Asasi ya CEDESOTA ilianzisha mradi wa utetezi na ushawishi kwa wanawake kumiliki ardhi na mali nyingine wilayani Meru mwaka 2016 ukiwa na lengo la kubadilisha mila potofu na imani zinazowabagua na kuwakandamiza wanawake.
Mila hizi zinakandamiza mfumo mzima wa maisha ya wanawake na kuwanyima ushiriki katika maamuzi ya familia, jamii na hata umiliki wa mali na rasilimali. Pia zimekuwa zikitoa mwanya kwa wanaume kuwa na sauti kubwa katika jamii, hivyo kuwakandamiza wanawake katika misingi ya kupata haki sawa na wanaume.
Mradi wa CEDESOTA ulijikita katika kuelimisha jamii kuhusu sheria zilizopo, pamoja na kubainisha ukandamizaji ili kuiwezesha jamii kubadilika na kuendana na sheria ambazo zinazingatia usawa wa kijinsia na haki kwa wote.
Lengo kuu la mradi ni kuchochea mabadiliko kulingana na matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuibua masuala ya haki na usawa wa kijinsia. Mradi huo umetekelezwa katika vijiji kumi na sita vya Kata nne za King’ori, Makiba, Maroroni na Leguruki wilayani Meru mkoani Arusha.
Ushirikishwaji jamii kwenye utatuzi wa changamoto
, CEDESOTA ilisimamia uanzishwaji wa majukwaa ya wanawake katika kila kijiji na Kata kwa lengo la kuwawezesha wanawake pamoja na kuwashirikisha wanaume katika masuala ya haki za ardhi, utawala bora, uwajibikaji kwa jamii, mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa kijinsia, pamoja na afya ya uzazi.
Pia, CEDESOTA ilianzisha mfumo wa mashirikiano kwenye jamii husika katika kufanikisha kampeni za kijamii za elimu, utetezi na uenenzi kupitia ushirikiano wa mifumo na harakati endelevu za kimila na serikali za mitaa,.Mradi uliwafikia:
Matokeo ya mradi
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa CEDESOTA, Bw. Jackson Muro, mafunzo, mijadala ya jamii, vipindi vya radio na mikutano iliwajengea jamii uelewa wa maswala ya haki za wanawake kumiliki ardhi na mali nyingine. Kupitia mafunzo hayo, kumekuwepo na mabadiliko chanya kutoka viongozi wa vijiji, dini na wa kimila na hivyo kuondoa hofu yao dhidi ya haki za wanawake katika umiliki wa ardhi na mali nyingine.
“Hali hiyo, imeleta hamasa kwa wanawake wengi kuomba kumilikishwa ardhi , familia zimeomba kumilikishwa ardhi kwa pamoja na wazazi wanamilikisha watoto wao wa kike na wa kiume ardhi bila ubaguzi. Wanawake sasa wanaweza kununua na kumiliki ardhi, ikiwa ni pamoja na kuandika wosia, jambo ambalo halikuwepo awali kutokana na misingi ya mila na desturi zilizokuwepo. Kwa ujumla, mafunzo yamekuwa kinga kwa wanawake na watoto dhidi ya mila potofu,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umiliki wa mali na ardhi kwa wanawake. Wamekuwa wakigusia masuala hayo katika mahubiri yao makanisani na mawaidha misikitini.
Hatua hiyo, imewasaidia pia wanawake kurejeshewa mali na ardhi zao ambazo walipoteza baada ya wazazi au wenza wao kufariki dunia.
Jukwaa la Wanawake Kata ya Makiba
Katika kubaini mafanikio ya kampeni ya haki za wanawake kumiliki mali na ardhi, tulipata fursa ya kuzungumza na wanachama wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Makiba ambapo maisha yao na jamii kwa ujumla, yameweza kubadilishwa.
Tofauti na wenzake, Upendo alikuwa muathirika mkubwa wa madhara ya wanawake kudhulumiwa haki ya kumiliki mali na ardhi kutokana na madhila na machungu aliyopitia, baada ya ya kumpoteza mume, watoto na dada yake katika ajali ya gari; hadithi ambayo hapendi kuzungumzia.
“Sikuwa najitambua, sikufahamu wapi nitapata haki zangu na nini cha kufanya, lakini kupitia mafunzo ya haki ya kumiliki ardhi kwa wanawake, utawala bora, uwajibikaji katika jamii na usawa wa kijinsia, nimeweza kutambua thamani yangu na nafasi yangu kama kiongozi wa familia na jamii,” anasema Upendo Silvester ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake katika Kata ya Makiba.
Aliongeza kwamba, awali wanawake hawakupata kufikiria kuwa viongozi wala kugombea nafasi za uongozi.
“Kulikua na dhana kwamba uongozi ni mojawapo ya majukumu ya wanaume. Watu hawakuamini katika uwezo wa wanawake kuongoza, hoja na mawazo yao yalipuuzwa. Hali hiyo ilichangia kudhoofisha kujiamini kwa wanawake. Lakini mafunzo haya yametubadilisha; tumekuwa shupavu, tunawania uongozi na jamii imekuwa inatushirikisha katika kutafuta ufumbuzi wa mambo mbalimbali. Tumekuwa tunaaminika zaidi kuliko viongozi wanaume,” anabainisha.
