AZAKI yashirikiana na Serikali za Mitaa kuboresha ufatiliaji kwenye kilimo wilayani Tunduru

Jukumu la kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma za kilimo ni jukumu la kila mmoja kwenye sekta hiyo. Na kipekee kabisa, wananchi wana nafasi na jukumu la kufuatilia na kuhoji uwajibikaji na matumizi ya rasilimali za umma kwenye kilimo pamoja na kufuatilia vyama vya ushirika vya wakulima na mfumo wa usambazaji pembejeo za kilimo katika jamii zao.

 

Asasi ya Tunduru Paralegal Centre (TUPACE) imekua ikijitahidi kwa miaka miwili sasa kujengea uwezo wananchi na jamii ili waweze kufuatilia uwajibikali kwa jamii na matumizi ya rasilimali za umma kwenye kilimo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma. Asasi hii imekua ikishirikiana na viongozi wa serikali za mitaa , jamii na wataalamu wa serikali wa kilimo. Jukumu lao la msingi lilikua ni kuanzishwa kwa Kamati za Kata za
PETS na kuwapatia elimu na nyenzo za kufanikisha kazi yao. Juhudi hizi zilihusisha Kata nne za Nakapanya, Ligoma, Majengo na Mlingoti Mashariki kama sehemu ya majaribio kabla ya kwenda kwenye eneo kubwa zaidi la utekelezaji. TUPACE waliamua kujenga uwezo wa wananchi na jamii baada ya tathmini yao kuona kuna mapungufu makubwa kwenye uwajibikaji na matumizi ya rasilimali za umma kwenye sekta za kilimo wilayani Tunduru. Na kazi ya kwanza ilikua ni kushirikiana na serikali za mitaa na kuhakikisha kila Kata ina Kamati ya PETS.

 

Tathmini ya mwanzo ya ndani ilionyesha kwamba TUPACE kama asasi ilihitaji kujengewa uwezo kabla ya kuanza kutekeleza mradi huu. Hivyo walipata ruzuku na huduma za kujenga uwezo wao kitaasisi kutoka Foundation for Civil Society (FCS). FCS ni moja ya wawezeshaji wakubwa sana wa AZAKI kupitia ruzuku na huduma za kujenga uwezo wa Asasi nchini Tanzania. Wamefanya hivi kwa miaka 17 sasa wakifikia asasi zaidi ya 5650 Bara na visiwani Zanzibar.

 

Mchakato wa kupata Kamati ya Ufuatiliaji (PETS) ulihusisha serikali za mitaa za kila Kata waliotoa tangazo na kuchagua wajumbe kutokana na vigezo walivyojiwekea. Kamati hizi zilizingatia ushiriki wa wanawake na wanaume. Baada ya hapo, jukumu la mafunzo maalum ya ufuatiliaji uwajibikaji kwa jamii na matumizi ya rasilimali za umma yalifanywa na TUPACE kwa kushirikiana na wataalamu wa serikali wilayani . Mafunzo hayo yalihusu masuala yote ya msingi kuhusu PETS, mipango na bajeti na jinsi ya kuzisoma na kuzifatilia.

 


Jukumu la kujitolea kwenye ufuatiliaji
Habiba Said (24) ni mjumbe kijana wa Kamati ya PETS ya Kata ya Nakapanya. Anaishi na mama yake na anaweka akiba ili baadae akasomee taaluma ya Uuguzi. “Nilituma maombi ya kujiunga kijijini kwangu na kisha kuhudhuria mafunzo ya TUPACE ya masuala ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya kilimo. Kazi hii kwa kweli ni ya kujitolea tu. Hatulipwi ujira wowote. Lakini tunajtoa ili kuona bajeti zetu za kilimo zinatumika ipasavyo” anasema.
 

Habiba ni miongoni mwa wajumbe 10 wa mwanzo kabisa wa Kamati ya PETS ya Nakapanya. Kutokana na changamoto nyingi za kuhudumia vijiji kwa kujitolea, wanakamati  wengi wamejitoa kwenye kamati. Pamoja na changamoto hizi Mtendaji wa Kata ya Ligoma Bi Asha Amanzi anabainisha kuwa juhudi za AZAKI ya TUPACE zimesaidia kujenga jamii katika masuala ya kufuatilia uwajibikaji na matumizi ya rasilimali za umma. “Sasa kuna nidhamu na uwajibikaji kwenye pesa za umma. Kuna nidhamu ya matumizi ya hizi fedha katika miradi na wananchi wanashiriki katika kila hatua ya utekelezaji. Kwa sasa kwenye kilimo kama kuna shida yoyote kwenye usambazaji wa pembejeo wananchi wanatoa ripoti haraka sana. Hii inarahisisha sana utendaji kazi wetu kama watumishi wa umma” anasema.

