinu kwa walemavu

Mazingira rafiki ni eneo ambalo mradi ulijikita pia kutetea na maeneo mengi ya ofisi za umma na huduma za jamii kuna njia maalumu za walemavu.Maeneo mengine ni hospitali shule   na hata nyumba za ibada.

 

Walemavu wilayani Kwimba

Aina ya ulemavu Wanaume Wanawake Jumla
Ulemavu wa viungo 589 402 991
Upofu/ulemavu wa macho 215 123 338
Kutokusikia/Uziwi 306 307 613
Ulemavu wa akili 59 42 101
Ulemavu wa ngozi/ualbino 39 51 90
Jumla ndogo 1298 925  
Jumla kuu 2133