Hali bora Zaidi kwa Walemavu wa ngozi

Mbinu

Kwa ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society, shirika la Caritas limetumia mbinu mbalimbali kuwafikia na kuhamasisha jamii juu ya haki za walemavu wa ngozi na matunzo. Mbinu hizo ni kama mafunzo maalumu, warsha kwa waalimu, wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari. Pia mradi ulitumia klabu za shule kuboresha mazingira ya kujifunza ya walemavu wa ngozi shuleni na kwenye jamii kiujumla.

 

Asante Caritas nilijifunza jinsi ya kuwatunza wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi

Wanafunzi na walimu wa shule ya Msingi Furaha ambayo ni maalum kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa ngozi ni moja ya wafaidika na mradi huu. Akisimulia walichopata kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Critas kwao na kwa wanafunzi Mwalimu Joel Masele alisema;

‘‘Nilifurahi kuhudhuri mafunzo haya kwani yalihusu elimu kuhusu ulemavu wa ngozi mfano tulijifunza ualbino ni nini na wanapaswa wakae kwenye mazingira gani ili wasiathirike na mazingira magumu kwao kama jua kali. Kwa hiyo tulifundishwa pia tuhakikishe wanavaa nguo za kuwakinga na miale ya jua na pia tulijifunza kuwa ni watu kama watu wengine ukiacha mahitaji yao maalumu. Pia kwenye mafunzo haya tulienda na wanafunzi wetu ambapo walijifunza jinsi ya kujiangalia na kutunza ngozi zao kwa kutimia mafuta maalum’’.

 

Nafurahi Kujitunza.

Mmoja ya wanafunzi waliohudhuria mafunzo haya pamoja na mwalimu wao ni Baraka Jeremiah (16) anaesoma darasa la tano shule ya msingi Furaha. Alikuwa na haya ya kusema;

‘‘Nilijisikia kuthaminiwa sana kwa mimi na wanafunzi wenzangu kushiriki katika warsha hiyo ya mafunzo kwa sababu nilijifunza kujitunza mwenyewe kama jinsi ya kutumia mafuta maalumu ya kuzuia miale ya jua. Nilijifunza jinsi ya kuepuka kupata kansa ya ngozi kama hatutunza ngozi zetu kwa kupaka mafuta na kuvaa nguo za kufunika ngozi zetu vizuri kuvaa miwani ya juu na kofia maalumu za kuzuia jua. Kabla ya mafunzo sikujua jinsi ya kujitunza na wala sikuona umuhimu wa kuvaa vizuri au kutumia mafuta mara kwa mara.’’

Baraka alisema, alifurahi sana darasani kwake wote walienda kupata mafunzo haya yamewasaidia sana.

 

Picha 1 Baraka Jeremiah (katikati) akiwa na wenzake ambao pia walihudhuria mafunzo hayo mjini Tabora yaliyoandaliwa na Caritas

 

Maalbino ni kama watu wengine!

Kwenye mradi huu, Caritas iliwahusisha walimu na wanafunzi wa shule za sekondari na kuwapa elimu juu ya haki za watu wenye ulemavu wa ngozi. Shule ya Tabora ya wasichana imeanzisha klabu malumu ya watu wenye ulemavu kuongeza uelewa wa wanafunzi juu ya ualbino. Katika klabu hii pia wanafunzi wasio na ulemavu huu huusishwa ili kupanua uelewa wa wanafunzi wote juu ya mahitaji maalumu ya watu wenye ualbino. Akizungumza kuhusu klabu hii Mwalimu Stephen Nyandwi, ambaye ni mlezi wa klabu hii alisema; 

‘‘Kwenye hii klabu wanafunzi hukutana kujadili mara moja kwa mwezi na majadiliano yenye kulenga kuongeza uwezo wa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kujiamini ili wajione wako sawa na wale wasio na ulemavu huo. Katika majadiliano haya tunawakutanisha na wale wasio na ulemavu kuimarisha mahusiano ili waweze kusaidiana pale kwenye uhitaji. Mada nyingi kuhusu jinsi ya kuwahusisha watu wenye ulemavu kwenye kazi za shule kwa pamoja kitu ambacho ni muhimu kwao. Tunashukuru sana mradi huu umeleta matokea chanya kwetu.’’

 

Nafurahi kuwa kwenye klabu

‘‘Nimekuwa kwenye hii klabu tangu nilivyokuwa kidato cha nne na tumekuwa wote kwenye klabu na wale wasio na ulemavu wa ngozi. Mada ninazopenda ni zile zinazohusu jinsi ya kutunza ngozi zetu pia zile zinazohusu changamoto zinazotukabili na jinsi ya kuzitatua kwenye masomo yetu pia changamoto tunazokutana nazo kwenye jamii’’ aliongeza Immaculate Olalankuba (19) mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari ya wasichana Tabora

Picha 2 Immaculate Olalankuba na mlezi wa klabu Mwalimu Stephen Nyandwi

 

Klabu hii ina jumla ya wanafunzi ishirini na inaongozwa na wanafunzi wawili mmoja ni mlemavu wa ngozi na mwingine ni mwanafunzi asiye na ulemavu. Inahusisha wanafunzi wengine ili kuwafanya wenye ulemavu wa ngozi wasihisi kutengwa licha ya mahitaji yao maalumu.