FCS imeanza utekelezaji wa mpango mkakati wake mpya ambao utadumu kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2022 hadi 2026. Katika Mpango Mkakati huu, FCS imebadili na kuboresha programu na mbinu zake. Lakini eneo la kijiografia litakalofikiwa na programu zake limebaki kuwa ni nchi nzima, Tanzania bara na Zanzibar (Unguja na Pemba. Hata hivyo, maeneo ya kipaumbele ya kijiografia yataainishwa kila mwaka kwa kila eneo la maudhui ya programu kulingana na vipaumbele vya kitaifa, takwimu za kitaifa na kadri itakavyoamuliwa mara kwa mara kuendana na mabadiliko ya mazingira husika. Wanufaika wakuu wa miradi ya FCS ni wananchi wa Tanzania hasa makundi ya watu maskini zaidi (wanawake na wanaume), wanawake, watoto, watu wenye ulemavu, vijana na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi na yaliyotengwa nchini Tanzania.
Mbinu
Utoaji wa Ruzuku
FCS itaendelea kutoa ruzuku kwa AZAKi. Hata hivyo, tofauti na mkakati wa awali, kapu la ruzuku litabadilika kulingana na rasilimali zitakazokusanywa kila mwaka. Pia FCS itafanya kazi na washirika wawezeshi (mashirika ya kitaalamu au makampuni binafsi yenye utaalam unaofaa kwa maeneo ya maudhui ya kipaumbele ya programu za FCS). Washirika wezeshi wataunganishwa na washirika wa utekelezaji ili kutoa ushauri na ujuzi wa kiutaalamu kulingana na maudhui husika.
Mchakato wa kuomba ruzuku pamoja na Maswali na Majibu
Maswali na Majibu
Kwa maelezo zaidi juu ya maswali na majibu katika utoaji wa ruzuku FCS tafadhali fuatilia zaidi kiunganishi hapa
Utekelezaji wa Moja kwa Moja
Utekelezaji wa Moja kwa Moja ni utaratibu ambapo FCS inachukua jukumu kamili la kuhamasisha na kutumia ipasavyo rasilimali zinazohitajika ili kupata matokeo yanayotarajiwa. Hivyo, FCS itachukua jukumu la jumla la usimamizi na uwajibikaji kwa utekelezaji wa mradi. FCS itashiriki kwenye utekelezaji wa moja kwa moja kupitia miradi maalum iliyopo au itakayoanzishwa. FCS inawaalika wafadhili wanaopenda kushirikiana nasi kupitia utaratibu usiyo wa mfuko mkuu wa ufadhili wawasiliane na FCS kwa ajili majadiliano ya namna ya kufanya kazi pamoja.
Ubia/Ushirikiano
FCS inakaribisha Asasi za Kiraia zilizo kwenye mfumo mkuu na vikundi vya kijamii kuomba ushirikiano na FCS kwa madhumuni ya kubuni miradi pamoja, kuchangia rasilimali na kujenga hisia za umiliki wa miradi na uendelevu. FCS itahakikisha inafanya tathmini na uchunguzi wa kina kwa mbia/mshirika anayeomba kabla ya kuanza kufanya naye kazi.
Maeneo ya vipaumbele ya programu kwa mwaka 2022 – 2026
Usawa wa Kijinsia, Watu wenye Ulemavu na Ujumuishwaji wa vijana
Katika kipengele hiki cha programu, FCS inatarajia kuwa ifikapo mwaka 2026 katika maeneo ya vipaumbele ambayo FCS inafanyia kazi, makundi ya wananchi yaliyotajwa kama walengwa wakuu yatapata fursa na rasilimali zinazohitajika kushiriki kwenye maswala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni na kufurahia maisha bora zaidi ndani ya jamii wanamoishi.
Maisha Endelevu
Katika kipengele hiki cha programu, FCS inatarajia kufikia matokeo mawili jumuishi ifikapo mwaka 2026 i) Vijana, watu wenye ulemavu na wanawake wameongeza uwezo wa kupata rasilimali za uzalishaji, masoko na ajira ii) Jamii imeongeza uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi endelevu ya maliasili.
Utawala bora
Katika kipengele hiki cha programu, FCS inatarajia kufikia matokeo mawili jumuishi ifikapo mwaka 2026 : i) Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) kwenye maeneo tunayofanyia kazi zinatoa huduma bora zaidi ii) wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye michakato ya uchaguzi ambayo ni huru zaidi, halali na jumuishi.
Kulinda Amani na ushirikiano wa kijamii
Katika kipengele hiki cha programu, FCS inatarajia kwamba ifikapo mwaka 2026, maeneo ya vipaumbele kuhusu jamii yanayofanyiwa kazi na FCS, yatakuwa na ufanisi zaidi katka kushughulikia migogoro.
Jinsi tunavyowapata wabia wa kufanya kazi na FCS kupitia utoaji wa ruzuku.
