Ruzuku

 

MAMBO MUHIMU YA KIMKAKATI

UTAWALA BORA

 

Programu ya Utawala inakusudia kupata matokeo matatu yanayoshabihiana kama ifuatavyo:-

  1. Ifikapo mwaka 2020, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zilizomo katika maeneo ambako FCS inafanya kazi na asasi za kiraia zitakuwa zinatoa huduma bora zaidi.
  2. Ifikapo mwaka 2020, kutakuwa na ongezeko la ushiriki wa wananchi katika vikao vya kufanya maamuzi na michakato ya kidemokrasia, hivyo kudhihirisha upatikanaji wa haki hasa kwa makundi ya watu wanaobaguliwa, kutengwa, watu wenye ulemavu  na walioko pembezoni katika maeneo yote ambako FCS inafanya kazi
  3. Ifikapo mwaka 2010, jamii itakuwa imejengewa uwezo mkubwa na kutakuwa na ongezeko la taasisi zenye uwezo wa kufanya majadiliano na kusimamia utatuzi wa migogoro.

 

Ili kufikia matarajio haya adhimu, FCS itafanya kazi kwa ukaribu na AZAKI za ngazi ya jamii na kitaifa na kuzifanya ziwe nyenzo muhimu ya kuwajengea uwezo wana jamii ili waweze kushughulikia masuala ya utawala.Matokeo ya mpango wa Utawala yatajikita katika maeneo manne:

  1. Ufuatiliaji wa uwajibikaji kwa jamii
  2. Haki za wanawake kumiliki ardhi na mali
  3. Kupambana na Mila potofu na Ushiriki wa Jamii
  4. Ujenzi wa Amani na utatuzi wa migogoro

 

Ili kufikia malengo haya, FCS itaziwezesha AZAKI ili kuwapa uwezo wananchi hasa makundi ya watu  wanaobaguliwa, watu wenye ulemavu, jamii za watu wachache na wanawake ili washiriki katika kutunga sera, kufuatilia bajeti, kudai uwepo wa uwazi na haki ya kushiriki kwa njia ya kutoa mapendekezo na madai yao kuhusu sera kwenda serikalini na bungeniTaasisi ya FCS itaziwezesha AZAKI kuimarisha uwezo makundi ya watu wanaotengwa wakiwemo watu wenye ulemavu ili wadai haki yao ya kushiriki katika vikao vya kufanya maamuzi na kufanya utetezi wa haki za vijana na wanawake. FCS inaamini kuwa kwa njia hii, watu waliobaguliwa, wenye ulemavu, wanawake na vijana watalindwa, kutetewa na kufaidi haki zao. Kadhalika, FCS itafanya kazi kwa umakini mkubwa na asasi ili ziweze kufanya kampeni za kuimarisha amani, kuendesha mazungumzo kuhusu amani katika ngazi mbalimbali na kuwezesha uundwaji na uimarishaji wa mfumo wa kutatua migogoro katika jamii.   

 

KUJIKIMU NA MASOKO

Programu hii ina lengo la kupata matokeo matatu yenye kushabihiana. Malengo hayo ni:-

  1. Kuhakikisha kuwa vijana na wanawake wajasiriamali wanapata fursa ya kuyafikia masoko na rasilimali za kujikimu. FCS ina amini kwamba kama vijana na wanawake watadai haki zao na kuongeza ushirikiano wao na serikali za mitaa, kama watatoa changamoto kwa sera zilizopo, basi serikali za mitaa zitafanya kazi kwa uwazi zaidi hususan kuhusu fursa za wanawake na vijana, serikali za mitaa pia zitatenga bajeti kwa ajili ya wanawake na vijana na kutenga maeneo ya masoko kwa ajili ya wajasiriamali wanawake na vijana ili waweze kupata faida kutokana na biashara zao.
  2. Kuwawezesha wakulima wadogo kupata huduma za ughani na uhakika wa kumiliki mashamba yao. FCS inaamini kwamba kama AZAKI zitahamasisha na kuongeza uelewa kwa wakulima wadogo kuhusu huduma za ughani na jinsi ya kupata masoko, kuna uwezekano wa kuundwa kwa vikundi vya wakulima yenye ufahamu na stadi, na hivyo kuongeza mahusiano na serikali za mitaa na maofisa ughani. Kutokana na kujengewa uwezo, wakulima wadogo watadai haki yao na kutoa changamoto kwa sera na shughuli za utekelezaji wa sera hizo.
  3. Kuhakikisha kuwa jamii ina uwezo wa kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa na Usimamizi wa Mali Asili. FCS inaamini kwamba ikiwa AZAKI zitahamasisha jamii na serikali za mitaa na kuwezesha kuwepo na kiungo kati ya jamii, wanawake, vijana na wakulima wadogo wadogo na sekta binafsi, basi serilkali za mitaa zitatambua kazi na majukumu yao, jamii itakuwa na uelewa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na usimamizi wa mali asili. Kutokana na kuongezeka kwa uelewa na stadi, jamii itafuatilia na kudai usimamizi bora wa mali asili kutoka kwa serikali za mitaa na matokeo ya vuguvugu hili  la jamii, serikali za mitaa zitachukua hatua dhidi ya lawama kutoka kwa jamii kuhusu usimamizi wa mali asili.