Kwa muda mrefu Mbeya imekua moja ya mikoa inayounda ‘Kapu la Kulisha Taifa’ hapa Tanzania kutokana na uwezo wa kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara. Hii inatokana na kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba, maji mengi, hali nzuri ya hewa kwa kilimo cha mwaka mzima na wenyeji wachapa kazi. Bahati nzuri, wasifu huu mzuri unawaamsha vijana wengi kwa sasa mkoani hapa kujitambua na kushiriki mchakato wa maendeleo. Asasi Za Kiraia (AZAKI) zina mchango mkubwa sana kwenye nadharia hii.
Maelfu ya kilomita kutoka Dar es Salaam, Mji Mkuu wa Biashara wa Tanzania, huko Bujingijila, juu kabisa katika Ukanda wa Nyanda za Juu za Kusini, unakutana na vijana wa Kikundi cha Wafugaji Samaki katika Halmashauri ya Busokelo, mkoani Mbeya. Hali ya hewa huku ni sawa na unapofungua jokofu likakupiga na upepo wake wa baridi. Lakini ukiangalia pande zote ni kijani kubichi na ardhi yenye rutuba sana. Na maji ya kutosha. Hapa ndio vijana hawa wameamua kufuga samaki kisasa kabisa wakifata maelekezo ya kitaalamu na ushauri toka kwa Maafisa Ugani na wa Maendeleo wa Serikali hapa Busokelo.
AZAKI na Serikali za Mitaa
Ili kuwafikia vijana na jamii ya wilaya hii, asasi inayotoa msaada wa kisheria ya PPJ ilitathmini changamoto zilizopo na kufanikiwa kuunganisha wadau ili kuzitatua. Walipata ushirikiano mkubwa toka Halmashauri ya Busokelo, Wilayani Rungwe, na kuunganishwa na Idara husika za Maendeleo ya Jamii. Juhudi hizi zikapata ruzuku na uwezeshaji kiufundi toka taasisi ya Foundation for Civil Society. FCS ni watoa ruzuku wakubwa kwa Asasi Za Kiraia (AZAKI) nchini Tanzania na wamekua wakifanya hivi kwa zaidi ya miaka 18 wakifikia AZAKI zaidi ya 5,700 kote Bara na visiwani Zanzibar.
Hapa Bujingijila ni Ukanda wa Juu kabisa na kuna baridi kali. Lakini unakuta mabwawa kadhaa ya kufugia samaki ya ukubwa wa robo mpaka ekari nzima. Yapo mengi katika sehemu iliyozungukwa na maji yanayotiririka kwenye chemchem yakielekea bondeni. Hiki ndio kitovu cha Kikundi cha Vijana wajasiriamali wafugaji samaki wa Busokelo. Ni wanachama wa Jukwaa la Vijana la Kata ya Kandete, mojawapo ya majukwaa manne katika Halmashauri hii. Mengine yapo Lwangwa, Itete na Lufilyo.
Changamoto kwa Vijana na jamii
Karibu sekta zote za maendeleo zina changamoto hapa, hasa kwa vijana. Nafasi za masomo ni chache na pia wakimaliza shule wanakosa mafunzo ya stadi za maisha kuwaandaa kupata ajira katika nyanja mbalimbali. Kwenye kilimo na ufugaji kuna ukosefu wa pembejeo na weledi wa uendeshaji kisasa. Ukishavuna shida kubwa ni masoko ya mazao.
Huku kunazalishwa maziwa mengi ya ngombe, kunalimwa ndizi, mahindi, kakao, kahawa na mazao mengine ya chakula kutokana na ardhi kuwa na rutuba nyingi. Lakini pamoja na yote, tathmini za PPJ zimeonyesha kuwa vijana wanatingwa na changamoto nyingi kujikwamua kimaisha.
Serikali inajitahidi kufanyia kazi changamoto lakini bado vigumu kufikia jamii pana kutokana na uwezo mdogo. Hivyo kusaidia juhudi za serikali katika vipaumbele vyake, AZAKI zimekua mstari wa mbele kuunganisha ushiriki na juhudi za wananchi kutatua changamoto zao za maendeleo. PPJ ikajikita kwa vijana.
Changamoto kubwa ya kwanza ni kufikia vijana wa Halmashauri kutokana na jiografia na miundombinu yake. “Ni vigumu kuwafikia vijana maeneo ya huku. Ni milimani na kuna changamoto kuwakusanya sehemu moja kwa ajili ya maongezi au mjadala” anasema Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kandete, Bw Guardian Noah, ambaye amefuatana na ziara hii akitumia pikipiki yake ya serikali. Ndio usafiri wake anapohudumu.
Na ukiweza kuwafikia, vijana wengi hawajitambui nafasi na majukumu yao kwa jamii. Hawajui thamani yao kwa taifa. Na hii, kwa mujibu wa tathmini ya PPJ, inaleta tofauti kubwa sana kati ya vijana hawa na wale wa maeneo ya mijini. “Changamoto ni nyingi, uelewa mdogo wa kutambua rasilimali na fursa zitolewazo na Serikali. Hapa tukaona kuna haja ya kuwaweka vijana pamoja, waelImishwe na waongee pamoja. Wachukue mustakabali wao mikononi mwao” anaongeza Bw Gabriel John, Mratibu wa PPJ.
Matokeo ya juhudi za AZAKI na serikali
Juhudi za kwanza za PPJ kwa kushirikiana na Halmashauri zililenga kuwafikia na kuwaunganisha vijana katika maeneo yao. Hapa ndipo majukwaa ya vijana yalianzishwa Katika Kata za Kandete, Lwangwa, Itete na Lufilyo yakiwa na wanachama 204 (Me=130, Ke=74). Serikali ilitoa malekezo juu ya uratibu wa zoezi na Halmashauri kutoa usajili na kutambua majukwaa haya katika ngazi ya Kata.