Kila mwaka FCS itabainisha vipaumbele vya kiprogramu na kijiografia kulingana na mazingira halisi. Uwekaji huu wa vipaumbele utakuwa msingi wa FCS katika kujielekeza kwenye miradi na programu katika mikoa mbalimbali. Kwa mfano, kujielekeza kwenye miradi ya kukomesha Ukatili wa Kijinsia itakuwa kwenye mikoa viliko shamiri vitendo vya ukatili wa kijinsia nk.
Taratibu za kufuata kwa Mashirika yanayopenda kufanyakazi na FCS mwaka 2022-2026.
Usajili mtandaoni kwa shirika linalotaka kufanya kazi na FCS umefunguliwa rasmi. Usajili wa mtandaoni ni ukurasa wa tovuti ya washirika mtandaoni ambao huiwezesha FCS kuwabainisha washirika wake kulingana na maeneo ya vipaumbele vya programu na mikoa waliko. Kwa Mashirika yote yanayotaka kufanya kazi na FCS hakikisha kuwa umesajili shirika lako kwenye tovuti ili uweze kupata matangazo ya wito wa kutuma dokezo la mradi na fursa nyingine za ufadhili kutoka FCS. Tafadhali soma kwa makini Mwongozo wa Upatikanaji Ruzku (PREG) kwa maelezo zaidi kuhusu usajili wa mtandaoni. AZAKi zinazopenda kufanyakazi nasi zitahitajika kujisajili kwenye Mfumo wa kidigitali katika tovuti wa wabia kwa kuandika maelezo ya wasifu wa mashirika yao. Mwombaji atatoa taarifa zinazohitajika kama inavyoelekezwa na taarifa za washirika iliyopachikwa kwenye tovuti ya wabia. Kanzidata itakuwa wazi muda wote, ili AZAKi ziweze kusajili na kuhuisha taarifa zao kwenye kanzidata muda wowote wanapoona wanahitaji kufanya hivyo. Kiunganishi cha tovuti hii ni hiki www.smartgrants.co.tz/partnerportal,
MADIRISHA YA UFADHILI
Foundation itakuwa na madirisha matatu ya kutoa ruzuku kwa mashirika mbalimbali nchini Tanzania.
Dirisha la Kutuma Maombi
Dirisha la ufadhili la kuombwa ni dirisha muhimu zaidi kwa AZAKi kupata ruzuku kutoka FCS. Dirisha hili litatekelezwaa kupitia mbinu ya kutoa wito wa kuomba ruzuku. Litaruhusu AZAKi zote ambazo zina akaunti zilizosajiliwa (Ubainishaji wa wabia/washirika) katika tovuti ya usimamizi wa ruzuku na kukidhi vigezo vya chini kupata fomu ya maombi na hivyo kuweza kuijaza na kuwasilisha maombi yao ya ruzuku.
Dirisha la Ruzuku Maalum ya haraka
Mojawapo ya maadili ya msingi ya FCS ni uwezo wa kubadilika ili kukidhi mahitaji ya wakati na wepesi kwa kuzingatia kwamba muktadha unabadilika kila wakati. FCS inatoa fursa ya dirisha maalumu la ruzuku ya haraka ambayo haiko kwenye dirisha la kutuma maombi kawaida. Chini ya dirisha hili FCS itatoa ufadhili wa haraka kwa mashirika ili kushughulikia changamoto/matukio yaliyoibuka ambayo asili yake yanahitaji kushughulikiwa haraka au yana matokeo chanya ndani ya muda mfupi.
Aina hii ya ufadhili inalenga kushughulikia masuala ya dharura yanayoibuka pasipo kutarajiwa au ambayo utekelezaji wake utakuwa na matokeo ya haraka kwa jamii kwa mfano, Mapitio ya Sera yanayohitaji mchango wa haraka wa AZAKi, au masuala yanayoibuka kwa dharula mara kwa mara. Kwa matukio ya aina hiyo, menejimenti itajadili na kuamua juu ya ufadhili huo kwa kuhalalisha kwa uwazi na inaweza kuidhinisha hadi Tsh 50,000,000 kwa tukio husika. Hata hivyo, jumla ya kiasi kitakachotengwa kwa ajili ya kushughulikia haraka miradi au masuala yanayoibuka kwa mwaka haitazidi Tsh 200,000,000.
Dirisha la Miradi Maalum na isiyo chini ya mfuko mkuu wa ufadhili
Mara kwa mara FCS husimamia fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya ufadhili nje ya wafadhili wakuu. Mara nyingi miradi hii hulenga maeneo maalum ya afua/shughuli. Mahitaji ya miradi kama hii yanaweza kuwa tofauti na yale ya wafadhili wa bajeti kuu. Kwahiyo, FCS itatoa ruzuku kwa mashirika kulingana na mahitaji ya wafadhili, maeneo ya kipaumbele, makundi lengwa na makubaliano yaliyofanywa kati ya FCS na Wafadhili. Katika dirisha hili, ufadhili hauwezi kufuata taratibu za FCS katika mfumo wa usimamizi wa ruzuku. Baadhi ya taratibu zinaweza kurukwa kulingana na makubaliano yaliyofanywa kati ya pande hizo mbili.
