FCS Yazindua Kampeni ya kusaidia Watoa Huduma wa Afya

Foundation for Civil Society (FCS) imezindua Kampeni ya ‘Jumanne ya Utoaji’ kuwasaidia na kuwalinda watoa huduma wa afya nchini Tanzania. Lengo la Kampeni ya mwaka huu ni kukusanya vifaa vya kujikinga (PPE) na maambukizi ya corona (COVID-19) kwa ajili ya watoa huduma hao kama hatua ya dharura ya kuitikia mahitaji yaliyosababishwa na mlipuko wa homa hiyo ya mapafu. Kampeni hii inawaalika wadau na umma kwa ujumla kuchangia pesa au vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Corona ( Barakoa, Sabuni, Vitakasa mikono,  Mavazi maalum ya watoa huduma, miwani ya upasuaji) kwa ajili ya watoa huduma wa afya ambao wako mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaripoti kuwa kila mwezi wahudumu wa afya duniani kote wanahitaji vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona . Vifaa hivi huwalinda wahudumu wa afya pamoja na wagonjwa wengine dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona. Lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo duniani, watoa huduma wengi hushindwa kupata vifaa hivyo .Kwakuwa wahudumu wa afya wanahudumia na kuilinda jamii, wanajamii lazima waungane kwa mshikamano kuonyesha shukrani na  kuwasaidia watoa huduma hawa katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Kampeni hii imepewa kauli mbinu ya #TujikingeTuwakingeWahudumaWaAfya itaendeshwa kwa wiki mbili kuanzia tarehe 21 Aprili hadi 5 Mei 2020. Kwenye kilele cha Kampeni hiyo vifaa  vitakavyopatikana vitatolewa kwa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) tarehe 5 Mei 2020

Kampeni hii ni harakati ya Jumanne ya Utoaji iliyozinduliwa mwaka 2012 na Umoja wa Mataifa (UN)  na Shirika la 92Y huko New York Marekani, kwa lengo la kusherehekea uhisani, na utoaji kwa kuchangia kuwasaidia wenye uhitaji. Kampeni hii ya Jumanne ya Utoaji imekuwa ikiandaliwa na kufanyika kila mwaka na kusherehekewa ulimwenguni kote .Nchi nyingi, makampuni, wafanyabiashara, shule, watu binafsi, familia na AZAKi husherekea kampeni hii. FCS imekuwa ikiendesha Kampeni hii ya Jumanne ya utoaji nchini kwa miaka 4 sasa kama njia ya kukuza moyo wa kusaidia wenye uhitaji .Mwaka jana, Kampeni hiyo ililenga kuwasaidia watoto wenye ulemavu wapatao 228 wanaosoma Shule ya Msingi ya Matumaini jijini Dar es salaam. Thamani ya vitu vyote vilivyotolewa kwa wa walezi wa watoto hao siku hiyo ilikuwa zaidi ya Sh milioni 9.5.

” Tumeona nguvu ya jamii kushirikiana kwa pamoja kusaidia wale wenye uhitaji. Tunajivunia kuona wadau mbalimbali; AZAKi, makampuni na watu binafsi wakijitokeza kuchangia kwa njia tofauti katika kampeni zetu katika miaka ya nyuma. Mwaka huu Kampeni inafanyika mapema kuanzia Aprili 21 hadi tarehe 5 Mei 2020 kama hatua za dharura kushughulikia mahitaji ya dharura yaliyosababishwa na COVID-19. Tunatoa wito kwa umma kujitoa kuchangia ama pesa kupitia akaunti ya M-PESA Na 0762767237 au kuleta Vifaa vya kinga (PPE) katika ofisi za FCS. Fedha zitakazotolewa zitatumika kununua vifaa hivi kwa ajili ya wahudumu wa afya.  Tarehe 5 Mei mwaka huu, tutakabidhi vifaa hivyo vitakavyonunuliwa ama kuletwa kwa Chama cha Madaktari Tanzania. Sisi kama jamii lazima tuazimie kushirikiana kwa pamoja ili watoa huduma wa afya ambao ni mstari wa mbele kusaidia wagonjwa wa Corona na kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi ya ugonjwa huu, wasije nao wakambukizwa na kuwa wagonjwa’, alisema Francis Kiwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS.

Bwana Kiwanga ameongeza kwa kusema kuwa, watoa huduma wa afya wanawahudumia watu wanaoshukiwa au wagonjwa waliothibitika kuambukizwa COVID-19. Alisema, Ni muda muafaka sasa kama jamii kuungana na kuonyesha shukrani zetu kwa watoa huduma hawa ”Tumehamasika kuwasaidia watoa huduma wa afya maana sisi sote ni sehemu ya jamii. Jukumu letu pia ni kuhakikisha kuwa katika kupambana dhidi ya virusi vya Corona tuna unga mkono juhudi za serikali katika mapambano haya. Hivi karibuni tuliongoza juhudi za kuchangia fedha kwenye Mpangokazi wa kitaifa wa kupambana na Virusi vya Corona. AZAKi 10 zilichangia kiasi cha shilling Tsh Milioni 79 Serikalini‘, aliongeza

Wakati ambapo sote tunakabiliwa na ugonjwa huu hatari, ukarimu ndio unaowaleta watu pamoja. Ukarimu unampa kila mtu nguvu ya kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa maisha ya wengine. Na ni kitu cha thamani sana ambacho kila mtu anaweza kufanya wakati wa Kampeni hii na kusimama kwa pamoja kupambana na ugonjwa huu.