Kuwawezesha Vijana

Kuwawezesha vijana ambao ndilo kundi kubwa katika

Vijana wanaunda kundi kubwa la nguvu kazi na lenye msukumo mkubwa katika maendeleo ya nchi hii. Hata hivyo, kundi hili linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira na kukosa elimu na huduma muhimu za afya.

Serikali ya Tanzania imetilia maanani sana suala la vijana katika mipango yake ya maendeleo. Mipango hii ni pamoja na kuwa na sera rafiki kwa masuala ya vijana na sheria mbalimbali kuhusu ushiriki wa vijana. Hivi karibuni serikali ilitoa waraka ukizitaka serikali za mitaa kutenga asilimia 4 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha vijana.

Katika kuunga mkono juhudu za serikali FCS inatoa ruzuku kwa asasi za kiraia zinazoendesha miradi yenye lengo la kuwapa vijana fursa ya kupaza sauti na kushiriki katika masuala ya kidemokrasia katika ngazi ya serikali ya mitaa, kata na vijiji.

FCS inawawezeshaje vijana?

FCS inawawezesha vijana kupitia ruzuku inayotoa kwa asasi za kiraia zinazotekeleza miradi yenye mikakati ifuatayo:

 1. Ushirikiano na serikali za mitaa kwa kuzingatia muundo wa serikali.
 2. Kutilia mkazo utekelezaji wa shughuli katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji/mitaa kama njia ya kuimarisha msingi katika ngazi ya taifa
 3. Kuanzisha na kuyaunga mkono mabaraza ya vijana kama njia ya kuwawezesha vijana kupaza sauti zao
 4. Kutumia njia shirikishi na rafiki za vijana kama vile Sanaa, michezo na burudani mbalimbali
 5. Kuwatumia mabalozi wa vijana, vijana mashuhuri na nhyota katika fani mbalimbali

Mafanikio

Katika mwaka wa fedha wa 2017/18 FCS iliziwezesha asasi 15 kutekeleza miradi katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Arusha, Mwanza na Pwani. Ruzuku iliyotolewa kwa asasi hizi ni zaidi ya Shilingi Milioni 688. Miongoni mwa shughuli zilizofadhiliwa na FCS ni pamoja na:

 • Uhamasishaji vijana kwa njia ya muziki na kuwajumuisha wanasanii
 • Kampeni za vijana na majadiliano kupitia majukwaa 108 yaliyoundwa pamoja na viongozi wao
 • Elimu kwa njia ya michezo kama njia ya kuwahamasisha vijana hasa jijini Dar es Salaam katika kata za Vingunguti na Buguruni
 • Matumizi ya nyenzo za Taarifa, Elimu na Mawasiliano kama vipeperushi, majarida na machapisho mbalimbali yenye ujumbe unaolenga Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007
 • Kampeni za uhamasishaji na uelimishaji jamii
 • Shughuli za kujenga uwezo katika masuala mbalimbali ikiwemo Uandaaji wa Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007

Matokeo

Kuundwa kwa majukwaa ya Vijana

Jumla ya majukwaa ya vijana 160 ya vijana yaliundwa kattika ngazi ya kata na wilaya na kuwa kiungo madhubuti kinachounganisha mitandao ya vijana na viongozi wa halmashauri

Vijana wanajadili masuala ya kiuchumi

Hivi sasa vijana wanaweka kipaunmbele zaidi katika masuala yanayogusa uchumi kuliko masuala mengine kwao.Licha ya miradi hii kuhusika na Utawala Bora lakini bado vijanawamepata fursa ya kukaa pamoja kutokana na kuona umuhimu wa kushirikiana katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali.

Serikali inaunga mkono juhidi za vijana

Katika baadhi ya maeneo yanakotekelezwa miradi ya vijana, serikali imesikia kilio cha vijana na inajihusisha kikamilifu kushughulikia masuala yao. Kwa mfano katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani serikali imetoa kibali cha vijana kumiliki sehemu ya ardhi kwa ajili shughuli zao za kilimo. Huko mkoani Mwanza, mabaraza ya vijana yamepata mikopo kutoka taasisi za fedha na kuanza kutekeleza miradi ikiwemo ya utengenezaji wa nguo za bariki, utengenezaji wa sabuni, kufungua maduka madogo na ufugaji. Jijini Dar es Salaam zipo juhudi za kuwapatia vijana kuiia vikundi vyao mitaji kwa ajili ya kufanya shughuli za ujasiriamali. Wilaya ya Ilala imetenga Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya mikopo kwa vijana. Hivi sasa mabaraza ya vijana yamo mbioni kujisajili na kuwasiliana na maafisa maendeleo ya jamii katika kata zao ili kuwaongoza jinsi ya kupata fursa za kiuchumi.

Ushiriki wa Vijana kuipitia Sera ya Vijana ya Mwaka 2007

Ushirikiano wa kimkakati umeanzishwa kati ya Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na sekta  ya kimkakati ya asasi za kiraia inachoshughulikia Uwezeshaji Vijana kama timu maalum yenye jukumu la kuandaa rasimu ya Sera ya Taifa ya Vijana. Hili ni jambo muhimu katika kuwapa uwezo vijana kushiriki katika kuandaa sera inayowahusu wao.

Ongezeko la ushiriki wa Vijana katika Utawala wa kidemokrasia na utawala bora

Vijana wamepata nafasi na kushiriki katika vikao na taasisi za maamuzi katika mitaa na kata zao. Taarifa hizi za kutia moyo zimeripotiwa kutoka mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Tanga, Pwani na Zanzibar

Vijana wamehamasika

Ongezeko la hamasa miongoni mwa vijana limeleta manufaa sana katika shughuli za maendelo ya jamii kama vile ujenzi wa miundo mbinu iliyoharibika wakati wa mvua.