Aina ya Ruzuku na muda wake
FCS inatoa ruzuku za aina tatu (3). Aina hizi zinatofautiana kutokana na aina ya mashirika. Zifuatazo ni aina za ruzuku zinazotolewa na FCS:
Ruzuku ya Kimkakati
Hii ndiyo ruzuku kubwa zaidi ambayo FCS itakuwa ikitoa na inalenga mitandao makini ya Asasi za Kiraia, mashirika mwamvuli na Asasi za Kiraia zinazofanya kazi katika ngazi ya Kitaifa zenye rekodi nzuri ya usimamizi wa fedha na mafanikio makubwa ya kitaifa yanayoonekana. Mashirika ya aina hii yatafadhiliwa kama “viongozi wa Klasta” yaani, kwa mfano – Kiongozi wa programu ya Ufuatiliaji wa Matumizi ya fedha za Umma au Ufuatiliaji wa Uwajibikaji kwa Jamii. Mashirika yatakayofadhiliwa chini ya dirisha hili ni yale yanayoandaa programu zao kwa namna ambayo wataweza kufanya kazi na AZAKi za jamii zinazoshughulikia maudhui yanayofanana na kazi zao kuu na kutumia mafunzo/ushahidi uliopatikana kutoka ngazi ya jamii kushawishi utetezi wa ngazi ya kitaifa huku wakitumia mambo waliyojifunza ngazi ya taifa kuboresha utekelezaji wa miradi ama shughuli zinazofanyika ngazi ya jamii
Ruzuku za Kati
Ruzuku za Kati zinachukua sehemu kubwa ya ruzuku za miradi zinazotolewa na FCS. Aina hii ya ruzuku inalenga mashirika ambayo yameomba ufadhili ndani ya viwango vya bajeti vilivyoainishwa kwenye tangazo kwa mashirika kuomba ruzuku na yamepitia tathmini na kuonesha uwezo wa kusimamia fedha na miradi.
Ruzuku ndogo
Dirisha hili linatoa fursa kwa kwa mashirika madogo, mapya na yanayochipukia yenye mawazo mazuri sana ya kutatua changamoto kwenye maeneo yao kupata ruzuku kutoka FCS. Msaada huo hautanufaisha AZAKi pekee bali pia vikundi vya kijamii (vilivyosajiliwa au visivyosajiliwa), watu binafsi na mashirika mapya. Inalenga mashirika ambayo yamefanya kazi kwa muda usiozidi miaka 2 na ambayo kwa hakika hayana ripoti za ukaguzi wa kitaasisi lakini yana taarifa za fedha zilizoidhinishwa.
Aina ya Ruzuku | Kiasi kwa mwaka (TZS) | Ukomo wa kipindi cha ruzuku | Mamlaka ya Uidhinishaji |
Ruzuku ya Kimkakati | 80,000,000-150,000,000 | Miaka 2 | Bodi ya FCS |
Ruzuku ya Kati | 31,000,000-79,000,000 | Miaka 2 | Menejimenti ya FCS |
Ruzuku ndogo | 0-30,000,000 | Miaka 2 | Menejimenti ya FCS |
Kanuni na vigezo vya Jumla vinavyotumika Kuchagua mradi
Kanuni kuu inayoongoza uamuzi wa kuchagua mradi wowote ili ufadhiliwe na FCS ni kwamba, afua/shughuli zilizopangwa za mradi lazima zilete manufaa yanayoonekana (ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja) kwa wananchi wa mikoa inakofanyakazi. Kanuni nyingine, mahususi zinaongoza mchakato wa kuchagua mradi ni pamoja na;
Vigezo Maalum vya uteuzi na uidhinishaji wa mradi (Vigezo vya uteuzi na uidhinishaji): Pamoja na vigezo vya jumla vilivyowekwa juu ya vyombo maalum vya uteuzi na uidhinishaji vitazingatia vigezo muhimu vifuatavyo katika mchakato wa kuchagua na uidhinishaji.
Uchaguzi wa washirika wengine
Kwenye Mpango mkakati wake wa mwaka 2022-2026, FCS imedhamiria kufanya kazi na asasi za kiraia nyingi zaidi yakiwemo makundi ya kijamii pamoja na watu binafsi ambao wanaonekana kuwa muhimu kwa muktadha na matokeo yaliyolengwa. Baadhi ya makundi hayo yanaweza kuwa:
Tafadhali soma Mwongozo wa Upatikanaji Ruzuku (PREG) kwa taarifa zaidi kuhusu utaratibu wa FCS wa kufanya kazi na ASASI na vikundi mbalimbali
Ujumbe muhimu kwa waombaji watarajiwa na washirika
Tunatumai mwongozo huu umetoa maelezo ya kutosha juu ya utaratibu mpya ya kutoa ruzuku. Hata hivyo, kama unapenda kupata ufafanuzi zaidi kuhusu huduma na taratibu zetu za utoaji wa ruzuku kulingana na mkakati wetu mpya, tafadhali wasiliana na Bi Edna Chilimo – Meneja wetu wa Programu za Utawala bora na Ujumuishwaji Jamii kwa baruapepe hii echilimo@thefoundation.or.tz