 

Kabla ya jitihada za TUPACE huko Ligoma, jamii ilitingwa na changamoto nyingi sana – chagamoto za usambazaji wa pembejeo, upungufu wa maafisa ugani na ugumu wa kufikiwa vijiji vyote kwa maafisa hawa kutokana na ukosefu wa usafiri. Pia wananchi walikosa mwamko kuhudhuria mikutano ya kijiji na kufatilia taarifa katika mbao za matangazo. Hawakua na mwamko wa kuhoji masuala ya msingi yahusuyo jamii yao na hawakutaka kushiriki vyema kwenye ufuatiliaji.

 

“Kwenye kilimo, wananchi hawakufata kilimo bora. Sikujiona nikiwa bize sana kwani hawakunihitaji. Lakini baada ya kampeni za hamasa na kuelimisha kuhusu ufuatiliaji (PETS) sasahivi nazungukia kila kijiji kutokana na kuhitajika kwa wakulima wengi. Uhitaji ni mkubwa mpaka nazidiwa. Hii imeboresha sana shughuli za kilimo” anasema Zawadi Hassan, Afisa Ugani wa Kilimo wa Ligoma.

 

Uchakachuaji wa wafanyabiashara wasio waaminifu kwenye usambazaji wa pembejeo ulipaisha bei ya mbolea kwa zaidi ya 100% kutoka shilingi 30,000 iliyowekwa na Serikali. Mfumo wa stakabadhi ulikua mzigo sana kwa mkulima. Ushirikiano wa karibu kati ya Kamati za Ufuatiliaji (PETS) na serikali za mitaa kwenye Kata ulifanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyapeleka Halmashauri ya Wilaya na hatua kali zilichukuliwa. Pia ikaamuliwa kutumia mfumo wa malipo kupitia benki badala ya vocha/stakabadhi. Hii ilihakikisha kuwa ni wakulima waliohakikiwa tu kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika ndio walipokea malipo kutokana na mauzo ya mazao yao. Mfumo huu unalenga kuwatoa kabisa kwenye mnyororo wa thamani wafanyabiashara wasio waaminifu na wachakachuaji. Jitihada za TUPACE za kujenga uwezo wa jamii na wananchi katika ufuatiliaji kwenye kilimo zinalenga kutatua matatizo kama haya kwenye sekta ya kilimo.

 

Zaidi ya kutoa fursa kwa wahamasishaji wa kujitolea kwenye jamii kujiunga na Kamati za PETS na kufuatilia kilimo kwenye vijiji vyao, pia kamati zimewajenga vijana katika masuala ya kutumikia jamii zao. Wamehamasisha wenzao na wanavijiji wote kupata taarifa kupitia mbao za matangazo na kushiriki kwenye mikutano ya kijiji na kuhoji maswali yahusuyo maendeleo yao.
“Fursa hii imenijenga binafsi kama balozi wa masuala ya ufuatiliaji wa uwajibikaji katika kijiji changu. Nimejifunza mengi nje na shule. Sehemu ya majukumu yangu kwa sasa ni kuelimisha, kuhamasisha na kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma kijijini kwangu” anasema Hassan Njongonda,Mjumbe wa Kamati ya PETS ya Kijiji cha Makoteni, Ligoma.

 

Kwa upande mwingine, Subira Njaidi kutoka Kamati ya PETS ya Kijiji cha Ligoma anasema kuwa fursa ya kujitolea kwenye kazi ya ufuatiliaji (PETS) imemkutanisha na watu wengi sana. “Nimejifunza mengi sana toka kwa watu kuhusu uongozi, ufuatiliaji na masuala ya kujitolea. Kwa sasa ninaweza kusoma na kuelewa bajeti na pia kufuatilia masuala yote ya msingi kwa jamii yangu” anaongeza.

 

Mtendaji wa Kata ya Ligoma anaamini kwa dhati kuwa TUPACE wamemwongezea nguvu kazi kupitia Kamati ya PETS. “Vijana hawa wanajitolea kwa dhati kwa ajili ya jamii zao pamoja na changamoto zote. Hawana usafiri lakini wanakwenda kwenye vijiji vyao na kuhudumia wakulima. Hawana bajeti ya mawasiliano lakini wanawasiliana na ofisi yangu na zile za maofisa wengine wa serikali kufuatilia au kutoa ripoti ya utendaji wao. Tunahitaji kuwajenga na kuwawezesha zaidi ili kazi yao iwe rahisi kwa vyovyote tuwezavyo” anasema.