Majukwaa haya yaliwezesha kampeni za hamasa na mafunzo kwa vijana katika masuala mengi ikiwemo kuitambua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007. Walihamasishwa kushiriki na kujihusisha na ufuatiliaji wa mustakabali wao kupitia mikutano ya jamii. Hii iliwapa ujasiri wa kushiriki mikutanoni, kuhoji na pia kuwania nafasi za uongozi wanazotengewa kisheria kwenye Kata.
Vikundi vya Uzalishaji
Kupitia majukwaa haya kulianzishwa Vikundi vya Vijana vya ujasiriamali. Ustawi wa vikundi hivi uliongeza uhitaji wa kusajiliwa na kutambuliwa rasmi na Halmashauri. Uliwezesha utoaji wa mikopo toka 4% iliyotengwa kisheria kwa ajili ya vijana toka mapato ya Halmashauri. Mikopo hii iliongeza nidhamu ya kazi, uwekaji akiba na kwa ujumla upatikanaji wa huduma za kifedha kwa vijana na jamii wanazotoka.
Kikundi cha Wafugaji Samaki Bujingijila, Kata ya Kandete: Wana mabwawa matatu ya ukubwa tofauti wakiwekeza vifaranga 3,000 katika bwawa dogo na 15,000 na 45,000 kwenye mengine. Wanategemea kuvuna mwezi Septemba. Kikundi kimesajiliwa na wamepata mkopo wa Shilingi milioni 4 toka Halmashauri ili kupanua shughuli zao.
Kikundi cha BUKYE, kutoka Jukwaa la Vijana Kata ya Lwangwa. Hawa ni wajasiriamali wa usindikaji wa bidhaa za kilimo na utengenezaji wa sabuni. Wanazalisha achali mbalimbali za matunda na mbogamboga na kusindika viungo. Wamefanikiwa zaidi baada ya kupata mkopo wa Shilingi milioni 7 toka Halmashauri. “Busokelo kuna mazao mengi yanapotea kila msimu. Sisi baada ya mafunzo tuliamua kuanzisha ujasiriamali kuongeza thamani kwa usindikaji viungo na kutengeneza mvinyo” anasema Ahazi Mwanyombole, Afisa wa Kikundi.
Kikundi cha JUHUDI, Kata ya Kandete: Wanalima mbogamboga katika shamba la ekari moja kwa sasa. Walipatiwa mkopo wa Shilingi milioni 4 kupanua shughuli zao. Wakati wa utafiti wa ripoti hii, walikua wanajiandaa kuvuna wastani wa matenga 400 ya nyanya msimu huu, waliyopanga kuuza kwa Shilingi 20,000 kwa tenga (wanategemea pato la Shilingi milioni 8 kwa msimu).
Kwa kipindi cha Septemba 2017 – Desemba 2018 Halmashauri ya Busokelo imeshatambua na kusajili vikundi 67 vya vijana, wote wakiwa wanachama wa majukwaa katika Kata. Kati ya hivyo vikundi, 30 vimepatiwa mikopo inayofikia zaidi ya Sh 78,000,000 kati ya milioni 85,000,000 kwa kipindi hicho. Pia vijana wanne (Ke=2, Me=2) wameingizwa katika Kamati mbalimbali za uongozi katika jamii zao.
Ushirikiano na ufanyaji kazi pamoja kati ya AZAKI na Halmashauri ni moja ya sababu ya juhudi za PPJ kufanikiwa. Ila bado uhitaji ni mkubwa sana kwa maeneo ambayo hayajafikiwa. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo Bw Paul Ngilangwa anatoa rai kwa PPJ kuongeza juhudi ili kupanua shughuli zinazolenga vijana na kuwapa hamasa, kujitambua na uelewa kuhusu fursa zinazowazunguka katika jamii na nafasi na haki zao kisheria kufaidika na zile 4% zilizotengwa toka mapato ya kila Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya vijana.
“Juhudi zenu zitawafungua macho vijana waone hizi fursa. Nasisitiza sana kwenye hili. Kwa sasa tunafanya jitihada kama Halmashauri ili wale vijana wafuga samaki wapate hati ya kimila ya maeneo ya kufugia. Hii itawapa uhuru wa kupanua shughuli zao” anaongeza Bw Ngilangwa. Wakati wa ziara hii, vijana wafugaji wa Bujingijila walikua wanajiandaa na ziara kubwa ya Mwenge wa Uhuru, ukiwa ni mmoja wa miradi iliyowekwa kwenye ajenda ya ziara. Kiwango hiki cha kutambulika na kupewa usaidizi na hamasa toka serikalini kinaipa moyo sana Asasi ya PPJ na kuwapa chachu ya kutaka kuongeza juhudi zaidi kufikia vijana wengine katika maeneo yaliyo nje ya mradi.
Changamoto bado nyingi
Pamoja na juhudi zote na ushirikiano baina ya wadau wote, bado vijana na jamii ya Busokelo wanazuiwa na changamoto nyingi. Kwa Asasi ya PPJ, wao wanatingwa zaidi na uhitaji mkubwa wa mradi na changamoto waliyopewa na Halmashauri kufikia jamii pana zaidi. Hii inawawia vigumu kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Kwa vijana wengi wanachama wa vikundi vya ujasiriamali, wao wana mahitaji ya mafunzo zaidi ya stadi za maisha na ujasiriamali. Pia ukosefu wa masoko kwa bidhaa wanazozalisha kwenye miradi yao unazuia upanuzi wa uwekezaji wao. Na zaidi ni ukosefu wa mitaji kwa shughuli za ujasiriamali zinazoongezeka kwenye vikundi baada ya mafunzo.