Zama zilizopita, haikuwa rahisi kwa wanawake kurithi ardhi kutoka kwa wazazi na waume zao. Anasema ilikuwa kawaida kwa familia na jamii kumteua mwanaume kusimamia mali na ardhi kwa niaba ya mwanamke, kwa sababu wanaume walithaminiwa zaidi kuliko wanawake.
“Lakini sasa nimetambua kwamba wote tupo sawa, na kwamba mwanamke ana haki ya kumili ardhi kama ilivyo kwa mwanaume. Haya majukwaa ya ardhi ya wanawake, yametusaidia kwa kiasi kikubwa. Ni sehemu yetu ya kujadili na kutafuta ufumbuzi wa masuala ya wanawake. Kupitia majukwaa haya, tumeweza kuwasaidia wanawake sita katika Kata ya Makiba na mwingine kutoka katika kijiji cha Mbuguni kurejeshewa ardhi zao ambazo zilikuwa tayari zimeporwa,” anasema Upendo.
Anaongeza kwamba, wanachama wa Jukwaa la Wanawake wamekuwa na msaada mkubwa katika jamii wanazopakana nazo kupitia elimu inayotolewa kwa njia ya radio. Katika tukio moja, wameweza kumsaidia mtoto pekee ambaye wazazi wake walifariki dunia wilayani Same, Kilimanjaro, kurejeshewa ardhi aliyoachiwa na wazazi wake. Ardhi hiyo ilikuwa imeporwa na ndugu zake, ambao licha ya kuwa wameelimika, bado walitaka kuendeleza mila za ukandamizaji na unyanyasaji. Binti huyo ambaye kwa sasa ameolewa, na kuishi Zanzibar, anakodisha ardhi yake kwa kilimo.
Mafaniko makubwa katika mradi huu, yametokana na ushirikiano wa viongozi wa vijiji na serikali za mitaa kwa msaada na ushirikiano wa Jukwaa katika jitihada za kutatua migogoro ya ardhi na kifamilia. Kimsingi, migogoro hiyo ilipaswa kutatuliwa na mamlaka za Serikali za Mitaa za wilaya. Hali hivyo, imeweza kuwajengea uwezo, utayari na umakini uongozi wa vijiji, pia kuwapunguzia kazi na mrundikano wa mashauri kwa serikali za mitaa.
Akitolea mfano namna elimu juu ya ustawi wa wanawake na mtoto wa kike ilivyochochea ufahamu kuhusu haki za kumiliki ardhi, katika suala zima la uwezeshaji wa wanawake, Kesia anasema ameweza kuandika wosia kwa binti zake watatu, ili warithi ardhi endapo yeye au mumewe atafariki dunia.
“Kupitia jukwaa letu, tumeweza kutatua migogoro mingi ya ardhi iliyohusisha wajane na wanawake wengine katika jamii za Wameru. Wajane hao watatu na wanawake wengi, walipatiwa ardhi na wazazi wao. Changamoto iliyokuwepo katika mila za Wameru ni kwamba, haikuwa kawaida kwa wanawake kurithi au kumiliki ardhi,” anasema Kesia Abel Kaaya, Naibu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake, katika kijiji cha Valeska, Kata ya Makiba.
Kwa upande wake Rosemary, aliyejitambulisha kama mwanamke jasiri katika jamii ya Wameru, ambaye aliachika na kuachiwa watoto wawili wa kulea, anasema aliamua kupigania haki yake baada ya mumewe kuanza kuuza ardhi pasipo kumgawia sehemu yake na watoto.
“Nilimshitaki kwa uongozi wa kijiji, lakini sikupata msaada wowote na kuamua kupeleka shauri langu katika Ofisi ya Mtendaji Kata, nikidai haki ya watoto wangu. Alizuiwa kuuza na nilipewa haki kwa niaba ya watoto wangu. Nililazimika kukabiliana na kuwashinda viongozi wa kimila kumi na mmoja ambao walikuwa wanapinga wanawake wa kabila la Wameru kurithi ardhi,” anasema Rosemary Peniel Nanyaro, Mwenyekiti wa Patanumbe.
Katika tukio lingine, Rosemary ambaye amebobea katika masuala ya haki za wanawake, alimsaidia mjane mmoja ambaye familia yake ilitaka kupora ardhi yake, kwa kuwasilisha shauri hilo katika Ofisi ya Mtendaji Kata, na kufanikiwa kurejeshewa shamba lake.
“Nashukuru sana kwa kile nilichojifunza kutoka CEDESOTA, nimejengewa ujasiri wa kuzungumza na wazee na wanajamii wengine kuhusu umuhimu wa haki za wanawake na watoto wa kike. Pia haki ya kushiriki na kufanya maamuzi pamoja na kuwania nafasi za uongozi,” anasema Dina Willian Laizer, Mjumbe wa Jukwaa.
“Elimu niliyoipata, imeniongezea werevu na ujasiri, kwa sababu nimeweza kufahamu haki za wanawake na kuweza kuongoza kitongoji chenye watu 250. Hivi sasa nafikiria kuwania Udiwani. Naamini naweza kuongoza jamii yangu, na watu wataniunga mkono,” anasema Mariam Daudi Msemo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji.