Kujenga na Kukuza Uwezo wa AZAKI

Kujenga na kukuza uwezo ni shughuli ya msingi ambayo FCS inafanya kuendeleza dira yake na kuimarisha matokeo ya programu zake kwa jamii.

Huduma ya kujenga na kukuza uwezo wa AZAKI inayofanywa na FCS imebuniwa ili kuhakikisha kuwa mashirika yanafadhiliwa yanajengewa uwezo na kuimarishwa kila wakati ili yaweze kufikia malengo, kutoa matokeo yanayotarajiwa na kuyaandika kwa mpangilio mzuri ili kuhakikisha kuwa ushahidi wa mafanikio yaliyopatikana unatolewa kwa jamii. Tunaamini kuwa kuimarisha uwezo wa asasi za kiraia ni jambo muhimu sana linalowapa sauti wananchi na kuwaweka mstari wa mbele kwenye masuala ya utawala bora na michakato ya kujipatia mahitaji ya kuishi na kukuza uchumi ambayo ni sehemu ya maisha yao ya kila siku. Katika muktadha huu, mpango wetu wa kujenga na kukuza uwezo wa AZAKI umelenga kusaidia kuboresha utendaji, ukuaji wa taasisi na Asasi, vile vile uwezo wa kushirikiana na kufanyakazi pamoja na mashirika mengine.

Uwezo gani tunaojenga na kuimarisha?

FCS inayaangalia mashirika/Asasi kwa mtazamo wa Mifumo ambapo masuala, matukio na nguvu ndani ya mashirika havitenganishwi, bali vinahusianishwa. Kwa maana hiyo, msaada wetu kwenye kujenga na kuimarisha uwezo umeundwa katika nyanja tatu: Uwezo wa KUJIENDESHA, uwezo wa KUTENDAKAZI na uwezo wa KUSHIRIKIANA na wengine.

Uwezo wa Kujiendesha

Hii inajumuisha nguvu ya ndani na uwezo wa kitaasisi wa kujiendesha kama taasisi yenye nguvu, inayojiamini, yenye mikakati na uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe. Kwenye eneo hili AZAKi zitasaidiwa kukuza muundo bora wa uongozi na utawala, mikakati ya kina na mifumo stahiki ya ndani. AZAKi zitasaidiwa kufanya tathmini ya uwezo wa shirika.

Uwezo wa Kutendakazi

Huu umejikita kwenye program za kijamii za AZAKI ambazo zinahusiana na maudhui ya FCS ya program ya utawala na mahitaji muhimu ya maisha. Kwahiyo, ukuzaji wa uwezo kwenye eneo hili itajumuisha ujengaji wa uwezo wa aina mbalimbali unaohusiana na usimamizi wa mradi, Ujuzi wa kitaalamu kuhusu Ufuatiliaji wa Matumizi ya fedha za umma(PETS) na Ufuatiliaji wa uwajibijaki jamii(SAM), Unyanyasaji wa Kijinsia, utetezi wa haki za watu wenye ulemavu (PWD) na ushiriki wa wananchi kwenye michakato ya kidemokrasia.

Uwezo wa Kushirikiana na wengine

Hii inahusu uwezo wa kujenga mahusiano mazuri na mashirika na taasisi nyingine. Lengo la kuimarisha uwezo huu ni kuwezesha kukua kwa ushirikiano uliopo kati ya wadau wa maendeleo kama msingi wa kuwezesha mshikamano mkubwa, umoja, kuongeza kasi ya utendaji na kusambaza matokeo mazuri ya miradi sehemu nyingine za nchi.

Tunajenga na kuendeleza uwezo wa nani?

Kwa kuzingatia majukumu na wajibu wake wa kipekee wa kukuza AZAKI Tanzania, huduma za kujenga uwezo za FCS zimejikita kwenye kukuza uwezo wa watendaji na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwa ni pamoja na:-

  • Watu binafsi: Kama vile viongozi wa AZAKI, wafanyakazi wanaofanya kazi kwa kutembelea jamii, wanajamii, pamoja na wanawake na vijana, watunga sera na viongozi wengine wa serikali n.k. Tunatambua kuwa mabadiliko hutokana na athari za hatua anazochukua mtu mmoja mmoja na hatua za pamoja. Hata hivyo, mabadiliko kwenye ngazi ya mtu mmoja mmoja ni muhimu zaidi kwa maendeleo ya asasi na jamii. Kwa kawaida malengo ya kukuza uwezo katika ngazi hii yamelenga kutoa mafunzo yaliyojikita katika kukuza ujuzi wa wafanyakazi na wana-AZAKI.
  • Asasi/Mashirika: FCS inatambua kuwa mahitaji mengi ya asasi ni zaidi ya ukosefu wa rasilimali na ujuzi. Kwahiyo, tunafanya mchakato wa kina wa ki-shirika wa kuongeza hamasa na kuchochea mabadiliko ya asasi. Mchakato huo unafanywa kwa njia ambayo umiliki wa mchakato wa mabadiliko umewekwa mikononi mwa asasi husika.
  • Mtandao wa asasi, Harakati na Jumuiya: Msaada wa kujenga na kuendeleza wa uwezo kwenye ngazi hizi unatilia mkazo makundi fulani fulani ya asasi, kwahiyo kuna usawa na maslahi ya pamoja miongoni mwa sekta mbalimbali. Lengo ni kuimarisha uwezo sanjari na maeneo maalum yenye maslahi ya pamoja na uboreshaji wa makundi hayo. Mkazo mkubwa zaidi umejikita kwenye kukuza uwezo wa kimahusiano, kwa lengo la kuimarisha sauti ya pamoja na wasifu wa makundi hayo maalum ya wadau na watendaji wa kijamii.

Kujenga uwezo wa kisekta

Katika ngazi hii, unalenga sekta nzima ya asasi za kiraia badala ya asasi moja moja. Ujenzi wa wezo katika eneo hili unatazama mahitaji ya pamoja ya sekta nzima ya asasi za kiraia na jinsi ya kuimarisha sekta hii. Mkazo mkubwa unawekwa katika kubainisha malengo ya sekta hii na heshima na umuhimu wake kwa maendeleo

FCS inajengaje uwezo kwa taasisi?

Katika kujenga uwezo wa kisekta, FCS inatumia mbinu na staili mbalimbali za kujifunza zikiwemo kuwezesha taasisi kujitathimini, mafunzo ya ana kwa ana, kutoa msaada wa kitaaluma katika kuandaa sera na miongozo ya taasisi husika, warsha zinazohusisha wadau muhimu wa taasisi na ushauri elekezi, mabadiliko katika utawala na ukuaji wa taasisi, kubadilishana uzoefu kupitia majukwaa, semina na mikutano, safari za kujifunza kwa wadau wengine, usimamizi kwa vitendo na utoaji wa maelekezo kwa vitendo, tafiti na uchambuzi na upashanaji wa taarifa.