KUJENGEA UWEZO

 

KUJENGEA ASASI UWEZO

Shughuli za kuzijengea uwezo asasi za kiraia ni mojawapo ya nguzo kuu za FCS katika kuitekeleza dira yake katika kutoa huduma kwa wananchi. Katika muktadha wa kuzijengea uwezo asasi, lengo kuu la FCS ni kuhakikisha kuwa asasi zimejengewa uwezo  ii ziweze kutekeleza miradi inayotoa matunda yanayotarajiwa na kuweka kumbukumbu za mafanikio hayo ili kuwashirikisha wengine kufahamu mbinu na matokeo ya miradi hiyo. Tunaamini kuwa ujengeaji uwezo wa asasi ni muhimu katika kuwapatia watu sauti  na kuwafanya kuwa muhimili katika utawala bora, kujikimu na maendeleo ya kiuchumi ambayo nisehemu ya maisha. Shughuli za kuzijengea uwezo asasi zinalenga katika kuinua na kuimarisha kiwango cha utendaji wa taasisi na uhusiano wa ukuaji huo na wafanyakazi wake.

 

FCS inajenga uwezo gani?

FCS inaitazama asasi katika mrengo wa kimfumo ambapo shughuli, matukio na nguvu mbalimbali za taasisi husika hazitenganishwi bali zinahusiana. Kutokana na mtazamo huu, shughuli za kuzijengea uwezo asasi zimeegemea katika nguzo kuu tatu za Uwezo wa KUWEPO, uwezo wa KUFANYA na uwezo wa MAHUSIANO

 

Uwezo wa Kuwepo

Aina hii ya uwezo inahusisha uwezo wa kitaasisi kutenda kwa umahiri kama asasi inayojisimamia yenywe. Katika eneo hili, asasi zitawezeshwa kutengeneza miundo imara ya kiuongozi na kiutawala yenye mikakati madhubuti. Asasi zinawezeshwa kujifanyia tathmini ili kubaini mapungufu na mahitaji ya kiuwezo.

 

Uwezo wa Kufanya

Hapa, FCS inazijengea uwezo asasi ili ziweze kuwafikia wananchi wengi katika utekelezaji wa miradi katika sekta za kujikimu na utawala. Miongoni mwa shughuli  zinazofanywa na FCS katika aina hii ya uwezo ni kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya usimamizi wa miradi, uweledi na ufundi katika Ufuatiliaji wa Miradi ya Umma na Uwajibikaji wa Miradi ya Umma, kuzuia Ukatili wa kijinsia , utetezi wa haki kwa watu wenye ulemavu na ushiriki wa wananchi katika michakato ya kidemokrasia.

 

Uwezo katika kuhusiana

Katika ujenzi wa mahusiano, lengo ni kuziwezesha asasi kuimarisha mahusiano baina ya asasi na asasi au taasisi nyingine. Lengo kuu la aina hii ya ujenzi wa uwezo ni kuziwezesha asasi kujenga mahusiano, ushirikiano, mshikamano na mtandao kama njia ya kupanua shughuli za asasi na kuwafikia walengwa wengi na matokeo makubwa zaidi.

 

FCS inajenga uwezo wa nani?  

Ikiwa na jukumu kubwa la kuzilea na kuzihudumia asasi za Tanzania, FCS ina lengo la kutoa huduma za ujenzi wa uwezo kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo:

  • Mtu mmoja mmoja: Kama viongozi na wafanyakazi wa asasi, wananchi wakiwemo wanawake, vijana, watunga sera na viongozi mbalimbali wa serikali. FCS inatambua kuwa mabadiliko kuanza kutokea kwa mtu mmoja mmoja na kisha katika hatua za pamoja. Kadhalika, mabadiliko ya mtu mmoja mmoja yanapelekea kuwepo kwa maendeleo ya kijamii.  Kwa kawaida, madhumuni ya kujenga uwezo katika hatua hii ni kutoa mafunzo ya kuimarisha stadi kwa wafanyakazi na wanachama wa asasi.
  • Asasi: FCS inatambua kuwa mahitaji muhimu ya asasi ni zaidi ya rasilimali na uwezo wa wafanyakazi wake.  Kutokana na mtazamo huu, tunaingia kwa undani katika kubaini hasa mambo mbalimbali yanayohitajika na asasi ili iweze kuwa yenye tija. Njia zinazotumika katika kujenga uwezo wa kitaasisi ni pamoja na kuhakikisha kuwa wadau wa asasi husika ndio wanakuwa wahusika wakuu wa kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
  • Taasisi za kimtandano na mjumuiko: Msisitizo wa kujenga uwezo katika ngazi hii unalengo vikundi na mitandano yenye madhumuni na mwelekeo unaoshabihiana kisekta. Lengo la ujenzi wa uwezo kwa makundi na mitandano hii ni kuiwezesha kuleta mshikamano, umoja na kuwa na sauti ya pamoja.

 

Kujenga uwezo wa kisekta

Katika ngazi hii, unalenga sekta nzima ya asasi za kiraia badala ya asasi moja moja. Ujenzi wa wezo katika eneo hili unatazama mahitaji ya pamoja ya sekta nzima ya asasi za kiraia na jinsi ya kuimarisha sekta hii. Mkazo mkubwa unawekwa katika kubainisha malengo ya sekta hii na heshima na umuhimu wake kwa maendeleo

 

FCS inajengaje uwezo kwa taasisi?

Katika kujenga uwezo wa kisekta, FCS inatumia mbinu na staili mbalimbali za kujifunza zikiwemo kuwezesha taasisi kujitathimini, mafunzo ya ana kwa ana, kutoa msaada wa kitaaluma katika kuandaa sera na miongozo ya taasisi husika, warsha zinazohusisha wadau muhimu wa taasisi na ushauri elekezi, mabadiliko katika utawala na ukuaji wa taasisi, kubadilishana uzoefu kupitia majukwaa, semina na mikutano, safari za kujifunza kwa wadau wengine, usimamizi kwa vitendo na utoaji wa maelekezo kwa vitendo, tafiti na uchambuzi na upashanaji wa taarifa.