Historia Yetu

 

Foundation for Civil Society (FCS) ni taasisi huru ya kitanzania isiyo ya kiserikali wala ya kibiashara, inayoshirikiana na wadau wa maendeleo katika kuwezesha asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) nchini. FCS inatoa ruzuku na kuzijengea uwezo asasi za kiraia (AZAKI) ili kuimarisha utendaji wao na kuwawezesha wananchi washirki kikamilifu katika shughuli za kupunguza na kuondoa umaskini nchini Tanzania. FCS ilisajiliwa Septemba 2002 na kuanza shughuli zake Januari mwaka 2003. Taasisi hii inaongozwa na Bodi huru na kufadhiliwa na Wadau wa Maendeleo.


 

Kazi kubwa ya FCS ni kutoa ruzuku na kuzijengea uwezo Azaki. Kwa kutumia ruzuku, tunaziwezesha Azaki kujiimarisha na kukuza ushirikiano wa kimaendeleo na kujengea uwezo ili kuleta mabadiliko endelevu ya kijamii na kiuchumi. FCS ni taasisi rafiki miongoni mwa taasisi chache zinazotoa ruzuku kwa azaki hapa nchini. Tunatoa ruzuku kwa Azaki changa ambazo katika hali halisi isingewezekana kupewa ruzuku.

 

FCS imetoa mchango mkubwa katika kuikuza na kuiendeleza sekta ya asasi za kiraia hapa nchini na hivyo kwa njia moja au nyingine kuziwezesha Azaki na wananchi kuwa muhimili mkuu wa kuleta mabadiliko chanya ya utawala wa kidemokrasia nchini Tanzania na ubora wa maisha kwa watu wote.